Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-13 15:44:22    
Jinsi Israel inavyokabiliana na migogoro miwili ya utekaji nyara

cri

Wanamgambo wa kundi la Hezbollah la Lebanon tarehe 12 waliwateka nyara askari wawili wa Israel kwenye mashambulizi waliyofanya kwenye eneo la mpaka wa kaskazini wa Israel. Israel ambayo imejitumbukiza kwenye msukosuko wa askari wake kutekwa nyara na wanamgambo wa Palestina, sasa inaibidi ikabiliane na migogoro katika pande mbili za kusini na kaskazini za nchi hiyo. Na serikali ya Ehud Olmert inakabiliwa na mtihani mgumu wa kisiasa na kijeshi ambao haujawahi kutokea kabla.

Wachambuzi wanasema waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert na serikali yake inakabiliwa na shinikizo mbalimbali kama zifuatazo:

Kwanza Israel inapaswa kupambana na kundi la Hezbollah ambalo lina nguvu kubwa za kijeshi zaidi kuliko kundi la Hamas. Hata hivyo Israel ilishindwa kupata ushindi katika siku zaidi ya 10 zilizopita kwenye operesheni ya kijeshi iliyoifanya dhidi ya Hamas. Kwa hiyo ni vigumu sana kwa Israel ikitumia nguvu ya kijeshi kulilazimisha kundi la Hezbollah liwaachie huru mateka wa Israel. Mbali na hayo eneo la kusini mwa Lebanon linajulikana kwa hali ya utata ya kijiografia na kiutamaduni. Kama Israel itapeleka jeshi la ardhi kwenye eneo hilo, itakabiliwa na hatari kubwa sana. Siku hiyo hiyo ya tarehe 12, askari wanne wa Israel waliuawa na mabomu yaliyotegwa ardhini na kundi la Hezbollah wakati walipovuka mpaka kati ya Israel na Lebanon, wakiwatafuta askari wenzao waliotekwa nyara.

Aidha, Lebanon ni nchi huru yenye mamlaka. Israel ikiivamia Lebanon, itabeba shinikizo la kimataifa na lawama za kisiasa kubwa zaidi kuliko jeshi lake kuingia kwenye sehemu ya Gaza. Tena, kundi la Hezbollah ni upande pekee unaohusiana na tukio hilo la kuvuka mpaka na kuwateka nyara askari wa Israel. Waziri mkuu wa Lebanon Bw. Fuad Siniora amesema serikali yake haikupata habari kuhusu kitendo hicho cha Hezbollah hapo kabla. Kutokana na hali hii, Israel kuishutumu serikali ya Lebanon na kupeleka ndege zake kupigia mabomu zana za kiraia nchini Lebanon, hiyo haitasaidia kutatua mgogoro.

Hivi sasa kuna mwelekeo dhahiri wa makundi ya Hezbollah na Hamas yaliyopo katika pande za kaskazini na kusini za Israel kushirikiana. Kiongozi wa Hamas amesifu kitendo hicho cha Hezbollah kuwa ni cha "ushujaa", ambacho kitasadia kuishinikiza Israel iwaachie huru Wapalestina inaowashikilia. Huku kiongozi wa Hezbollah pia ameeleza nia ya kuingilia kati mgogoro wa mateka kati ya Israel na Palestina. Hayo yanaonesha kuwa, migogoro hiyo miwili imeunganishwa, hivyo kuongeza ugumu wa kuitatua, na kuliwekea changamoto jeshi la Israel ambalo linapaswa kufanya mapambano katika sehemu mbili.

Mfuatano wa matukio ya wanajeshi wa Israel kutekwa nyara umetoa pigo kuwa imani ya jamii ya Israel na hisia za kutoiamini serikali na jeshi zimeongezeka miongoni mwa watu wa Israel. Kwa upande wa kundi la Hezbollah, kwa vile lilipanga kwa makini tukio hilo la kuwateka nyara wanajeshi wa Israel, pia limekuwa tayari kukabiliana na mashambulizi ya kijeshi ya Israel. Hezbollah imeeleza bayana kuwa, kama Israel inataka kuwaokoa wanajeshi wake, haina njia nyingine ila tu kufanya mazungumzo kwa kupitia upande wa tatu na kubadilisha mateka wa pande mbili. Kwa hiyo kukubali kubadilisha mateka au la ni suala gumu linaloikabili serikali ya Israel.

Sasa Israel itafanya nini? Wachambuzi kadhaa wanasema serikali ya Israel haina karata nyingi za kucheza. Kitendo cha kijeshi cha kulipiza kisasi kinafanya kazi za kuadhibu na kutoa onyo tu, lakini sio ufumbuzi wa kimsingi wa matatizo yaliyopo. Njia halisi inayoweza kuchukua ni kufanya kitendo cha kijeshi hadharani na juhudi za kidiplomasia faraghani kwa wakati mmoja, ambapo lengo la kitendo cha kijeshi ni kuhimiza mazungumzo, na hatimaye migogoro hiyo ingetatuliwa kwenye meza ya mazungumzo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-07-13