Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-18 18:27:41    
Nchi mbalimbali zaharakisha kuwaondoa raia wao wanaoishi nchini Lebanon

cri

Kutokana na kukabiliwa na hali ambayo mgogoro kati ya Israel na jeshi la Chama cha Hezbollah unapamba moto siku hadi siku, nchi mbalimbali zinaharakisha kazi ya kuwaondoa raia wao wanaoishi nchini Lebanon.

Mwandishi wetu wa habari mjini Cairo tarehe 17 usiku alifanya mahojiano kwa njia ya simu na ofisa wa ubalozi wa China nchini Lebanon Bwana Chi. Bwana Chi alisema baada ya kutokea kwa mgogoro kati ya Lebanon na Israel, ili kulinda usalama wa wachina, ubalozi wa China nchini Lebanon umekodi mabasi ya utalii kuwaondoa wafanyakazi wa makampuni ya China nchini Lebanon, wafanyakazi kadhaa wa ubalozi wa China nchini Lebanon na jamaa zao, wachina wanaoishi nchini humo na ndugu wa Hong Kong walioko nchini humo. Mpaka sasa wachina 105 wameondoka salama na kufika Syria, jirani ya Lebanon, ambapo wamepokewa na kupangiwa vizuri na ubalozi wa China nchini Syria, na wengi kati yao wako tayari kupanda ndege kurudi nyumbani China.

Bwana Chi amesema hivi sasa ubalozi wa China nchini Lebanon umeunda kikundi cha kukabiliana na hali ya dharura, ambacho kinashughulikia kuwaondoa wachina wanaoishi nchini Lebanon. Miongoni mwa wachina wanaoishi nchini Lebanon, watu wengi wameondoka salama isipokuwa wachache ambao hawataki kuondoka huko kwani wameoana na walebanon. Lakini Bwana Chi alisema, tarehe 17 wachina 20 wanaofanya utalii na biashara nchini Lebanon waliwasiliana na ubalozi wa China nchini Lebanon na kuomba msaada wa kuondoka Lebanon, ubalozi wa China ukawasaidia kuondoka haraka. Bwana Chi alisema, ubalozi wa China nchini Lebanon unafuatilia hali ya usalama ya huko, ili kukabiliana na matukio mbalimbali ya dharura, na kufanya juhudi zote kuwasaidia wachina walioko nchini Lebanon.

Mbali na China, nchi nyingine pia zimeanza kuwaondoa raia wao wanaoishi nchini Lebanon. Hivi sasa wafaransa wanaoishi nchini Lebanon wanafikia 17000, pamoja na wafaransa wengine zaidi ya 5000 wanaotalii nchini Ufaransa. Meli moja iliyotumwa na serikali ya Ufaransa tarehe 17 ilifika Beirut, mji mkuu wa Lebanon, meli hiyo imewachukua wafaransa zaidi ya 1000 pamoja na raia wa nchi nyingine za Ulaya na Marekani na kuwahamishia kwenye Bandari Larnaca nchini Cyprus iliyoko umbali wa kilomita 85 kutoka magharibi ya Beirut. Ubalozi wa Italia nchini Lebanon tarehe 17 ulidokeza kuwa, manowari moja ya Italia siku hiyo ilifunga safari kutoka Bandari ya Larnaca ya Cyprus na kuelekea Beirut, ili kuwaondoa raia wa Italia wapatao 200 na raia wa nchi nyingine wapatao 120 walioko nchini Lebanon. Balozi wa Uingereza nchini Lebanon siku hiyo pia alisema, Uingereza imewaondoa waingereza 40 kwa helikopta za kijeshi kutoka Beirut, na manowari kadhaa za kivita za jeshi la maji la kifalme la Uingereza hivi sasa zimefika kando la bahari ya Beirut, na kati ya siku moja na mbili zijazo, manowari hizo zitawasaidia watu wenye pasipoti za Uingereza walioko Lebanon waondoke huko.

Aidha hivi sasa Ujerumani imeondoa raia wake 200 kutoka Lebanon, na itaendelea kuwasaidia raia wake wengine 500 waondoke huko; Sweden imewaondoa raia wake 1300 na kuwahamishia nchi jirani Syria, wengine 300 walifika kwenye sehemu iliyopangwa na Syria tarehe 17. Zaidi ya hayo, raia wengi wa Fenland, Denmark, Nigeria, Ghana, Senegal, na Ethiopia pia wameondoka na kuelekea Syria. Hivi sasa Marekani imeondoa wafanyakazi wake 21 wa ubalozi wake nchini Lebanon. Marekani imefanya takwimu ikisema, hivi sasa wamarekani, au watu wenye pasipoti za Marekani, pamoja na wamarekani wengine ambao pia ni raia wa nchi nyingine wapatao 25000 wanaishi nchini Lebanon, hivyo mpango kabambe wa kuondoa wamarekani hao unapangwa haraka.

Wachambuzi wanaona kuwa, kutokana na Israel na chama cha Hezbollah zote hazitaweza kujali mwito wa jumuiya ya kimataifa wa kuzitaka zisimamishe vita, mgogoro wa kijeshi kati ya pande hizo mbili utapamba moto. Katika hali hiyo nchi mbalimbali zinazohusika zitaendelea kuharakisha kazi ya kuwaondoa raia wao wanaoishi nchini Lebanon.