Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-11 15:43:31    
Barua 0709

cri

Katika wiki zilizopita tuliwaletea kipindi maalum cha Shindano la Chemsha bongo kuhusu Mimi na Radio China kimataifa, tunaimani kuwa wasikilizaji wetu wengi wamesikiliza makala 4 tulizowasomea katika kipindi hiki. Na mpaka leo tumepata majibu kutoka kwa wasikilizaji wetu kadha wa kadha, na tunatarajia kuwa hivi karibuni tutapata majibu mengi kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Shinyanga Tanzania ametuletea jibu lake kuhusu chemsha bongo hilo, ambapo amesema akitumai kwamba tutaendelea kushirikiana na kuwasiliana mara kwa mara, kukuza na kuimarisha urafiki na uhusaino kati yetu na wasikilizaji wetu. Angependa sana kushiriki na kuhudhuria sherehe ya maadhimisho ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa Radio China kimataifa, ambayo ni radio kubwa kabisa hapa duniani.

Tunamshukuru sana na kufurahishwa na jibu lake la chemsha bongo, kwani siku nyingi hatujapata barua yake, lakini tunadhani hii ni kutokana na kazi zake kuwa, tunakubaliana naye kuwa tungedumisha mawasiliano na urafiki kati yetu, na matumaini yetu kuwa, Bwana Kulwa ataendelea kutuletea barua mara kwa mara, tunatumai ataendelea kutoa maoni na mapendekezo yake ili kutusaidia kuboresha vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Consolata W. Mang'ara wa sanduku la posta 5088 Nairobi Kenya ametuletea jibu la shindano la chemsha bongo kuhusu "Mimi na Radio China kimataifa" pamoja na shairi moja fupi, shairi lake linasema hivi:

Inapotimiza sitini na tano miaka,

Radio China kimataifa, mengi kujivunia,

Ulimwenguni kusikika, na hata mashariki Afrika,

Habari motomoto kutujuza, pia tamaduni za kichina.

Je! Kunayo idhaa, kama Radio China kimataifa Afrika?

Ingine hakuna, toka bara Asia,

Inayotangaza, kwa tofauti lugha,

Kiswahili, hata kiingereza,

Kivietnam, hata kiindonesia,

Je! Kunayo idhaa, kama Radio China kimataifa Afrika?

Inavutia, mithili ya ua waridi,

Nyimbo za kuvutia, za kichina na Afrika,

Watangazaji wake, wenye sauti za kuvutia,

Mpangilio mwafaka, na vipindi elimisha.

Je! Kunayo idhaa, kama Radio China kimataifa Afrika?

Kituo cha FM kuanzisha, Afrika mashariki-Kenya,

Kuleta Daraja la urafiki, kati ya China na Afrika,

Pia mafundizo elimisha, ya lugha ya kichina,

Basi hadi tamati, nawauliza wenzangu Afrika,

Je! Kunayo idhaa, kama Radio China kimataifa Afrika?

Na msikilizaji wetu Benjamin Bongoman Mwana wa Nanjero wa sanduku la posta 2001, Nakuru, Kenya ametuletea barua akieleza furaha nyingi kutoka kwake na hata kwa mkewe Rose Mutonyi ambaye ni mpenzi wa Radio China Kimataifa.

Anasema kwanza anatushukuru kwa kazi yetu nzuri ya kuwaeleza mambo yanayotokea nchini China. Hayo ni matukio ambayo walikuwa hawafahamu kama yanatokea nchini China. Pia anasema picha ambayo alipata ya ukuta mkuu wa China ilimfurahisha sana.

Pili anasema , ni kazi nzuri ya kuanzisha kituo cha matangazo ya FM huko Nairobi Kenya. Lakini angeomba wasikilizaji wengi wa CRI wako mbali na Nairobi, pesa zikipatikana, vituo kama hivyo visikike sehemu kama Nakuru, Kisumu, Eledoret, Bungoma, Kisii, ambapo kuna mashabiki wengi wa Radio China kimataifa. Anasema kama akipata nafasi ya kutembelea China angefurahi sana.

Tunamshukuru Bwana Benjamin kwa barua yake, ni matumaini yetu kuwa yeye, mkewe, pamoja na jamaa na marafiki zao wataendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo ya kutusaidia kuboresha vipindi. Pia mkishikilia kushiriki katika shindano la chemsha bongo linaloandaliwa kila mwaka na Radio China kimataifa, mnaweza kubahatika kupata nafasi ya kuja kuitembelea China.

Msikilizaji wetu Ally Omar Seif Mlindo, Pandani, Wete -Pemba sanduku la posta 114 Tanzania ametuletea barua akianza kwa kutusalimu. Anasema yeye ni mzima, na anaendelea kuisikiliza idhaa yetu ya Kiswahili ya radio China Kimataifa. Anasema mwaka huu ameyapata mafanikio mengi ndani ya matangazo ya Radio China Kimataifa, hasa kutokana na mpangilio mzuri wa vipindi kuimarika vizuri sana.

Zaidi ya hayo anatoa shukurani zake kwa wahusika wote wa CRI kwa kuweza kupokea maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wake, na kuweza kuwaongezea muda wa saa moja badala ya nusu saa. Anasema anashukuru kwa hilo. Kwa hivyo anapenda kurudia tena na maoni yake pamoja na mapendekezo. Ingawa marekebisho mazuri tayari yamefanyika, lakini anaomba kama mabadiliko yatafanyika tena, ikiwezekana kianzishwe kipindi cha yasemavyo magazeti nchini China na kipindi cha Daraja la Urafiki kipewe muda wa japo dakika 2o kwa sababu kimemvutia sana. Pia anatuomba jina lake tuliweke ndani ya jarida la Daraja la Urafiki.

Amaliza barua yake kwa kutuomba tumjulishe kama tayari tumechapisha jarida la daraja la urafiki, na kama tayari anaomba tumtumie jarida hilo. Anatutakia kazi njema yenye mafanikio na afya njema na viongozi wa nchi ya China.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Ally Mlindo kwa barua yake na tunapenda kumwambia kuwa hatuwezi kumsahau, mawasiliano kati yetu yataongezeka siku hadi siku, na tunamuomba tafadhali asubiri, kwani katika miezi kadhaa iliyopita, tulikuwa na kazi nyingi kweli, hivyo mpaka sasa bado hatujachapisha jarida dogo la Daraja la urafiki, tutajitahidi. Tunaomba radhi mbele ya wasikilizaji wetu wanaopenda jarida hilo.

Na msikilizaji wetu Hassan Kipkerich wa Nairobi Kenya ametuletea shairi lake lisemalo:

Mheshimiwa rais wa Jamhuri ya watu wa China Hu Jintao

Karibu kwetu

Jamii zetu tu wandugu,

Ifurahie Kenya yetu

Kwa shangwe twakulaki.

Wakenya twakuheshimu,

Twatambua nyingi hisani

Shukrani twatoa kwa serikali ya China

Misaada twazipokea

Elimu twanufaika nayo

Biashara imeshamiri

Utamaduni twabadilishana

Mazingira twafundishana

Habari za China twazipokea

Utalii umeimarika

Yote twajivunia

Wakenya twatoa shukrani uzipokee.

Nafika kikomo kwa kumpongeza balozi

Heko balozi heko ubalozi

Juhudi mmefanya uhusiano umeimarika

Mwito natoa na Wakenya tunatoa

Juhudi tuzidishe, uhusiano tuimarishe

Utalaamu tubadilishane, biashara tuzidishe.

Namaliza kwa salaam kwa wandugu wa Jamhuri ya watu wa China.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-11