Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-18 15:12:33    
Barua 0716

cri

Msikilizaji wetu Richard Wekesa Wekoyi wa sanduku la posta 1031-50200 Bungoma Kenya ametuandikia barua akianza kwa kutusalimu kutoka Bwake Salamu Club Bungoma Kenya. Anasema wanatutakia mwaka wenye furaha na mafanikio, na wanatushukuru sana kwa kuzinduliwa rasmi kwa Kituo cha FM huko Nairobi, wana furaha tele kutufahamisha kuwa matangazo ya Radio China kimataifa huko kwao wanayapata vizuri sana, hata kuliko ya vituo vingi vya matangazo vya huko mjini mwao. Pia wanaomba tuendelee kuwatumia jarida la daraja la urafiki na kadi za salamu ili uwanja wao wa salamu uzidi kupanuka.

Tunamshukuru Bwana Richard Wekoyi kwa barua yake, ni matumaini yetu kuwa yeye na wenzake wa klabu yao wataendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo yao, na sisi tutakapochapisha jarida la daraja la Urafiki hatutawasahau, kadi za salamu pia tutawatumia .

Msikilizaji wetu Susan Wanjala Rubia wa sanduku la posta 172, Bungoma Kenya ametuandikia barua naye akianza kwa salamu na akitueleza kuwa yeye ni mzima, na anatumai kuwa nasi ni wazima na tunaendelea kuchapa kazi kwa bidii mjini Beijing, China. Kwanza kabisa ana furaha kuu kwa Bwana Ayub Mutanda kupata nafasi ya pili katika mashindano ya chemsha bongo yaliyoandaliwa mwaka jana na Radio China kimataifa. Anasema hii imekuwa changamoto kwake, kwani hata kama yeye akishiriki katika mashindano hayo anatumaini kuwa miongoni mwa wale watakaonyakua nafasi tatu za kwanza.

Bwana Wanjala anasema anataka kushiriki katika shindano la chemsha bongo la mwaka huu, lakini tunaona kuwa amechelewa, kwani kuanzia tarehe 14 mwezi Mei tulitangaza makala 4 za chemsha bongo, na baadaye tulirudia matangazo yetu ya makala hizo 4. Shindano la chemsha bongo la mwaka huu litamalizika mapema kidogo. Ni matumaini yetu kuwa, yeye atashiriki kwenye mashindano mengine ya chemsha bongo yatakayoandaliwa na Radio China kimataifa mwaka kesho, na kila mwaka Radio China kimataifa inaandaa mashindano kama hayo.

Msikilizaji wetu Mogire Machuki wa sanduku la posta 646 kijiji cha Nyankware, Kisii, Kenya ametuletea barua naye akianza kwa salamu kwa wafanyakazi na watangazaji wa Radio China Kimataifa, Beijing China. Anasema ni matumaini yake kuwa sisi ni wazima wa afya, na tunaendelea kuchapa kazi ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu, anasema anafuraha kubwa kutuambia kuwa wanaendelea kuyafurahia matangazo na vipindi vya Radio China Kimataifa kila siku jioni.

Anatufahamisha kwamba vipindi vya Radio China Kimataifa vinaendelea kuvutia siku hadi siku. Kwa sasa hivi tatizo la usumbufu wa usikivu wa matangazo yetu halipo tena kwa wasikilizaji wa Kenya. Tatizo sasa ni ufupi wa vipindi, anapendekeza kurefushwa kwa baadhi ya vipindi kama vile sanduku la barua na kuboreshwa kwa kile kipindi cha burudani. Muziki unaochezwa hapa hautoshelezi, na ni ombi lake ni kuwa kipindi hiki kiwe na burudani ya jadi kutoka jamii mbalimbali kutoka barani Afrika na taifa la China. Kwa kipindi fulani muziki unaochezwa kwenye safu hii huwa ni marudio ya kipindi cha awali.

Kweli pendekezo lake hilo ni zuri, lakini hivi sasa bado tunakabiliwa na taabu mbalimbali, si rahisi kwetu kupata muziki mwingi kutoka kwa nchi mbalimbali za Afrika, tena siku hizi bado kuna taabu kutengeneza vipindi vingi vya burudani, lakini hata hivyo tutafanya juhudi kuboresha kipindi hiki, ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu.

Bwana Machuki anasema, anachukua fursa hii kutoa hongera zake za dhati kwa wahusika wa Radio China Kimataifa kwa kuuboresha ukurasa wa tovuti wa Radio China Kimataifa-idhaa ya Kiswahili kwa kuipa sura na umbo jipya. Anawaambia wasikilizaji wenzake kuwa ukurasa wa Radio China Kimataifa www.cri.cn ukichagua Kiswahili, unavutia sana na umejaa habari kemkem kuhusu taifa la China na uhusiano wake wa kibalozi na mataifa kadha kutoka kila pembe ya dunia. Ni bahari ya kujiongezea maarifa na daraja thabiti la kuelewa tamaduni na maisha ya watu wa China.

Anasema ni desturi yake kuwa mara moja kwa wiki lazima atenge dakika kadhaa za kumwezesha kuufungua ukurasa huu na kuutembelea ipasavyo. Anawaomba wasikilizaji wa CRI kama wana na uwezo wa kutembelea ukurasa huu wafanye hivyo, na ana hakika watavutiwa na taarifa ambazo zimechapishwa huko. Waswahili husema "mwonja asali haonji mara moja". Anasema tushirikiane ili tuiendeleze Radio China kimataifa.

Tunamshukuru sana Bwana Machuki kwa maoni yake juu ya tovuti yetu kwenye mtandao wa internet. Kweli siku hizi tumepunguza vipindi fulanifulani, ili tupate nafasi ya kuchapisha vizuri zaidi vipindi vinavyovutia zaidi. Tuna imani kuwa katika siku za usoni tovuti yetu itawafurahisha zaidi wasomaji wetu.

Bwana Machuki pia anasema, anaona furaha kuwa miongoni mwa wasikilizaji wachache watachaguliwa kupewa zawadi baada ya kukamilika rasmi shindano la chemsha bongo kuhusu Taiwan-kisiwa cha hazina cha China. Ni matumaini yake kuwa itafikia siku njema ambapo kisiwa cha Taiwan kitarudi chini ya mamlaka ya China.

Na mwisho anachukua fursa hii kumpongeza Rais wa China Bw. Hu Jintao na ujumbe wake kuitembelea Kenya. Ziara ya Rais Hu nchini Kenya ilifanyika wakati ambapo Kenya inakabiliwa na hali ngumu kiuchumi. Alipokutana na viongozi wa ngazi za juu wa Kenya, Rais Hu alizungumzia mambo kadha wa kadha hasa kwenye sekta ya uchumi ambayo kwa ushirikiano mzuri, nchi ya Kenya itapata faida nyingi. Anasema ana imani kuwa mikataba iliyosainiwa kati ya rais Hu Jintao na Rais wa Kenya Mwai Kibaki itachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza pato la Mkenya wa kawaida.

Anasema uhusiano kati ya Kenya na China kama vile Bw. Hu alivyoelezea ni wa jadi. Mwanamaji maarufu kutoka China Zheng He aliwahi kuongoza ujumbe wake hadi pwani ya Kenya yapata miaka 600 iliyopita. Aidha uhusiano huu unaendelea kuimarika siku hadi siku. Hii sasa Kenya inavitega uchumi vingi kutoka China. Anasema wao wakenya wanaendelea kufurahia uhusiano huu kwa vile sehemu kubwa ya bidhaa zinazotumika nchini Kenya zinatengenezwa China. Hivyo basi urafiki kati ya China na Kenya ni wa kipekee ili hofu iliyopo ni kuwa baadhi ya mataifa ya magharibi huenda yatapinga uhusiano huo.

Bwana Machuki anasema Rais Hu alipokuwa nchini Kenya, alipata fursa ya kukutana na wanafunzi wa Chuo cha Confucius cha kujifunza lugha ya kichina katika Chuo kikuu cha Nairobi, alipigwa butwaa na furaha pia kusikia kuwa Chuo cha Confucius kwenye chuo kikuu cha Nairobi ndicho cha kwanza kuanzishwa na serikali ya China barani Afrika. Pili, Radio China Kimataifa ilichagua Kenya kama eneo lake la kwanza la uzinduzi wa kituo cha kimataifa inayosikika kwenye wimbi la FM. Hizi ni baadhi ya faida ambazo Kenya imeridhika nazo kutoka kwa serikali ya watu wa China.

Bwana Machuki pia ansema wakenya wengi walivutiwa sana na ziara ya Bw. Hu nchini Kenya, na Redo China Kimataifa na vyombo vya habari vya Kenya vilitumia muda mwingi kuandika na kutangaza habari za ziara hiyo na uhusiano kati ya mataifa haya mawili.

Bwana Machuki anaeleza matumaini yake kuwa, daima wazidi kutuombea dua njema ili tuendelee kuwahudumia wasikilizaji. Radio China Kimataifa inachangia sana kujenga daraja la urafiki kati ya China na mataifa mengine duniani. Hivyo habari inazozitangaza wanaziamini kama chombo cha kimataifa ambacho kinafuatilia kanuni za kutangaza habari.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Bwana Mogire Machuki kwa barua zake zinazoeleza mambo mengi ya kututia moyo, kweli Bwana Machuki kila mara anatuandikia barua na kutoa maoni na mapendekezo mazuri kutusaidia kuboresha vipindi vyetu. Ni matumaini yetu kuwa tutadumisha urafiki na mawasiliano ya karibu.

Idhaa ya kiswahili 07-18