
Waziri mkuu wa Iraq Bw. Nuri al-Maliki tarehe 10 alipotoa hotuba katika bunge la sehemu ya Kurd iliyoko kaskazini mwa Iraq, alitoa wito wa kutaka wairaq waungane na kuvunjilia mbali tishio la ugaidi na njama ya kuirudisha Iraq katika "zama za giza".
Waziri mkuu Maliki alitoa wito huo baada ya matukio ya umwagaji damu kutokea nchini Iraq katika siku 3 zilizopita kutokana na mapambano kati ya madhehebu ya kidini nchini humo. Tarehe 10 kiasi cha watu 30 walikufa katika mapambano hayo, yaliyotokea wakati mji wa Sadr wanaokaa waislamu wa madhehebu ya Shia ulioko sehemu ya kaskazini mashariki mwa Baghdad uliposhambuliwa mara 2 kwa mabomu, ambapo watu 12 walipoteza maisha na wengine 62 walijeruhiwa. Huko ni mahali lililoko "Jeshi la Mehdi" linaloongozwa na madhehebu ya Shia lenye msimamo mkali wa kisiasa. Mashambulizi hayo mawili yanachukuliwa ni vitendo vya kulipiza kisasi dhidi ya wanamgambo wa Sadr, ambao wanatuhumiwa kuwaua waislamu wa madhehebu ya Sunni.

Mapambano hayo kati ya madhehebu ya Shia na Sunni yalizuka tarehe 8 mwezi huu. Siku hiyo msikiti mmoja wa madhehebu ya Shia ulioko mjini Baghdad ulishambuliwa, na kusababisha watu wawili kupoteza maisha yao na wengine 19 kujeruhiwa. Jeshi la madhehebu ya Sunni linaloipinga Marekani pamoja na wanamgambo wa madhehebu ya Shia wanachukuliwa kuwa ni waanzilishi wa mashambulizi ya kisilaha. Sera za jeshi linaloipinga Marekani la Sunni, ambalo nguvu zake muhimu ni Kundi la al Qaeda, ni kushambulia misikiti ya madhehebu ya Shia na waumini wa madhehebu hayo, kuchochea mapambano ya madhehebu na kukwamisha mchakato wa kisiasa nchini Iraq. Baada ya kiongozi wa kundi la al Quid Abu Musab al-Zarqawi nchini Iraq kuuawa, kulikuwa na watu waliodhani kuwa huenda kundi hilo litabadilisha sera zake na kukusanya nguvu zake kulishambulia jeshi la Marekani, lakini kundi hilo bado linadhaniwa kuendelea kuchochea mauaji ya kidini.
Jeshi la wanamgambo wa madhehebu ya Shia pia linalaumiwa na kutakiwa kubeba lawama kuhusu mapambano yanayopamba moto siku hadi siku. Naibu katibu mkuu wa chama cha kiislamu cha madhehebu ya Sunni nchini Iraq Ayad Al-Samarrai tarehe 9 alililaani vikali jeshi la Mehdi linaloongozwa na Sadr kwa kuwaua watu ovyo. Chama cha Iraqi Accordance cha madhehebu ya Suni kinataka serikali ilivunje jeshi hilo, na kuwanyang'anya silaha askari wa jeshi hilo na kuwazuia wasiendelee na shughuli zao.
Jeshi la polisi la Iraq linashutumiwa kutokuwa haki kuhusu mapambano ya madhehebu, na lilichangia kupamba moto kwa mapambano ya madhehebu. Kiongozi wa chama cha Iraqi Accordance, Adnan al-Dulaimi anawakosoa polisi wa Iraq kuwa ni walinzi wa jeshi la wanamgambo, ambalo kwa kiasi fulani lilianzisha mauaji ya kikabila.
Wachambuzi wanasema ingawa mwezi uliopita Bw Maliki alitoa mpango wa usuluhishi wa kitaifa, lakini mpango huo haukutaja suala la ratiba ya kuondoka kwa jeshi la Marekani, ambalo linafuatiliwa sana na watu, wala haukutoa mapendekezo na hatua kamili kuhusu kuwaachia huru wanamgambo wanaoipinga Marekani wa madhehebu ya Sunni pamoja na kuvunja jeshi la wanamgambo. Kutokana na kukabiliwa na kupamba moto kwa mapambano kati ya madhehebu ya kidini, kazi za haraka kwa Bw Maliki ni kuimarisha usalama wa nchi na kuboresha mpango wa usuluhisho wa kitaifa ili kuiwezesha Iraq ielekee kwenye amani ya kudumu kwa hatua madhubuti.
Idhaa ya Kiswahili 2006-07-11
|