Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-19 14:26:52    
Mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na Naibu mkuu wa Idara kuu ya Radio, Filamu na Televisheni ya China Bwana Tian Jin

cri

Naibu mkuu wa Idara kuu ya Radio, Filamu na Televisheni ya China Bwana Tian Jin amekwenda Nairobi Kenya kufanya ukaguzi na upimaji juu ya Kituo cha 91.9 FM Nairobi Kenya, kabla ya kuondoka Beijing, mwandishi wetu wa habari alifanya mahojiano na Bwana Tian Jin.

Mwandishi: Viongozi wa China na Kenya walipokutana walisifu sana kujengwa kwa Kituo cha 91.9 FM Nairobi Kenya, na wameagiza mara kwa mara matangazo ya kituo hicho yaendeshwe vizuri, wewe unaona ufuatiliaji wa viongozi hao umeonesha nini?

Bwana Tian: Mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, Rais Hu Jintao wa China alifanya ziara rasmi nchini Kenya, alipofika Nairobi alisikiliza matangazo ya China kwenye 91.9 FM Nairobi Kenya. Alipotembelea Chuo cha Confucius katika Chuo kikuu cha Nairobi Kenya aliwaambia walimu na wanafunzi wa chuo hicho kuwa, alisikiliza wimbo wa kichina kwenye 91.9FM Nairobi Kenya, na amejua wanafunzi hao wanajifunza kichina na utamaduni wa China. Rais Mwai Kibaki wa Kenya pia alisifu sana kituo hicho cha FM kilichoanzishwa na Radio China kimataifa huko Nairobi Kenya, aliona kuwa kuanzishwa kwa kituo hiki kumefungua ukurasa mpya wa maendeleo ya uhusiano kati ya China na Kenya. Ufuatiliaji wa viongozi wakuu wa China na Kenya juu ya mradi huo umetoa uungaji mkono mkubwa kwa kuzidisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye sekta za radio na televisheni, pia umeonesha matumaini ya wananchi wa China na Kenya ya kuongeza maelewano. Hii imewataka wafanyakazi wa Radio China kimataifa waandae vipindi vizuri zaidi siku zijazo ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wa Nairobi.

Mwandishi: Wewe una matarajio gani kuhusu matangazo ya 91.9 FM huko Nairobi Kenya?

Bwana Tian: Radio China kimataifa siku zote inashikilia kanuni ya kutangaza habari kwa kufuata hali halisi na kwa msimamo wa haki, CRI imepata uaminifu katika sekta ya matangazo duniani. Matangazo ya 91.9 FM Nairobi Kenya yanapaswa kufuata kanuni hizo, kutangaza habari kwa kufuata hali halisi na kwa msimamo wa haki, na lazima kuonesha wajibu wa radio kwa jamii, kuchangia kuhimiza utulivu wa jamii, masikilizano kati ya watu, kusukuma mbele maingiliano na maendeleo kati ya nchi zenye utamaduni tofauti, kuhifadhi aina nyingi za ustaarabu duniani. China ni nchi inayoendelea, imewahi kukumbwa na hali nyingi zinazofanana na zile zilizozikumba nchi nyingi za Afrika ikiwemo Kenya, China na nchi nyingi za Afrika zina matakwa mengi ya pamoja katika kusukuma mbele maendeleo na ujenzi wa taifa. Ndiyo maana matangazo yetu yanapaswa kuonesha vilivyo sauti na maslahi ya nchi nyingi zinazoendelea, kuimarisha urafiki na wananchi wa Kenya na wananchi wa nchi nyingine za Afrika, pamoja na wananchi wa nchi nyingi zinazoendelea.

Mwandishi: Mwezi Agosti mwaka 2005, viongozi wa China na Kenya walihudhuria sherehe ya kusainiwa kwa mradi wa ushirikiano kati ya serikali za China na Kenya pamoja na waraka wa ushirikiano kwenye sekta ya matangazo. Wewe ukiwa mmoja wa maofisa wanaohusiana na mradi huo wa ushirikiano, tafadhali tueleze zaidi ufuatiliaji wako wa siku zote juu ya maendeleo ya Kituo cha FM cha Radio China kimataifa.

Bwana Tian: Mwezi Novemba mwaka 2004, nilipotembelea Kenya nilifikia maoni ya pamoja na waziri wa habari na mawasiliano wa Kenya Bwana Tuju kuhusu mradi huo, baadaye pande mbili zilihimiza utekelezaji wa mradi huo. Mwezi Agosti mwaka 2005, Rais Mwai Kibaki wa Kenya alipofanya ziara nchini China, mimi na waziri Tuju tulitia saini kwenye nyaraka za serikali kuhusu mradi huo, ambapo rais Hu Jintao na rais Kibaki walihudhuria sherehe ya kusainiwa kwa waraka. Baada ya kufanya juhudi za pamoja za Radio China kimataifa, Shirika la utangazaji la Kenya KBC na idara nyingine, kituo hiki cha FM kilitangaza rasmi kuanzia tarehe 27 Februari mwaka huu, na siku hiyo mimi nilihudhuria sherehe iliyofanyika hapa Beijing.

Radio ni chombo muhimu cha mawasiliano ya habari cha umma. Kituo cha FM huko Nairobi Kenya hakika kitafanya kazi zenye juhudi katika kusukuma mbele maingiliano ya utamaduni kati ya China na Kenya na kuongeza maelewano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili. Kuna urafiki kati ya China na Kenya, tunataka kufanya vitendo halisi kuwasaidia marafiki zetu wakenya na kuleta manufaa halisi kwa wakenya; kwa kupitia matangazo yetu huko Nairobi Kenya, kuwawezesha wasikilizaji wetu wapate habari mbalimbali duniani kwa wakati, kuwaandalia vipindi vya burudani za muziki na utamaduni, ili waelewe zaidi utamaduni wa China na wa nchi mbalimbali duniani; na kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na wenzetu wa sekta za radio na televisheni. Nina imani kuwa, baada ya juhudi za pamoja za wasikilizaji wetu wa Kenya na watangazaji na watayarishaji wa kituo cha FM cha CRI, vipindi vya matangazo ya 91.9 FM ya Nairobi Kenya hakika vitaboreshwa siku hadi siku, na vitawavutia wasikilizaji wengi zaidi na kuwa daraja la urafiki kati ya China na Kenya na China na Afrika.

Mwandishi: Wewe uliwahi kusema kuanzishwa kwa Kituo cha FM cha CRI huko Nairobi Kenya ni chaguo la lazima la wananchi wa China na Kenya wenye maslahi ya pamoja katika zama tulizo nazo katika kuungana mkono, kushirikiana kwa kusonga mbele na kupata maendeleo ya pamoja. Tafadhali uwaeleze wasikilizaji wa Kenya maana kuhusu "chaguo la lazima".

Bwana Tian: Kwenye sherehe ya kuanzishwa rasmi kwa matangazo ya CRI 91.9 FM Nairobi Kenya iliyofanyika tarehe 27 Februari mwaka huu hapa Beijing, nilisema ingawa China na Kenya, China na nchi za Afrika ziko mbali, tena zina hali tofauti, lakini zote ni nchi zinazoendelea ambazo zina maslahi ya pamoja ya kimsingi. Kwani urafiki ulioanza tangu enzi na dahari ni msingi imara kwa China na nchi za Afrika kuendeleza urafiki wa jadi; kujenga dunia yenye ustawi, maendeleo, masikilizano na amani ni matumaini yetu ya pamoja, pia ni msingi wetu wa kutafuta maendeleo ya pamoja; kutoa sauti ya pamoja katika jukwaa la siasa ya kimataifa ni msingi wetu wa kisiasa wa kuongeza maelewano; kutafuta haki na halali, amani na maendeleo ni msingi wetu wa utamaduni wa kupatana na kuelewana; umaalum na nguvu bora za China na Kenya na China na Afrika ni msingi wetu wa kiuchumi kwa kusaidiana na kushirikiana ili kupata maendeleo ya pamoja.

Ni matumaini yangu kuwa, wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa wanaobeba jukumu la kihistoria watafanya juhudi kubwa za kuandaa vizuri vipindi vya matangazo ya CRI 91.9 FM Nairobi Kenya, na kuwa daraja la kusukuma mbele mawasiliano kati ya wananchi wa China na Kenya, na China na Afrika.

Na kwa kupitia matangazo ya CRI 91.9 FM Nairobi Kenya napenda kuwashukuru marafiki wote wa Kenya pamoja na balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli na wengine wote waliochangia kuanzishwa kwa kituo cha FM cha CRI huko Nairobi Kenya.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-18