Mabomu 7 yalilipuka ndani ya magarimoshi yaliyokuwa njiani jioni ya tarehe 11 huko Mumbai, mji mkubwa wa kwanza kibiashara nchini India, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 170 na wengine mamia kujeruhiwa. Serikali ya India imethibitisha kuwa tukio hilo ni mashambulizi ya kigaidi.
Jioni ya tarehe 11 majira ya saa 12, bomu lililowekwa ndani ya garimoshi lililojaa abiria lilipuka kwanza karibu na kituo cha Khar, kaskazini magharibi mwa Mumbai. Katika muda wa zaidi ya nusu saa baada ya hapo, magarimoshi mengine 6 yaliyokuwa njiani yalikumbwa na milipuko ya mabomu. Mabomu hayo yalikuwa na nguvu kubwa na yote yaliwekwa ndani ya behewa la daraja la kwanza.
Milipuko ya mabomu ilisababisha tafrani kubwa kwenye magarimoshi yaliyokumbwa na mashambulizi na vituo vilivyo karibu. Mjini Mumbai, huduma za simu na simu za mkononi zilisimamishwa kutokana na idadi kubwa ya watu waliojaribu kuwasiliana na jamaa na marafiki zao. Hospitali zote zilijishughulisha kuwaokoa watu waliojeruhiwa. Idara ya reli ya mji huo ilifunga huduma za reli kote mjini, na kuwataka wananchi wasikaribie vituo vya magarimoshi. Polisi ya Mumbai pia iliimarisha ulinzi katika majengo makubwa, viwanja vya ndege na mahekalu. Serikali ya India ilitangaza hali ya tahadhari kubwa katika mji mkuu New Delhi, na Bangalore unaojulikana kama silicon valley nchini India, na sehemu zote nyeti nchini humo. Waziri mkuu wa India Bw. Manmohan Singh aliwaomba wananchi watulie.
Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani wa India Bw. Shivraj Patil, vyombo vya upelelezi viliwahi kupata habari kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi, lakini vilishindwa kuthibitisha tarehe na mahali pa mashambulizi hayo kutokea. Habari nyingine zilizopatikana kutoka kwa maofisa wa polisi ya Mumbai zilisema, polisi iliwahi kukamata mabomu katika miji kadhaa iliyopo karibu na Mumbai, na kwa maoni ya polisi, ofisi ya uongozi ya kundi la kigaidi ipo katika sehemu fulani mkoani Maharashtra, uliko mji wa Mumbai.
Usiku wa tarehe 11, waziri mkuu wa India Bw. Singh aliitisha mkutano wa dharura uliowashirikisha waziri wa mambo ya ndani, wasaidizi wa mambo ya usalama wa taifa na makatibu wakuu wa mambo ya ndani. Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo inasema milipuko mbalimbali ya mabomu iliyoikumba Mumbai imewashutusha watu, na magaidi ni watu waliohusika na matukio hayo.
Mumbai ni mji mkuu wa mkoa wa Maharashtra, nchini India. Mji huo una wakazi wapatao milioni 17, na kuna bandari kubwa kabisa ya India. Mji huo ni mji mkubwa wa kwanza kibiashara na mji muhimu wa mawasiliano nchini India, unajulikana kama mji mkuu wa kifedha wa India na mlango wa magharibi wa nchi hiyo. Reli ya mji wa Mumbai inaunganisha eneo la biashara lililoko kusini mwa mji huo na eneo la ofisi za serikali pamoja na eneo la makazi lililoko kwenye kitongoji cha kaskazini. Magarimoshi ni chombo muhimu cha mawasiliano cha wakazi wa Mumbai, ambao watu milioni 6.5 wanasafiri kwa magarimoshi. Wakati wa pilikapilika nyingi za kusafiri kwa kawaida kila garimoshi linabeba abiria elfu 4 na mia 7.
Wachambuzi wanasema kutokana na kutokuwa na ukaguzi mkali wa tiketi katika vituo mbalimbali vya magarimoshi mjini Mumbai, hali hiyo ilitoa fursa kwa magaidi kufanya mashambulizi. Na walilipua mabomu jioni wakati watu wengi walipokuwa kwenye magarimoshi wakirudi nyumbani, lengo lao ni kuhatarisha usalama wa jamii ya Mumbai, kuathiri sura ya mji huo kwa wawekezaji duniani ukiwa mji mkubwa wa kwanza wa India, na kuharibu maendeleo ya uchumi wa India. Wachambuzi pia wamesema hata hivyo njama yao haitashinda, badala yake itawafanya wananchi wa India waimarishe nia ya kupambana na ugaidi, kulinda utulivu wa jamii na kukuza uchumi wa taifa.
Idhaa ya Kiswahili 2006-07-12
|