Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-12 16:01:46    
Kampuni ya Mcmillan nchini Kenya

cri

Kampuni ya Mcmillan nchini Kenya ilianza 1971, ikiwa ni kituo cha usambazaji wa vitabu vya kampuni kubwa ya Mcmillan duniani, hivi sasa imekuwa kampuni kubwa ya kitaalamu kwa uchapishaji nchini Kenya. Kampumi ya Mcmillan inatarajia kuwa kampuni itakayotoa vitabu vilivyofanyiwa uchunguzi wa kutosha bila kuwa na makosa ya aina yoyote na vitakavyouzwa kwa bei nafuu, ili kuwawezesha wakenya wengi waweze kuvinunua kwa urahisi.

Zaidi ya kuchapisha vitabu na vifaa vingine vya mashuleni vya hali ya juu, kampuni ya Mcmillan inasadia jamii kwa njia nyingine mbalimbali. Njia mojawapo ni kuandaa semina na warsha mbalimbali kwa walimu na kuwafundisha namna ya kutumia vitabu vya Mcmillan na njia bora zaidi ya kufuata mitaala ya masomo mashuleni, jinsi ya kufundisha vizuri na kwa ufanisi na namna ya kutumia pesa katika shule zao. Bwana Mwazemba alisema pamoja na kuwa kampuni yao ya Mcmillan ni kampuni ya kibishara inayotaka kupata faida, lakini haisiti kutoa misaada kwa jamii ya Kenya, kwa mfano kampuni imeamua kukuza lugha ya Kiswahili kwa kuchapisha vitabu vya hadithi, riwaya na tamthiliya kwa wanafunzi, hali ambayo imechangia kujenga na kuongeza tabia ya watoto kupenda kusoma. Pia kampuni ya Mcmillan hutoa misaada ya vitabu mashuleni ambapo imeshawahi kutoa msaada ya vitabu katika shule za Upili,shule za sekondari na katika maktaba ya taifa ya Kenya. Kampuni hiyo pia hutoa msaada wa kuwalipia gharama za masomo baadhi ya wanafunzi ambao wapo chini ya kampuni hiyo, kwa mfano kwa hivi sasa kampuni inawalipia ada za masomo wanafunzi 30.

Katika mwaka huu wa 2006 kampuni ya Mcmillan imeshachapisha vitabu vya hadithi za watoto ambazo ni za kwanza, zinaitwa hadithi changamka, mpaka hivi sasa vimeshafika vitabu 10, kitabu cha kwanza kinaitwa zawadi ya salimu, pia kuna haki ya Ruto vilivyoandikwa na A.Yamtuku ambaye ni mwandishi chipukizi lakini hodari katika hadithi za watoto.

Pia kuna kuna kisa cha peremende kilichoandikwa na David Mairu ambaye ni mwandishi gwiji nchini Kenya, ukiangalia hapa utaona kuwa kampuni yetu inajaribu kuwaleta pamoja waandishi wa vitabu wachanga na wale waliobobea katika uandishi.Vitabu vingine ni paka na panya, kuku na mayai ambavyo vimeandikwa na Frolence Nyakeri. Pia kuna vitendo vya jamila, matu atunzwa na barua ya maisha ambavyo vimeandikwa na Bwana Hezron Mugambi.Kwa hiyo tumeanza na vitabu 10 na vingine viko njiani vinakuja.

Bwana Mwazemba amesema si kama kampuni ya Mcmillan imeaza kuchapisha vitabu mwaka huu tangu ilipoanza shughuli zake nchini Kenya, ila hii mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuanza kuchapisha vitabu kwa mfululuzo. Miaka iliyopita walikuwa wanachapisha vitabu vya kiswahili lakini sio kwa mfululizo, kwa mfano labda kwa mwaka mmoja kitabu kimoja,kampuni imeshachapisha vitabu kadhaa vya kiswahili miaka iliyopita kama vile Hekaya za Abunuasi, lakini sasa kampuni hiyo imeamua kuanza kuchapisha kwa mfululuzo kwa sababu kiswahili bado kina vitabu vichache sana ikilinganishwa na kiingereza.

Pia kiswahili ni lugha inayokua hivi sasa, hivyo kampuni kama ya Mcmillan ina wajibu wa kukisaidia kiswahili kikue na kupanuka zaidi, na tatu wao kama wachapishaji lengo sio faida tu, bali pia kutoa maadili mema kwa jamii kama vile kutoa mafundisho kuhusu ukimwi au mazingira kwa njia rahisi ya hadithi ambako kutainufaisha jamii nzima. Pia ili kujenga mazingira ya watoto kukua huku wakiwa na mazoea ya kusoma ni lazima wawe na vitabu vya kusoma.

Kuhusu usomaji wa vitabu vya kiswahili nchini kenya, Bwana Mwazemba amesema, usomaji wa vitabu vya kiswahili nchini bado sio mkubwa sana na pia unakabiliwa na vikwazo vingi, kwa mfano baadhi ya wakuu wa shule huwazuia wanafunzi kuongea kiswahili, na huwaruhusu kufanya hivyo wakati wanapofundishwa somo la kiswahili, hivyo wanafunzi hupaswa kuongea kingereza kwa muda mwingi,na hili ni tatizo kubwa.

Bwana Mwazemba ametoa changamoto kwa waandishi wa vitabu kuandika mambo muhimu yanoigusa jamii kama vile ukimwi, dawa za kulevya na mazingira na kuyaandika katika lugha inayoeleweka na itakayoweza kumfundisha mtoto.

Bwana Mwazemba amemaliza kwa kuwataka wasomaji wa hadithi za kiswahili na wale wanaojifunza kiswahili wakae tayari kwani kampuni ya Mcmillan inawatayarishia vitabu vingi vya hadithi, riwaya, tamthilia ambavyo viko mbioni kutoka.

Idhaa ya Kiswahili 2006-07-12