Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-20 15:51:57    
Watoto yatima 300 na mama yao

cri

Katika mji wa Fuyang, mkoani Anhui, katikati ya China, kuna kundi la watoto yatima ambao wazazi wao wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa ukimwi. Watoto hao walikuwa wanaishi katika mazingira magumu mpaka alipojitokeza mwanamke mmoja ambaye sasa watoto hao wanamwita mama.

 Msichana aliyeimba wimbo anaitwa Nan Nan, ana umri wa miaka 16. Miaka minne iliyopita, wazazi wake walifariki dunia kutokana na ugonjwa wa ukimwi, Nan Nan akawa yatima. Na kwa bahati mbaya sana, Nan Nan mwenyewe pia anaishi na virusi vya ukimwi ambavyo aliambukizwa na mama yake.

Wakati alipokuwa amekata tamaa, Nan Nan alikutana Bibi Zhang Ying mwenye umri wa miaka 37. Bi. Zhang Ying ni mfanyabiashara mwenye mfanikio.

Siku moja mwaka 2003, Bi. Zhang Ying alikutana na Nan Nan kwa mara ya kwanza, ambapo mtoto huyo alikuwa amechuchumaa na kuvumilia uchungu mkubwa ulioletwa na ukimwi. Picha hiyo iligusa sana hisia za Bi. Zhang Ying. Akikumbusha alisema "Wakati huo labda kwa sababu mimi mwenyewe milikuwa ni mama, nilimhurumia mtoto huyo, amepoteza wazazi, naye mwenyewe ameambukizwa virusi vya ukimwi, kutokana na ugonjwa hakuweza kuendelea na masomo. Niliona anahitaji misaada ya watu wengine."

Siku iliyofuata, Bi. Zhang Ying alimpelekea Nan Nan sweta, nguo nzito ya kukinga baridi, chakula, na kumpatia pesa kiasi cha Yuan 300. Lakini baada ya kurudi kwenye nyumba yake, Zhang Ying hakuweza kutulia, alimfuatilia sana Nan Nan mwenye mwili mwembamba na sura yake inayojaa uchungu. Kwa hiyo aliamua kumchukua mtoto huyo na kumleta Beijing, mji mkuu wa China ili apate matibabu.

Alisema"Wakati huo ilikuwa zimebakia siku 4 au 5 kabla ya mwaka mpya wa jadi wa China. Nilimchukua ili kumpeleka Beijing. Tulikuwa tumehangaika sana, kwa sababu ya kukaribia mwaka mpya. Tulishuka garimoshi, na kuelekea hospitali moja kwa moja. Tulipofika hospitali, ilinibidi nilipie ili aweze kupimwa mwili, na kumwandalia chakula."

Baada ya matibabu, hali ya Nan Nan ilianza kutulia na kuendelea kuwa nzuri, hali ambayo ilimtia moyo sana. Tabia yake ilianza kubadilika kutoka kujitenga na wengine mpaka kupenda kuwasiliana na wengine. Mabadiliko hayo yalimfurahisha Bi. Zhang Ying.

Katika mji wa Fuyang, mbali na Nan Nan bado kuna watoto yatima wengine waliofiwa na wazazi wao kutokana na ukimwi. Kwa sababu ya umaskini wakulima kadhaa wa huko iliwabidi wauze damu, na vituo vichache haramu vya kutoa damu vilitumia zana za kukusanya damu kwa marudio. Hali hiyo ikawafanya baadhi ya wakulima waambukizwe ukimwi. Ingawa serikali ilichukua hatua kali dhidi ya shughuli hizo haramu, na kuwapatia misaada watu walioambukizwa virusi vya ukimwi, lakini watoto yatima kama Nan Nan wamejitokeza.

Mwishoni mwa mwaka 2003, Bi. Zhang Ying aliacha biashara yake yenye thamani ya mamilioni ya Yuan, bila kujali upinzani wa jamaa na marafiki, akaanzisha shirika la kuwasaidia watoto yatima wa ukimwi, naye mwenyewe alijikita kwenye shughuli za shirika hilo.

Dada Huang Jinhong na ndugu yake Huang Jinlei ni watoto yatima waliopata misaada ya shirika hilo lilipoanzishwa, ambapo haikupita muda mrefu wazazi wao walipofariki dunia, watoto hao wawili walikuwa katika hali ya huzuni na upweke. Dada huyo alisema "Wakati huo baba na mama walikuwa wamefariki dunia, watoto wengine hawakucheza nasi, tulikuwa tunacheza sisi wenyewe na tulibaki na upweke mkubwa." Na ndugu yake mdogo Huang Jinlei aliongeza kwa kusema, "Majirani walifunga milango ya nyumba zao, na hawakuturuhusu kupita mbele ya nyumba zao. Hata hatukuthubutu kulia nyumbani kwetu, kwani hatukutaka kumletea huzuni babu yetu."

Baada ya kupata habari kuhusu watoto hao wawili, Bi. Zhang Ying aliwatembelea kwenye nyumbani kwao mara 5. Na kila safari alikwenda pamoja na vitu vingi vya mahitaji ya maisha.

Katika shughuli hizo za kuwasaidia watoto yatima, Bi. Zhang Ying alipata wazo moja kuwa, misaada ya mahitaji ya maisha haitoshi kwa watoto hao yatima. Aliona kuwa, watoto wengi yatima hawapendi kuzungumza na sio hodari katika masomo, wal ipozungumza na Bi. Zhang Ying walitokwa na machozi mara kwa mara. Zhang Ying aliona kuwa, watoto hao wanabeba mzigo mkubwa moyoni mwao.

Majira ya siku za joto mwaka 2004, Zhang Ying aliwaongoza watoto yatima zaidi ya 30 kufunga safari kwenda nje kutalii. Katika utalii huo, si kama tu watoto yatima walicheza kwa furaha kama watoto wengine wa rika yao walivyo, bali pia Bi. Zhang Ying alipata nafasi ya kuwasiliana nao kwa kina.

Mtoto Huang Jinlei akikumbusha alisema "Nilifurahia sana utalii huo, nilipata upendo wa mama Zhang Ying, na nikabadilika kuwa mtoto anayependa kuongea na kucheza na wengine kutoka mtoto asiyependa kuzungumza."

Mpaka hivi sasa watoto yatima zaidi ya 300 wamepata misaada kutoka kwa Bi. Zhang Ying. Na watoto hao wanampenda sana na kumwita mama. Wanachora picha au kutengeneza vitu vidogovidogo kama zawadi kwa mama huyo.

Zhang Ying ana mtoto mmoja mwenye umri wa miaka minne. Kwa kuwa anabanwa na shughuli mbalimbali na kukosa wakati wa kucheza na mwanaye, hata hivyo anaona angetoa upendo mwingi zaidi kwa watoto yatima. Alisema "Nikipata muda naweza kucheza na mtoto wangu, lakini watoto yatima ambao wamepoteza wazazi wananichukulia kama ni mama yao. Kwa hiyo wakipata shida ama wakiumwa, inanibidi niende kuwapa pole."

Katika miaka miwili iliyopita, Bi. Zhang Ying ametoa Yuan zaidi ya laki 3 katika shughuli za kuwasaidia watoto yatima. Alisema fedha hizo zinastahili kama watoto hao yatima wanapata furaha.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-20