Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-17 15:22:31    
Hekalu la Jidu

cri

Hekalu la Jidu lililoko katika mji wa Jiyuan mkoani Henan ni hekalu kubwa kabisa kati ya mahekalu ya kuabudu mungu wa mito nchini China. Hekalu hilo limekuwepo kwa miaka 1400, na limeorodheshwa katika urithi wa kitaifa wa utamaduni. Wataalamu wanalisifu hekalu hilo kuwa ni makumbusho ya majengo ya kale ya China.

Safari ya kufika kwenye Hekalu la Jidu kwa basi kutoka mji wa Zhengzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Henan, inachukua muda wa saa moja na nusu hivi. Eneo la hekalu hilo ni mita za mraba elfu 80, na mpangilio wa majengo ukiangaliwa kutoka juu unaonekana kuwa ni umbo la mraba kwa sehemu yake ya mbeleya mbele na umbo la duara kwa sehemu ya nyuma, mpangilio huo wa ujenzi unatokana na dhana za wahenga wa China kwamba umbo la mbingu ni duara na umbo la dunia ni la mraba. Mwongozaji wa watalii Bw. Duan Po alieleza,

"Neno 'du' la Kichina maana yake ni mito inayoingia baharini, kwani wahenga wa China waliona kuwa mito iliyostahili kuitwa 'du' nchini China ni mito ya Changjiang, Huanghe, Huaihe na Mto Ji, kwa hiyo hekalu la kumfanyia tambiko mungu wa Mto Ji linaitwa Hekalu la Jidu. Mahekalu ya mungu wa mito iliyoingia baharini ni mahekalu ya ngazi ya juu kabisa kati ya mahekalu yote ya mungu wa mito, lakini lililobaki sasa ni hekalu hilo tu."

Baada ya kuingia mlangoni na kupita kwenye milango mingine kadhaa ya mbao nene na njia yenye urefu wa mita zaidi ya mia mbili iliyotandazwa kwa mabamba ya mawe unafika kwenye ukumbi wa mungu wa Mto Ji, ukumbi huo ni jengo kuu katika kundi la majengo ya hekalu hilo. Ukumbi huo una eneo la mita za mraba zaidi ya mia moja, jengo hilo lilijengwa kwa mbao, ukumbi unahimiliwa kwa nguzo kadhaa kubwa. Mungu wa Mto Ji mwenye sura ya rehema akilala juu ya kitanda kilichochogwa kwa maua, ndevu zake nyeusi na ndefu ikitawanyika hadi nje ya mto wa kulalia, na malaika watatu wakisimama karibu yake wakionekana kama wanazuia watu wasikatishe usingizi mzuri wa mungu huyo.

Mwongozaji wa watalii Bw. Duan alieleza,

"Nchini China kuna dini za kibuddha, kikristo, kiislamu na nyingine lakini katika dini hizo hakuna sanamu ya mungu aliyelala, ila dini ya Dao ambayo iko nchini China peke yake. 'Mungu' wa Mto Ji amelala huko kwa starehe bila kuwa na wasiwasi wowote, anaudhibiti Mto Ji na kuhakikisha watu wanaishi salama."

Nyuma ya ukumbi huo ni chanzo ya Mto Ji. Mandhari ya ajabu ni kwamba, huko kuna chemchemi kadhaa inayobubujika miaka yote bila kukauka, mtiririko wa chemchemi hiyo unakwenda mashariki na kuingia baharini baada ya kupita mikoa ya Henan na Shandong, safari yake ni kilomita zaidi ya elfu moja kwa ujumla. Wataalamu wanasema, chemchemi hiyo ya ajabu inawafanya watu waiabudu sana katika miaka yote toka zamani hadi leo.

Baada ya kueleza chanzo cha Mo Ji, sasa tunawaeleza majengo ya hekalu hilo. Majengo ya hekalu la Jidu yana mitindo yote ya enzi za Song, Yuan, Ming na Qing. Katika kundi la majengo ya hekalu hilo jengo lililojengwa zamani sana limekuwa na miaka zaidi ya elfu moja, hilo ni jengo la ukumbi wenye kulala kwa mungu wa Mto Ji. Majengo ya hekalu la Jidu ni maarufu kwa muundo wake wa mbao zinazoumana, na mitindo tofauti ya enzi mbalimbali inaonekana wazi.

Mtalii aliyetoka Beijing Bw. Guo Xiaoke alisema,

"Kundi la majengo ya Hekalu la Jidu ni makumbusho makubwa ya majengo ya zamani nchini China. Sanaa za ujenzi wa China ya kale zinawastaajabisha sana watu wa leo, watu licha ya kushangaa ufundi mkubwa wa majengo hayo, pia wanastaajabu utamaduni mkubwa ulivyokuwa."

Jengo la mlango wa mbele wa hekalu hilo ni la ajabu. Paa kubwa la mlango huo lililohimiliwa kwa nguzo kubwa nne ni madhubuti ingawa limekuwa na miaka 500. Kwenye chanzo cha Mto Ji kuna mlango mmoja kwenye njia ya kufika kwenye chemchemi, mlango huo ulijengwa katika Enzi ya Yuan, hadi leo umekuwa na miaka 700. Kibanda kilichoko karibu na chemchemi ni johari ya taifa kwa thamani yake ya kisanaa, kibanda hicho kilijengwa kwa mitindo ya enzi kadhaa za kale za China, msingi wake wa mawe ulijengwa katika Enzi ya Song ambao hadi leo umekuwa na miaka zaidi ya elfu moja; nguzo za kibanda hicho zilijengwa katika Enzi ya Yuan ambayo imekuwa na miaka 700 hadi leo, na paa la kibanda hicho lilijengwa upya katika Enzi ya Ming, ambalo pia limekuwa na miaka 500.

Uzio wa mawe unaozunguka sehemu ya chemchemi ni uzio pekee uliokamilika hadi leo, uzio huo ulijengwa katika Enzi ya Song, hadi leo umekuwa na miaka zaidi ya elfu moja. Kwenye uzio yamechongwa mapambo ya dini ya kibuddha yakiashiria "baraka". Mapambo hayo yaliyotokea kwenye mahali hapo pa dini ya Dao yanaashiria kwamba, dini za kibuddha na kidao ziliwahi kuwa na uhusiano katika historia ya China.

Hivi sasa katika hekalu hilo la Jidu kuna masufii kadhaa wanaoshughulikia mambo ya ibada, mmoja kati yao alisema,

"Watu wanaokuja hapa huwasha udi na kufanya ibada wakiomba amani, katika hekalu hili kuna shughuli kubwa za ibada kila mwaka."

Tarehe sita mwezi Februari kwa kalenda ya Kichina ni siku ya kuzaliwa kwa mungu wa Mto Ji, katika siku hiyo watu hufanya shughuli kubwa za ibada katika hekalu hilo. Inafahamika kwamba hapo zamani katika siku hiyo ibada hiyo ilikuwa inafanywa kwa kuchinja ng'ombe na mbuzi hata kiasi cha elfu kumi. Hivi sasa ingawa ibada sio kubwa hivyo lakini watalii wanaweza kushughudia jinsi wahenga wa China walivyofanya ibada hiyo kwa heshima kubwa katika zama za kale.

Hivi sasa ukitembelea huko unaweza kuangalia vya kutosha jinsi mungu wa Mto Ji alivyolala ukiwa katika mazingira ya utulivu, na utaona hazina adimu za taifa la China, kwa sababu katika miaka kadhaa iliyopita majengo yote ya hekalu hilo yalikarabatiwa na kufunguliwa tena kwa watalii, unaposikiliza waongozaji wa watalii wanavyokusimulia hadithi za ajabu zilizotokea katika miaka mingi iliyopita, utajikuta kama umekuwa katika mazingira ya siku za kale.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-17