Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-13 15:42:01    
Wanamitindo wa China wanaong'ara kwenye jukwaa la maonesho

cri

Kutembea jukwaani, kuonesha mitindo ya mavazi na kufuatiliwa na kamera, ni kazi ya uanamitindo inayowavutia sana warembo. Katika makala hii, mtasikia maelezo kuhusu wanamitindo kadhaa wa China.

Dada Zhang Yingqian ana urefu wa mita 1.8, nywele ndefu nyeusi na macho maangavu, mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 20 ameonesha sifa maalumu. Msichana huyo anayetoka mkoa wa Liaoning, kaskazini mashariki mwa China alijitokeza na kuwa mshindi katika mashindano ya 6 ya wanamitindo ya China, sasa amesaini mkataba na kampuni moja maarufu ya wanamitindo hapa Beijing.

 Anasema, "Watu husema nina mustakabali mzuri katika fani hiyo, umbo na sura zangu vinaendana na sifa ya mwanamitindo. Ninafaa kuonesha nguo za aina mbalimbali, lakini napendelea kuonesha nguo zenye umaalumu."

Mwanzoni Zhang Yingqian alipofahamishwa kuhusu fani ya uanamitindo alikuwa anasoma katika shule ya sekondari. Wakati huo kulikuwa na mashirika kadhaa ya kutoa mafunzo kwa wanamitindo, ambapo wasichana wengi warembo walishiriki kwenye mafunzo hayo akiwemo Dada Zhang Yingqian. Baadaye alijiunga na shule ya kufundisha wanamitindo, akaanza kufanya kazi ya mitindo.

Hivi sasa nchini China kuna wanamitindo zaidi ya elfu 50 na kampuni za mitindo zaidi ya elfu 5. Kuhusu suali la kwa nini amechagua kazi hiyo, mwanamitindo wa kike Wu Xiaochen alisema bila kujificha, anasema "Wanamitindo maarufu wanaoneshwa mara kwa mara kwenye vipindi vya televisheni, nawaonea wivu, wao ni kama nyota zinazong'ara, na wanafuatiliwa na kamera nyingi kwenye maonesho. Naona nikiwa kwenye jukwaa la maonesho, najiamini zaidi."

Ni kweli wanamitindo wanapaswa kufanya kazi kubwa ili kufanya maonesho yanayovutia. Mwanamitindo Zhang Yingqian alieleza kuwa, inawabidi kufanya mazoezi mbalimbali. Alitoa mfano wa zoezi la kusimama kuwa, anapaswa kusimama kwa muda usiopungua nusu saa huku kisigino, uti wa mgongo na kisogo vyote vikiwa vimeegamia ukutani. Alisema baada ya zoezi la namna hii, kila mara yeye na wenzake wanakuwa wamechoka sana.

Hata hivyo mwanamitindo huyo aliona inambidi akabiliane na shida hizo ili atimize ndoto yake ya maisha.  Anasema "Naona inastahili kazi kubwa, kwa vile jitihada zote nilizofanya hazijapotea, sasa naweza kufanya maonesho jukwaani."

Miongoni mwa wanamitindo wanaume wa China, Wang Hui mwenye umri wa miaka 28 ni mmoja wa wale wanaoongoza. Mbali na kuonesha nguo, pia ameshiriki kwenye maonesho ya bidhaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vito, kompyuta, saa, magari na simu za mkononi. Wasanifu wa mitindo wanasema kijana huyo anatafsiri vizuri mitindo ya bidhaa hizo kwa maonyesho yake.

Wang Hui alimwambia mwandishi wa habari kuwa, aliwahi kushiriki kutengeneza matangazo ya biashara ya televisheni kwenye mlima wa Xiangshan uliopo karibu na Beijing, ambapo alikuwa anaigiza nafasi ya mwanariadha wa mbio za marathon. Wakati huo hali ya hewa ilikuwa ya baridi sana kiasi kwamba halijoto ilikuwa nyuzi 10 chini ya sifuri, na ilimbidi akimbie kwenye njia ya milimani akiwa amevaa fulana na suruali fupi tu, na kazi hiyo iliendelea kwa siku mbili. Kijana huyo alikumbusha akisema, "Mwanzoni niliona si vigumu sana, lakini baada ya muda mfupi niliona kuwa, si rahisi kuendelea na kazi hiyo mpaka mwisho. Usiku niliporudi nyumbani, nilisikia baridi mwili mzima, nasikia ubaridi umeingia mwilini mwangu."

Ingawa kazi hiyo ina ugumu, lakini wanamitindo wanafurahia kazi hiyo inayowaletea mapato. Nchini China wanamitindo wanalipwa vizuri, ambapo mwanamitindo wa kawaida ana mapato ya Yuan elfu 10 kwa mwezi, sawa na dola za kimarekani elfu 1.25. Na wakati wa mapumziko, wanamitindo hao wanakutana na kuburudika kwa pamoja, kwa mfano kula chakula kwenye migahawa na kuimba nyimbo kwa pamoja.

Kama mnavyojua, wanamitindo wanategemea ujana. Basi vijana hao watakuwaje katika siku zijazo? Wanamitindo wenye umri mkubwa zaidi wameanza kuandaa mpango kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Bw. Wang Hui alisema anapenda sekta ya mitindo baada ya kujiunga na sekta hiyo kwa miaka mingi, siku za baadaye hatafanya kazi ya uanamitindo, lakini hataiacha sekta ya mitindo.

Wanamitindo kadhaa wameanzisha kampuni zao kama alivyofanya Dada Jiang Peilin, ambaye anamiliki kampuni moja ya kuwahudumia wanamitindo.

Kuna kampuni kadhaa ambazo zimefanya maandalizi kwa mustakabali wa wanamintindo waliosaini mikataba nazo. Mfanyakazi wa kampuni moja Bi. Fan Xin alimwambia mwandishi wa habari kuwa, mbali na kuwapatia wanamitindo nafasi za kushiriki kwenye maonesho ya nguo na kushiriki kwenye mashindano ya wanamitindo, kampuni hiyo pia inawaandalia nafasi za ajira zikiwemo utangazaji kwenye vyombo vya habari na uigizaji wa filamu au vipindi vya televisheni. Zaidi ya hayo, inawasaidia wanamitindo kuendelea na masomo, kama vile kuinua kiwango cha lugha ya Kiingereza.

Bi. Fan Xin alisema "Tunawaandalia wanamitindo waliosaini mikataba na kampuni yetu njia mbalimbali za kujiendeleza. Si lazima wawe wanamitindo, bali tunawaandalia mipango inayolingana na hali halisi ya kila mwanamitindo, ambapo baadhi yao wataweza kuendelea na masomo, na wengine wataweza kujiunga na sekta ya filamu."

Idhaa ya kiswahili 2006-07-13