Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-19 21:20:37    
Mwalimu wa rafiki mwema wa watoto wa China

cri

Je, mmewahi kuona watoto wenye udadisi mkubwa, ambao wanauliza maswali mengi mpaka unashindwa kuwajibu? Wazazi wa watoto wengi wa China mara kwa mara hukumbwa na 'tatizo hilo', hata hawajui namna kuwajibu maswali ya watoto wao. Lakini kitabu cha watoto kinachoitwa encyclopedia ya watoto wa China kinasaidia kutatua usumbufu huo. Kitabu hicho kinapendwa sana na watoto na kimekuwa mwalimu na rafiki mwema wa watoto wa China.

"Wang Yuhan: China ilichukua nafasi gani katika michezo ya Olimpiki ya Athens?

Yang Xiaoming: ya pili."

Wasikilizaji, mlikuwa mnasikiliza sauti ya mkutano mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi kwenye wilaya ya Chaoyang mjini Beijng ambao kauli mbiu ya mkutano huo ni 'mwewe mdogo aruke kwa nguvu ya kisayansi'. Mkutano huo ulikuwa na shughuli nyingi, zikiwemo mashindano ya ujuzi kuhusu michezo ya Olimpiki, michezo ya kuigiza, dansi na maonesho ya utamaduni wa chai wa China.

Mwanafunzi msichana Xu Tong aliyeshiriki kwenye michezo hiyo alisema, michezo hiyo yote ilitungwa nao wenyewe kutokana na ujuzi walioupata kwenye encyclopedia ya watoto wa China. Alisema:

"kabla ya kutunga michezo hiyo, tulitafuta taarifa nyingi husika kwenye encyclopedia. Kwa mfano, ngozi ya binadamu haiwezi kuboreshwa kwa kutumia Facial Mask mara moja tu. Ujuzi huo ndio tumeupata kwenye kitabu hicho."

Encyclopedia aliyoitaja Xu Tong ni encyclopedia ya watoto wa China inayoonesha umaalum wa utamaduni wa China kwa kutumia picha. Seti hiyo ya Vitabu ilichapishwa rasmi miaka mitano iliyopita. Xu Tong alisema, seti hiyo ya vitabu inanunuliwa sana na wanafunzi. Katika shule aliyosoma, kila darasa lina seti moja ya vitabu hivyo.

Seti hiyo ya Encyclopedia ina majuzuu matatu yaani mambo ya kimaumbile, sayansi na teknolojia na mambo ya kijamii, na inahusisha mambo mengi duniani yakiwemo elimu ya kosmografia na unajimu, dunia ya viumbe, miradi ya mawasiliano, elimu ya matibabu, utamaduni, michezo na historia. Lakini kinachowavutia watoto zaidi ni picha za kupendeza na maneno ya kuvutia kwenye vitabu hivyo. Kwa mfano, mwandishi anapofafanua maana ya "nguvu" kwa taaluma ya fizikia, anazihusisha na kuzilinganisha nguvu za aina mbalimbali na hali mbalimbali katika maisha yetu. Kwa hiyo watoto si kama tu wanaweza kuelewa haraka nadharia za sayansi, bali pia wataweza kujifunza kueleza hali nyingine mbalimbali katika maisha yao.

Bi. Zhao Xiuqing anayeshughulikia kazi ya uhariri wa vitabu hivyo alieleza, kwa kuwa watoto wanavutiwa zaidi na picha, hivyo walipoandika vitabu hivyo, walichagua picha nyingi za kupendeza, na kuunda mfumo wa ujuzi kwa kutumia picha hizo, maneno rahisi kwenye vitabu hivyo yanasaidia kuleta uelewa tu.

Bi. Zhao Xiuqing alisema, ili kujua wanavyopenda watoto, wahariri walichora picha zenye mitindo mbalimbali na kuzionesha kwa watoto wa shuleni na kuwaacha watoto wachague mtindo wanaoupenda. Alisema:

"picha wanazopenda ni kama hivyo, picha moja kubwa iwe katikati, kwani inaweza kuwavutia mara moja, halafu kuna picha kadhaa ndogo zinazozunguka picha hiyo, pia kuna picha kadhaa za michoro ya katuni. Kisha tumechukua maoni yao katika kazi yetu ya kutunga vitabu hivyo, na kuzitumia picha hizo za kupendeza kwenye vitabu hivyo."

Bi. Zhao Xiuqing alisema, kwa kuwa watoto hawawezi kuwa makini kwa muda mrefu, kwa hivyo vitabu hivyo vimegawanya mfumo wa ujuzi katika sehemu ndogondogo, na kila sehemu fupi inahusiana barabara na maisha ya watoto. Kwa mfano, wakati wa kueleza mfumo wa kupumua wa binadamu, ujuzi huo umegawanyika katika sehemu kadhaa, zikiwemo kupiga chafya, kupiga miayo na kukohoa. Hii inasaidia watoto waelewe mfumo nzima wa kupumua kwa kupitia sehemu hizo ndogondogo.

Aidha, vitabu hivyo pia vimetaja ujuzi na ustadi wa maisha na uwezo wa kujilinda, na vinasifiwa sana na wazazi wengi wa watoto.

Takwimu husika zimeonesha kuwa, tangu kuchapishwa kwa vitabu hivyo, seti milioni 3 zimenunuliwa. kinachofurahisha zaidi ni kwamba, watoto wengi wamenufaika kutokana na vitabu hivyo. Mwanafunzi wa shule moja ya msingi ya Beijing Liu Yichang alisema:

"vitabu hivyo vinanisaidia sana. Nilipotembelea jumba la makumbusho la China pamoja na marafiki za wazazi wangu, tuliona vitu vyingi vya kauri, walikuwa hawajui hivyo ni vitu gani, basi niliwaelezea mpaka wakashangaa sana."

Kwa kuwa vitabu hivyo vinapendwa sana na watoto, shule za sehemu mbalimbali nchini China zilifanya shughuli mbalimbali kuhusu vitabu hivyo, kwa mfano kusoma vitabu hivyo katika matangazo ya radio ya shuleni. Katika shule moja ya msingi katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur, wanafunzi walishiriki kwenye mashindano ya ujuzi na kuchagua "mwanafunzi hodari wa kusoma vitabu" kila mwezi.

Wazazi wa watoto wengi wanaona kuwa, ingawa hivi sasa kuna vitabu vingi vya watoto kwenye soko la vitabu nchini China, lakini ni vichache tu vinavyopendwa na wototo. encyclopedia ya watoto wa China imefanya jaribio mema katika kuelekeza hamu ya kujifunza ya watoto.