Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-07 15:46:49    
China inayopenda kutetea haki kwa ajili ya nchi za Afrika katika mambo ya kimataifa

cri

Mkutano wa 7 wa wakuu wa Umoja wa Afrika tarehe 1 Julai ulifanyika huko Banjul, mji mkuu wa Gambia, ujumbe wa serikali ya China ulihudhuria mkutano huo kama mchunguzi. Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, ofisa wa wizara ya mambo ya nje ya China anayeshughulikia mambo ya Afrika alisema, China itaendelea kutetea haki kwa ajili ya nchi za Afrika katika mambo ya kimataifa.

Ujumbe wa serikali ya China kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika ni moja ya shughuli za kimkakati kati ya China na Afrika zilizopangwa kufanyika mwaka huu. Mwezi Aprili mwaka huu Rais Hu Jintao wa China alitembelea nchi tatu za Afrika ambazo ni Cameroon, Nigeria na Kenya. Mwezi Juni mwaka huu, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alitembelea nchi saba za Afrika ambazo ni Misri, Angola, Ghana, Afrika ya kusini, Kongo Brazaville, Tanzania na Uganda. Mwezi Novemba mwaka huu, mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika unatazamiwa kufanyika hapa Beijing. Mawasiliano ya mara kwa mara ya viongozi wa ngazi ya juu kati ya China na nchi za Afrika yanaonesha kuwa, ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Afrika umefikia kwenye kiwango kipya.

Mkurugenzi wa ofisi inayoshughulikia utafiti kuhusu mambo ya Afrika katika Taasisi ya uhusiano wa Kimataifa ya China Bwana Xu Weizhong alisema, nchi zinazoendelea zinapaswa kuungana ili kuhimiza uhusiano wa kimataifa uendelee kwa njia ya kidemokrasia, kuzihimiza nchi zilizoendelea kutilia maanani zaidi maslahi ya nchi zinazoendelea, na kuhakikisha nchi zinazoendelea zinakuwa na hadhi zinazostahili katika dunia yenye ushindani mkali.

Kutokana na uungaji mkono wa nchi zinazoendelea zikiwemo nchi za Afrika, mwaka 1971China ilirudishwa kiti halali kwenye Umoja wa Mataifa. Kuanzia miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana na uungaji mkono wa nchi za Afrika na nchi nyingine zinazoendelea, mara 13 China ilikanusha pendekezo la ati "Taiwan irejeshwe kwenye Umoja wa Mataifa", na kuishinda mara 10 njama ya utawala wa Taiwan kujaribu kujiunga na Shirika la Afya Duniani WHO, na kushinda mara 11 pendekezo la kuipinga China lililotolewa na nchi za magharibi kwenye mkutano wa kamati ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alipoizuru Misri alisema, watu wa Afrika wameitendea mema China, na wachina kamwe hawatasahau fadhila walizotendewa. Hivyo serikali ya China siku zote inaunga mkono nchi za Afrika katika mambo ya kimataifa. Kwa mfano kuhusu suala la haki za binadamu serikali ya China inapinga kithabiti vitendo vya kuingilia kati mambo ya nchi nyingine kwa kisingizio cha haki za binadamu, na kushirikiana vizuri na nchi za Afrika na kuziunga mkono nchi za Afrika kadiri iwezekanavyo.

Ofisa wa wizara ya mambo ya nje ya China alisema, China inatilia maanani maoni ya Afrika katika mambo yanayozihusu nchi za Afrika, na kuunga mkono mapendekezo na misimamo ya nchi za Afrika, inatetea kuwa maslahi halali ya nchi za Afrika yanapaswa kuheshimiwa ipasavyo.

Masuala mengi yaliyothibitishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yalihusiana na nchi za Afrika. China mara nyingi inatumia fursa za kuwa mwenyekiti wa baraza hilo kuielekeza jumuiya ya kimataifa kufuatilia amani na maendeleo ya nchi za Afrika. Kuhusu suala la mageuzi ya Umoja wa Mataifa, China siku zote inatetea kuwa, upanuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unapaswa kuzingatia kwanza uwakilishi wa nchi zinazoendelea hasa nchi za Afrika, na kwenye mazungumzo ya Shirika la Biashara Duniani, China inajitahidi kulinda maslahi ya Afrika na kudai kupunguza ruzuku za mazao ya kilimo, kupunguza ushuru wa forodha, kufungua zaidi soko kwa mazao ya kilimo ya nchi zinazoendelea na kupunguza vizuizi vya kuhamisha teknolojia.

Mtafiti wa mambo ya Afrika Bi. He Wenping alisema, China inaunga mkono amani na maendeleo ya Afrika, pia pamoja na juhudi zinazofanywa na nchi za Afrika na jumuiya ya kimataifa katika kutatua migogoro, na kulinda amani na utulivu wa kikanda, pia inaziunga mkono nchi za Afrika kutekeleza mpango wa ushirikiano mpya wa maendeleo ya uchumi kwa Afrika NEPAD, ili kuleta utulivu na maendeleo endelevu barani Afrika.

China siku zote inatetea kutatua migogoro ya wenyewe kwa wenyewe na kati ya nchi na nchi kwa kufanya mazungumzo. Ili kuunga mkono Umoja wa Afrika ufanye kazi ya kulinda amani, mwaka 2005 na mwaka 2006 serikali ya China iliupatia Umoja huo msaada wa dola za kimarekani laki nne kila mwaka, ili kusaidia harakati zake za ulinzi wa amani kwenye sehemu ya Darfur nchini Sudan. Serikali ya China pia ilituma vikosi vya kulinda amani kutekeleza majukumu ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani barani Afrika.

Serikali ya China pia inaunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika za kujitahidi kuujenga umoja huo, kuanzia mwaka 2000 kila mwaka inaupa umoja huo msaada wa fedha taslimu dola za kimarekani laki tatu. Hivi sasa China imetuma wajumbe wake kwenye Jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

Msaada wote wa hali na mali unaotolewa na China kwa nchi za Afrika unatokana na msingi wa kuheshimiana, kuwa na usawa na kunufaishana na kutoingilia kati mambo ya nchi nyingine. Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alipofanya ziara barani Afrika alisistiza: "China inaunga mkono ujenzi wa utawala wa kisheria na kidemokrasia wa Afrika, lakini China hailazimishi hata kidogo watu wengine wakubali nia yake. Tunaamini kuwa, watu wa sehemu na nchi yoyote wana haki na uwezo wa kushughulikia mambo yao wenyewe. Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuheshimu njia ya maendeleo inayochaguliwa na nchi za Afrika."

Mwaka 2006 ni mwaka wa maadhimisho ya miaka 50 tangu China na Afrika zianzishe uhusiano wa kibalozi. Mwanzoni mwa mwaka huu, serikali ya China ilitoa waraka wa sera ya China kwa Afrika, ikieleza kuanzisha uhusiano mpya wa kimkakati na kiwenzi na nchi za Afrika kwenye msingi wa kuwa na usawa na uaminifu kisiasa, kufanya ushirikiano wa kunufaishana kiuchumi, kufanya maingiliano na kufundishana kiutamaduni.

Kabla ya kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika, mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bwana Alpha Konare alikutana na mkuu wa ujumbe wa serikali ya China, ambaye pia ni balozi wa China nchini Zambia Bwana Li Baodong. Bwana Konare alisifu ufuatiliaji wa China katika kazi za Umoja wa Afrika na uungaji mkono wa serikali ya China katika juhudi za kuleta amani na maendeleo barani Afrika.

Kuimarisha mshikamano na ushirikiano kati ya China na bara la Afrika lenye nchi 53 na idadi ya watu milioni 800 siku zote ni sehemu muhimu ya sera ya kidiplomasia ya China. Serikali ya China itaendelea kuunga mkono nchi za Afrika kwenye jukwaa la kimataifa ili kutetea maslahi ya Afrika.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-07