Mazungumzo kati ya kundi la nchi 8 na nchi 6 zinazoendelea China, India, Brazil, Afrika ya Kusini, Mexico na Kongo Brazzaville yalifanyika tarehe 17 mwezi huu huko St. Petersburg, Russia. Mkutano huo hasa ulijadili mada 4 za usalama wa nishati, udhibiti wa ugonjwa wa kuambukiza na elimu duniani pamoja na maendeleo ya Afrika. Rais Hu Jintao wa China alishiriki na kutoa hotuba katika mkutano, na alitoa maelezo kuhusu usalama wa nishati duniani, tena alitoa pendekezo kuhusu mtazamo mpya wa usalama wa nishati, ushirikiano wa kunufaishana, maendeleo ya aina mbalimbali na kuanzisha dhamana kwa ushirikiano.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika mazingira yenye matatizo mengi ya kimataifa yakiwa pamoja na matukio mengi ya kikanda, ukosefu wa uwiano wa maendeleo ya uchumi, kupanuka kwa tofauti kati ya kusini na kaskazini ya dunia, ugaidi, uchafuzi kwa mazingira, maafa ya kimaumbile na magonjwa ya kuambukiza. Hivyo mazungumzo kati ya kundi la nchi 8 na nchi zinazoendelea yanafuatiliwa zaidi.
Mwenyeji wa mkutano huo rais Putin wa Russia alitoa pongezi na hotuba mara tu baada ya kufunguliwa kwa mkutano, hapo baadaye viongozi washiriki walibadilishana maoni kuhusu mada za mkutano. Rais Hu Jintao akitoa hotuba alisema, mazungumzo hayo yenye mada kuhusu usalama wa nishati, udhibiti wa ugonjwa wa kuambukiza na elimu duniani pamoja na maendeleo ya Afrika, yanaendana na wakati tena yanazingatia mustakabali wa siku za mbele. Kutatua vizuri masuala hayo au la, kunahusiana na maslahi ya nchi mbalimbali pamoja na watu wake, pamoja na mustakabali wa maendeleo ya binadamu.
Rais Hu Jintao alisema kila nchi ina haki ya kukuza maendeleo yake kwa kutumia rasilimali za nishati, karibu nchi zote hazitaweza kupata dhamana ya usalama wa nishati bila ushirikiano wa kimataifa. Hivyo jumuiya ya kimataifa inatakiwa kutekeleza mtazamo mpya wa usalama wa nishati kwa ushirikiano wa kunufaishana, kuendeleza nishati kwa njia mbalimbali na kuweka dhamana kwa ushirikiano, na kutaka jitihada za pande tatu zifanyike: kwanza, kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana katika uendelezaji na matumizi ya nishati. Pili, yatakiwa kuanzisha mfumo wa kimaendeleo wa utafiti wa teknolojia ya nishati pamoja na uendelezaji wa teknolojia mpya. Tatu, kuhifadhi mazingira mazuri ya kisiasa ya utulivu na usalama wa nishati.
Rais Hu Jintao pia alieleza mkakati wa nishati wa China, ambao ni kuweka mkazo katika udhibiti wa matumizi, kujitegemea kwa rasilimali za nchini China, kujiendeleza kwa njia mbalimbali, kuhifadhi mazingira, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa kunufaishana na kujenga mfumo imara wa nishati isiyotoa uchafuzi na ya bei rahisi.
Rais Hu Jintao alisisitiza kuwa China ni nchi inayotumia nishati kwa wingi, na pia ni nchi inayozalisha nishati kwa wingi. China itaimarisha ushirikiano na nchi zote zinazozalisha na kutumia nishati kwa msingi wa usawa na kunufaishana, na kuhifadhi kwa pamoja usalama wa nishati duniani.
Kwenye vitabu vya hotuba vilivyosambazwa mkutanoni, rais Hu Jintao pia alieleza maoni ya China kuhusu udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza, elimu na maendeleo ya Afrika. Rais Hu Jintao alisema, kuimarisha udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza ni kazi ya haraka ya jumuiya ya kimataifa kwa hivi sasa. Alitoa pendekezo la kufanikisha kazi hiyo kwa kupunguza bei za dawa au kuhamisha hataza za dawa ili kuongeza nguvu ya kupambana na Ukimwi.
Kuhusu suala la elimu rais Hu Jintao alisema, kwa nchi zinazoendelea kuharakisha maendeleo ya elimu kunaweza kuhimiza ongezeko la ajira na maendeleo ya uchumi, pamoja na kubadilisha hali ya udhaifu ya sekta mbalimbali. Baada ya mkutano huo kumalizika, rais Hu Jintao na washiriki wa mkutano walishiriki kwenye hafla ya mchana iliyoandaliwa na mwenyeji rais Putin, ambapo aliendelea kubadilishana maoni na baadhi ya viongozi kuhusu masuala ya kimataifa na kikanda yanayofuatiliwa na watu wengi.
|