Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-20 15:48:42    
Uzinduzi wa reli ya Qinghia-Tibet waleta maisha mapya

cri

Reli ya Qinghai-Tibet ambayo ni ipo kwenye uwanda wa juu wenye mwinuko mkubwa kabisa duniani ilizinduliwa tarehe mosi Julai, ambapo Tibet ikamaliza historia ya kutounganishwa na reli. Kwa wakazi zaidi ya milioni 2 wa mkoa wa Tibet, licha ya kuwa reli hiyo itawarahisishia mawasiliano na kuwaletea bidhaa zenye bei nafuu, jambo muhimu zaidi ni kuwa, reli hiyo itabadilisha maisha na mitizamo ya wakazi wa mkoa huo.

Mzee Dorje Wangdark ni mfugaji mwenye umri wa miaka 70, anaishi huko Nagqu, kaskazini mwa Tibet. Familia ya mzee Dorje Wangdark ina watu 7 ambao wanajishughulisha na ufugaji. Hivi sasa familia hiyo ina nzao wa manyoya marefu zaidi ya 30 na mbuzi 100, mifugo hiyo ni mali ya familia na chanzo cha pesa. Mwaka 2002 wafanyakazi wengi walikwenda katika sehemu iliyo karibu na nyumba ya mzee Dorje Wangdark na kuanza kujenga reli, hali hii iliwavutia wafugaji wengi na mzee Dorje Wangdark mwenye busara alitumia fursa hii kuanzisha biashara.

Alikumbusha akisema "Wakati ujenzi wa reli unaendelea, nilijenga kibanda kando ya ofisi ya mradi wa ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet, nikawa nauza vinywaji, sigara na vyakula vidogovidogo. Mwaka jana nilikuwa na pato la Yuan elfu 3."

Licha ya hayo, watu wote wa familia hiyo walijiunga na kikundi kilichokuwa kinashiriki kwenye ulinzi wa reli hiyo kilichoanzishwa na serikali ya huko, na kupata mshahara. Mwaka jana, idadi ya mifugo ya mzee Dorje Wangdark haikuongezeka, lakini kutokana na ujenzi wa reli ya Qinghai-Tibet, pato la familia hiyo liliongezeka maradufu na kufikia Yuan elfu 10, sawa na dola za kimarekani elfu 1.25.

Wajenzi wa reli wanatembelea sehemu mbalimbali kutokana na kazi yao. Kutokana na kuzungumza nao, mzee Dorje Wangdark alipata habari nyingi kuhusu soko la mifugo la mkoa wa Qinghai, ambao uko jirani na Tibet. Akagundua kuwa bei ya mifugo mkoani Qinghai ni juu zaidi kuliko ile ya soko la kwao la Nagqu, wazo moja la kishujaa likamjia. Alisema "Nataka kufanya biashara ndogo kwa kutumia reli. Yaani napanda garimoshi kwenda Golmud kuuza bidhaa za kijiji chetu zikiwemo ngozi za nzao wa manyoya marefu, ngozi za mbuzi na manyoya ya mbuzi, halafu nikarudi na vitu vya mahitaji ya kila siku nikawauzia wanakijiji wenzangu."

Wakati mzee Dorje Wangdark anafanya maandalizi ya biashara yake ya kuvuka mpaka wa mikoa, kijana Loyul Sangshi anayesomea uandishi wa habari katika chuo kikuu cha Lhasa, naye pia ana mpango wake kufuatia kuzinduliwa kwa Reli ya Qinghai-Tibet. Kijana huyo anavutiwa na harakati mbalimbali za majadiliano ya kitaaluma na mawasiliano kati ya wanafunzi zinazoandaliwa mara kwa mara na vyuo vikuu mbalimbali katika sehemu nyingine za China. Awali kutokana na hali duni ya mawasiliano, ilikuwa ni nadra kwa chuo kikuu cha Lhasa kuandaa harakati za namna hiyo, jambo ambalo lilimsikitisha sana kijana Dorje Wangdark.

Kufuatia kuzinduliwa kwa Reli ya Qinghai-Tibet, Dorje Wangdark ambaye ni mjumbe wa kamati ya wanafunzi ya chuo kikuu cha Lhasa ameanza kuwasiliana na vyuo vikuu vya sehemu nyingine za China, kujadiliana maandalizi ya harakati za wanafunzi na semina ya kitaaluma. Alisema vyuo vikuu vingi vimevutiwa na pendekezo lake.  "Tumeridhika sana na tunafurahi sana. Kwa kupitia reli hiyo, ndugu zetu kutoka sehemu nyingine za China wataweza kuja mkoani Tibet, ambapo tutawasiliana mara kwa mara, pia tutaweza kuwaalika na kuandaa semina katika chuo kikuu chetu au kuwasiliana nasi uso kwa uso."

Yaliyotajwa hapo ni mifano miwili tu ya kuonesha jinsi reli ya Qinghai-Tibet inavyobadilisha maisha ya wakazi wa Tibet. Naibu mkuu wa Idara ya mambo ya kiuchumi ya Taasisi ya sayansi ya jamii ya Tibet Bw. Wang Daiyuan alieleza kuwa, kuzinduliwa kwa reli hiyo kutaeneza utamaduni wa jadi wa Kitibet. Alisema "Kuzinduliwa kwa reli hiyo kumeondoa hali ya utamaduni wa Kitibet kujitenga na sehemu nyingine na kuuletea uhai mpya. Tamaduni za makabila mbalimbali mkoani Tibet na nje zitawasiliana kwa haraka na kwa ufanisi, hali ambayo italeta maelewano ya kiutamaduni kati ya makabila tofauti."

Mtaalamu huyo pia alisisitiza kuwa, reli hiyo itailetea Tibet watalii wengi zaidi. Hivi sasa magarimoshi manne yanayobeba abiria elfu 4 hivi yanaingia mkoani Tibet kila siku. Ikiwa ni pamoja na abiria wanaopanda ndege, idadi ya watalii wanaotembelea Tibet itaongezeka kwa mara moja kwa siku. Kutokana na hali hii, hifadhi ya mabaki ya kale inafuatiliwa sana na watu.

Mwandishi wetu wa habari alipotembelea hekalu la Jokhang, ambalo ni hekalu lenye historia ndefu zaidi kuliko mengine mjini Lhasa, Lama Nyima Tsering wa hekalu hilo alimwambia kuwa, ana mpango wa kushirikiana na idara ya reli na kufanya matangazo kuhusu utamaduni wa Kitibet kwenye magarimoshi.

Alisema "Naona kutakuwa na matokeo mazuri kama tutaandaa matangazo kwenye magarimoshi, ili watalii wafahamu utamaduni wa Kitibet kabla ya kuwasili hapa. La sivyo, wakishafika itakuwa vigumu kwetu kuwafahamisha kwa undani utamaduni wa Kitibet mara moja, lakini wakikosa ujuzi husika wanaweza kuharibu mabaki ya kale bila kukusudia. Hali hiyo hiyo itawavunja moyo watu."

Kuzinduliwa kwa reli ya Qinghai-Tibet kumebeba matumaini na ndoto za watu wengi. Kama alivyosema Nyizla Budhaa kuwa,  "Reli ya Qinghai-Tibet ni reli ya baraka na reli ya uchumi. Kama tungeyachukua maji ya Mto Yarlu Tsang Po yawe wino na kufanya Mlima Himalayas kuwa kalamu, nisingeweza kuandika na kumaliza makala yangu kuhusu manufaa makubwa yanayoletwa na reli hiyo kwa Watibet wala furaha yao kubwa."

Idhaa ya kiswahili 2006-07-20