Alasiri ya Tarehe 16 Julai, Rais Hu Jintao wa China aliyehudhuria mkutano wa mazungumzo kati ya viongozi wa kundi la nchi 8 na nchi zinazoendelea alikutana na rais Bush wa Marekani huko Saint Petersburg, Russia, ambapo walibadilishana maoni kuhusu uhusiano kati ya China na Marekani na masuala ya kimataifa na kikanda yanayofuatiliwa na pande mbili.
Baada ya mkutano huo, rais Hu Jintao na rais Bush walikutana pamoja na waandishi wa habari, ambapo rais Hu kwanza alitathimini hali ilivyo ya sasa ya maendeleo ya uhusiano kati ya China na Marekani, halafu alijulisha maoni ya pamoja yaliyofikiwa kati ya pande mbili kuhusu kuendeleza zaidi uhusiano kati ya China na Marekani. Rais Hu alisema:
Tumekubaliana kuwa ni lazima kutendea na kushughulikia uhusiano kati ya China na Marekani kwenye kiwango cha juu cha kimkakati na kutupia macho siku za mbele, ili kujitahidi kupanua maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili, kuimarisha ushirikiano halisi katika sekta mbalimbali. Wakati huo huo tunapaswa kuheshimu na kuzingatia ufuatiliaji wa kila upande, kutatua ipasavyo masuala nyeti yaliyoko katika uhusiano kati ya China na Marekani ili kuhimiza uhusiano kati ya nchi hizo mbili uendelee kukuzwa.
Rais Bush alisema ziara aliyofanya rais Hu Jintao Mwezi Aprili mwaka huu nchini Marekani ilipata mafanikio makubwa. Marekani inatilia maanani uhusiano kati ya Marekani na China, na inapenda kuimarisha siku hadi siku ushirikiano kati ya nchi hizo na kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema:
Kwangu mimi, mkutano huo ni mazungumzo yanayoendelea kati ya Marekani na China baada ya ziara ya rais Hu nchini Marekani mwezi Aprili.
Kwenye mkutano huo, walipozungumzia ushirikiano kati ya China na Marekani katika sekta za uchumi na biashara, rais Hu alisisitiza kuwa, pande mbili zinapaswa kushughulikia ipasavyo mikwaruzano ya kibiashara kwa kufuata kanuni za kuwa na usawa na kunufaishana, ili kupata maendeleo ya pamoja. China itaendelea kuchukua hatua kupanua uagizaji bidhaa kutoka Marekani, kuimarisha uhifadhi wa hakimiliki ya ujuzi, na kujitahidi kuhimiza mageuzi ya utaratibu wa ubadilishaji wa fedha za Renminbi yafanywe kwa hatua madhubuti na mwafaka. Pia alisema China inaitaka Marekani itilie maanani zaidi kushughulikia ufuatiliaji wa China kuhusu mambo ya uchumi na biashara, kupunguza vizuizi vya kuiuzia China bidhaa zenye teknolojia za hali ya juu, na kuzipatia kampuni za China mazingira ya haki katika shughuli zao za biashara na uwekezaji nchini Marekani.
Rais George Bush alisema ongezeko la uchumi wa China linasaidia kupanua soko la mauzo ya bidhaa za Marekani, uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Marekani na China ni wa kunufaishana. Alisema Marekani inatilia maanani msimamo ulioelezwa na China, Marekani inapenda kupanua siku hadi siku uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Marekani na China.
Kuhusu Suala la Taiwan rais Hu alidhihirisha kuwa, China inasifu Marekani ambayo imeeleza kushikilia sera ya kuwepo kwa China moja, na kupinga kitendo chochote cha upande mmoja kinachoweza kusababisha kuifanya Taiwan ijitenge na taifa la China. Viongozi hao wawili pia walijadili hali ya peninsula ya Korea, suala la nyuklia la Iran na mchakato wa amani ya mashariki ya kati.
Rais Hu Jintao alisisitiza kuwa, njia ya kimsingi ya utatuzi wa suala la nyuklia la peninsula ya Korea ni kurudisha mapema iwezekanavyo mazungumzo ya pande 6, akisema:
Mimi na rais Bush tumeahidi kujitahidi kulinda amani na utulivu wa peninsula ya Korea na amani na utulivu wa Asia ya kaskazini mashariki, kuendelea kusukuma mbele mazungumzo ya pande 6 ili kutimiza lengo la kuifanya peninsula hiyo iwe sehemu isiyo na nyuklia.
Rais Hu Jintao alipozungumzia suala la nyuklia la Iran na hali ya mashariki ya kati alisema, China inapinga kueneza ilaha za nyuklia, na kupendekeza kutatua suala kwa njia ya kidiplomasia na mazungumzo; China inafuatilia hali wasiwasi ya mashariki ya kati na kuzitaka pande mbalimbali zijizuie na kutochukua vitendo vya kuifanya hali izidi kuwa mbaya.
|