Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-13 16:00:45    
Watoto wa kabila la Wapumi waliokosa elimu warudi shuleni

cri

Kabila la Wapumi lina watu wasiozidi elfu 30, ni miongoni mwa makabila madogomadogo yenye watu wachache hapa nchini China. Wapumi wengi wanaishi katika wilaya ya Lanping, mkoani Yunnan, kusini magharibi ya China, ambapo kutokana na umaskini sehemu hiyo haikuwa na shule, na watoto wengi wa kabila la Wapumi walikuwa wanashindwa kupata elimu. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na misaada ya serikali ya China, sekta ya elimu imeboreshwa kwa udhahiri katika maeneo wanakoishi watu wa kabila la Wapumi, ambapo watoto wote waliokosa elimu wamerudi shuleni.

Mkuu wa shule ya msingi ya Ganzhuhe Bw. Xiong Yuwen anatoka kabila la Wapumi, yeye ameshuhudia mchakato wa kuboreshwa kwa sekta ya elimu ya huko.

Asubuhi ya kila siku, Bw. Xiong Yuwen anaamka mapema, kumsaidia mpishi wa shule hiyo kuwaandalia kifungua kinywa wanafunzi wanaokaa mabwenini. Ndani ya kantini ndogo na safi, meza na viti vipya vilipangwa vizuri. Bw. Xiong alisema, "Zana zote zikiwemo meza na viti ni mpya. Kwa jumla kuna seti tatu za meza na viti, watu wanane wanatumia meza moja kwa wakati mmoja na jumla ya watoto 24 wanakula kwenye kantini hiyo."

Hivi sasa shule hiyo ya msingi ya Ganzhuhe ina wanafunzi zaidi ya 150. Wanafunzi wanaoishi mbali na shule wanakaa katika mabweni ya shule. Ili kuwatunza vizuri watoto hao, shule ilianzisha kantini hiyo ndogo. Na hapo awali iliwabidi wanafunzi hao wajigharamie chakula, ambapo jambo la kwanza lililofanywa na watoto wengi baada ya masomo lilikuwa ni kujipikia chakula.

Tatizo la chakula lilikuwa ni moja tu kati ya matatizo mbalimbali yaliyokuwa yanaikabili shule hiyo. Bi. Zhang Min ni mwalimu aliyehamishwa kutoka shule ya wilaya ya Lanping, sasa yeye na walimu wenzake wanafanya kazi katika shule ya Ganzhuhe kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kuhamishwa kwao ni hatua iliyochukuliwa na serikali ya wilaya ya Lanping kwa lengo la kuinua ufundishaji katika shule ya msingi ya Ganzhuhe.

Walimu hao waliohamishwa kutoka wilayani wanawafundisha watoto wa wakulima kwa makini, hali ambayo inamfurahisha sana mkuu wa shule Bw. Xiong Yuwen. Hata hivyo anawaomba radhi walimu hao kutokana na hali duni ya mazingira wanayokaa inayotolewa na shule, ambapo walimu kadhaa wanabidi kukaa katika chumba kimoja kidogo. Mwalimu Zhang Min alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema "Hapa kuna hali duni ya kukaa. Mwanzoni tulipofika, kulikuwa na panya wengi, kiasi kwamba tulipolala usingizi, panya walitembea hapa na pale chumbani kwetu."

Hivi sasa serikali imetenga fedha zaidi, hatua ambayo imeondoa wasiwasi wa mkuu wa shule, ambapo nyumba moja yenye ghorofa mbili sasa inajengwa karibu na shule hiyo kwa ajili ya walimu. Hadi itakapofika mwezi Septemba mwaka huu, walimu wataweza kuhamia katika nyumba mpya. Mkuu wa shule Bw. Xiong Yuwen alisema,  "Kila ghorofa ina vyumba 6, na kila mwalimu atapata chumba kimoja, kwa hiyo hali ya mazingira yao ya kuishi itaboreshwa sana. Walimu kutoka nje wakija kwetu, sina uwezo wa kuwanufaisha na kitu kingine isipokuwa najaribu kuwafanya waridhike na makazi."

Mkuu huyo Bw. Xiong Yuwen mwenye umri wa miaka 57 anaipenda sana shule ya Ganzhuhe, na yeye mwenyewe alihitimu kutoka kwenye shule hiyo. Alikumbusha wakati aliposoma hapa shuleni kwamba, wakati huo kulikuwa na nyumba kadhaa tu zilizojengwa kwa mbao, ambazo siku za joto zilishindwa kukinga mvua na siku za baridi upepo uliingia nyumbani bila kizuizi kikubwa. Bw. Xiong alisema  "Hapa kwetu kuna hali mbaya ya umaskini. Nilichambua sababu kuu ya umaskini, ni kukosa watu waliopata elimu. Wenyeji walizingatia tu ufugaji na kilimo. Kama hali hii itaendelea, tutakuwa watu maskini zaidi bila kuwa na maendeleo yoyote."

Mwaka 1995 Bw. Xiong Yuwen alirudi kwenye maskani yake baada ya kufanya kazi nje kwa miaka mingi, na kuwa mkuu wa shule ya msingi ya Ganzhuhe. Mabadiliko ya shule hiyo yalimtia moyo sana. Alisema "Niliporudi niliona maendeleo ya shule hiyo, wanafunzi kadhaa waliohitimu kutoka shule hiyo ya msingi walifaulu mitihani ya kuingia sekondari na hata vyuo vikuu. Nafurahi sana, natumai vijana wengi zaidi wataweza kujiunga na vyuo vikuu. Hii pia itawanufaisha wakazi wa hapa kwa ujumla."

Sera mpya iliyotolewa na serikali ya China ilimpa moyo mkuu huyo wa shule. Kwa mujibu wa sera hiyo, wanafunzi kutoka familia zenye matatizo ya kiuchumi wanasamehewa ada ya vitabu na kupatiwa ruzuku na serikali.

Yin Zhaoquan mwenye umri wa miaka 13 alilazimika kuacha masomo alipokuwa kidato cha tatu kutokana na familia yake kukumbwa na matatizo ya kiuchumi. Alikuwa anatamani sana kurudi shuleni. Alisema "Nilipumzika nyumbani kwa nusu muhula, ambapo nilisoma vitabu au kuchunga ng'ombe. Wakati huo nilidhani kama ningekuwa na pesa, ningeweza kuendelea na masomo kama wanafunzi wenzangu."

Matumaini ya kijana huyo yalitimizwa kwa haraka. Kwa mujibu wa sera ya serikali, alisamehewa ada ya vitabu na kupata ruzuku ya Yuan 40 kwa mwezi, kiasi ambacho kinamwezesha azingatie masomo. Katika wilaya ya Lanping, wanafunzi wapatao elfu 18 wamenufaika na sera hiyo.

Mkuu wa shule ya msingi ya Ganzhuhe Bw. Xiong Yuwen alieleza imani kubwa kuhusu mustakabali wa shule hiyo. Alisema  "Mpaka hivi sasa hakuna wanafunzi walioacha masomo, hali ambayo inanitia moyo sana. Naamini wanafunzi wangu watakuwa hodari zaidi kuliko mimi."

Idhaa ya kiswahili 2006-07-13