Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-14 15:38:31    
Ziara ya Wen Jiabao barani Afrika kuhimiza uwekezaji wa kiraia kati ya China na nchi za Afrika

cri
Mwezi Juni mwaka huu, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alifanya ziara katika nchi saba za Afrika ambazo ni pamoja na Misri, Afrika ya kusini, Tanzania na Uganda, ziara yake imefuatiliwa sana na jumuiya za kiuchumi za kiraia na wanakampuni wa China na nchi za Afrika. Mkuu wa idara ya mawasiliano na nje ya shirikisho la kiraia la biashara kati ya China na Afrika Bwana Chu Shuntang alisema, katika ziara hiyo ya waziri mkuu Bw. Wen Jiabao barani Afrika alifuatana na wajumbe wa wanakampuni binafsi wa China, na katika kila nchi aliyotembelea Bw. Wen Jiabao kuna makampuni mengi yaliyowekezwa na watu binafsi wa China, hivyo ziara hiyo ya Bw. Wen Jiabao barani Afrika bila shaka itahimiza maingiliano ya uchumi ya kiraia kati ya China na nchi za Afrika, na kuwahimiza wanakampuni binafsi wengi zaidi wa China wawekeze barani Afrika.

Wataalamu wamechambua kuwa, mawasiliano ya mara kwa mara ya kisiasa kati ya China na nchi za Afrika yataweka mazingira mazuri katika kuongeza uwekezaji wa pande mbili mbili. Hivi sasa uwekezaji wa moja kwa moja wa China kwenye nchi za Afrika umefikia dola za kimarekani bilioni 1.18, na makampuni yaliyowekezwa na wachina barani Afrika yamefikia 700 hivi.

Uwekezaji wa kiraia unaongezeka siku hadi siku katika mawasiliano ya kiuchumi kati ya China na Afrika. Mfanyabiashara wa Cameroon aliyeishi mjini Beijing kwa miaka zaidi ya 7 Bw. Adem ametoa mchango mkubwa katika kuhimiza uwekezaji wa kiraia kati ya China na Afrika. Kampuni yake ya Afeikese ya Beijing inashughulikia hasa kuyasaidia makampuni ya China kuwekeza na kuendeleza soko la Afrika.

Bw. Adem alisema nchi za Afrika zinayakaribisha sana makampuni ya China hasa makampuni binafsi kuanzisha viwanda huko, na zimetunga sera zinazotoa kipaumbele kwa wawekezaji kuhusu ushuru na forodha ili kuvutia uwekezaji. Hivi sasa anashirikiana na kampuni ya ujenzi wa nyumba ya Cameroon kuyaalika makampuni ya China kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa nyumba nchini humo.

Balozi wa Kongo Brazaville nchini China Bwana Pierre Basi alisema, serikali ya China inatakiwa kuyahimiza makampuni yenye uwezo kuwekeza barani Afrika ili kupunguza tofauti za kibiashara kati ya China na nchi nyingi za Afrika.

Wizara ya biashara ya China imeeleza kuwa, uwekezaji wa makampuni ya China umepanuka kuelekea barani Afrika kutoka nchi jirani za Asia. Waraka wa sera za China kwa Afrika umedhihirisha kuwa, serikali ya China itayaunga mkono makampuni yake kuwekeza barani Afrika kwa kutoa mikopo nafuu, pia inayakaribisha makampuni ya Afrika kuwekeza nchini China.

Shirikisho la biashara kati ya China na Afrika linalolenga kuyaelekeza makampuni binafsi ya China kuwekeza barani Afrika limeanzisha ofisi zake nchini Nigeria, Ghana, Tanzania, Msumbiji, Cameroon na Kenya, ambazo zimetoa misaada ya aina mbalimbali kwa makampuni ya China kuwekeza katika nchi hizo. Shirikisho hilo pia limeunda ujumbe wa wanakampuni binafsi wa China kufanya ukaguzi kwenye soko la Afrika.

Afrika ya kusini ni mshirika mkubwa kabisa wa kibiashara wa China barani Afrika. Naibu waziri wa mambo ya nje wa Afrika ya kusini Bwana Aziz Pahad alisema, ziara ya waziri mkuu Bw. Wen Jiabao nchini Afrika ya kusini itahimiza uwekezaji wa makampuni ya China nchini humo, alisema licha ya sekta ya uchimbaji madini na utengenezaji wa bidhaa, nchi hizo mbili pia zina uwezo mkubwa wa kushirikiana katika nishati, mitambo, mambo ya fedha, teknolojia ya viumbe, ujenzi wa miundo mbinu, utengenezaji wa mazao ya kilimo na utalii.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kuwa, katika miezi minne ya kwanza ya mwaka huu, thamani ya biashara kati ya China na Afrika ya kusini iliongezeka kwa asilimia 22.7 kuliko mwaka jana wakati kama huu. Na ifikapo mwishoni mwa mwaka 2005, kulikuwa na makampuni zaidi ya 100 yaliyowekezwa na wachina nchini humo, ambayo thamani ya jumla ya uwekezaji imefikia dola za kimarekani milioni 250, makampuni hayo yanashughulikia sekta mbalimbali za biashara, kilimo, nguo, vifaa vya elektroniki vya nyumbani, mitambo, chakula, vifaa vya ujenzi, uchimbaji wa madini, uchukuzi na mawasiliano ya simu.

Waziri mkuu Bwana Wen Jiabao tarehe 18 Juni alipofanya ziara nchini Misri alisisitiza kuwa, China inatilia maanani kukuza uhusiano wa uchumi kati yake na nchi za Afrika, China na nchi za Afrika zina uwezo mkubwa wa kushirikiana kiuchumi. Serikali ya China inayahimiza makampuni yake kufanya ushirikiano na nchi za Afrika ili kuinua uwezo wa nchi za Afrika wa kujiendeleza.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-14