Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-20 20:25:51    
Fundisho la kutokea tena tsunami nchini Indonesia

cri

Takwimu mpya zilizotolewa na serikali ya Indonesia tarehe 19, zinaonesha kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha tarehe 17 kutokana na tsunami iliyotokea kwenye bahari kusini mwa kisiwa cha Java imeongezeka hadi 550, na wengine 275 hawajulikani mahali walipo. Haya ni maafa ya pili ya tsunami kwa kufuatia maafa ya tsunami yaliyotolea mwishoni mwa mwaka 2004 nchini Indonesia. Wataalamu wanasema, vifo na majeruhi vingi vilivyosababishwa na tsunami kwa mara nyingine tena vinaonesha kuwa mfumo wa tahadhari kuhusu maafa ya tsunami unatakiwa kuboreshwa kwa haraka.

Wataalamu wamesema matetemeko ya ardhi na tsunami yaliyotokea mara kwa mara katika miaka ya karibuni nchini Indonesia na kusababisha vifo na majeruhi wengi, kwa upande mmoja ni kutokana na kuwa nchi hiyo iko kwenye kanda yenye matetemeko ya ardhi kwenye bahari ya Pasifiki, lakini kwa upande mwingine ni kutokana na kukosekana mfumo wa tahadhari wenye ufanisi kuhusu maafa ya kimaumbile.

Ofisa wa idara ya utafiti wa teknolojia ya wizara ya mambo ya nchi ya Indonesia, tarehe 18 mwezi huu alikiri kuwa kabla ya kutokea kwa tsunami, serikali ya Indonesia ilipata onyo kutoka kituo cha tahadhari ya tsunami cha Marekani kilichoko kwenye bahari ya Pasifiki na idara ya hali ya hewa ya Japan likisema, huenda tetemeko la ardhi la safari hiyo litasababisha tsunami, lakini serikali ya Indonesia haikuwafahamisha wananchi kuhusu onyo hilo. Shirika la habari la Associated press lilitoa habari zikisema, serikali ya Indonesia ilipata onyo kuhusu tsunami dakika 40 kabla ya nchi hiyo kushambuliwa na mkumbo wa kwanza wa tsunami, lakini makamu wa rais wa Indonesia Bw. Yusuf Kalla tarehe 18 usiku alisema, maafa ya tsunami ilitokea dakika 15 tu baada ya kutokea tetemeko la ardhi, kiasi ambacho walishindwa kutoa onyo. Lakini vyombo vya habari vya Indonesia vilisema, hata kama idara husika ya serikali iliweza kutoa onyo kwa wakati, lakini serikali katika ngazi za chini bado hazina uwezo wa kuwafahamisha na kuwaondoa wakazi wote wa huko.

Ofisa mmoja wa idara ya hali ya hewa ya Indonesia anayeshughulikia uanzishaji wa mfumo wa tahadhari ya tsunami, alisema, njia ya moja kwa moja ya kutoa onyo kwa wakazi ni kuweka ving'ora kwenye fukwe za bahari.

Hata hivyo vyombo vya habari vinasema, kwenye fukwe zilizokumbwa na tsunami hakuna zana za kutoa onyo, hivyo hata kama serikali katika ngazi za chini za huko zikipata habari kuhusu kutatokea kwa tsunami, lakini hazina uwezo wa kuwafahamisha wakazi na watalii walioko karibu na ufukwe wa huko. Habari zinasema, wakati huo kulikuwa na watu wengi kwenye fukwe, na hawakuwa na habari yoyote kuhusu tetemeko la ardhi lililotokea. Mbali na hayo, siku ile maji ya bahari yalikuwa machache, hivyo karibu watu wote hawakuona maji ya kurudi sehemu ya ndani ya bahari, dalili ambayo ni ishara ya kutokea kwa tsunami, kwa hiyo watu wengi walikumbwa na maafa.

Ikilinganishwa na Indonesia, nchi za Thailand na Malaysia, pia zilikumbwa na maafa ya tsunami iliyotokea kwenye bahari ya Hindi mwaka 2004, lakini zimepata maendeleo ya haraka katika ujenzi wa mfumo wa tahadhari ya tsunami. Hivi sasa, Thailand imejenga mnara wa kutoa onyo kwenye fukwe za pwani ya kusini mwa nchi hiyo, ambao unaweza kutoa sauti kubwa ya onyo baada ya kupata onyo kutoka idara husika za kikanda, na kutangaza kwa lugha za aina nyingi na kutaka watu waondoke mara moja. Malaysia nayo imejenga maboya mawili ya kuchunguza tsunami, ambayo yanaweza kutoa onyo kwa wakazi wa pwani saa 1 kabla ya kutokea kwa tsunami, ambapo ujumbe unapelekwa kwa watu wenye simu za mkononi, hali kadhalika vituo vya televisheni na radio pia vinatangaza habari na kutoa onyo kwa watu.

Kwa kuwa matetemeko ya ardhi yanatokea kwa mara elfu kadhaa kwa mwaka nchini Indonesia, na tsunami zinazosababishwa na matetemeko zinatishia usalama wa wakazi wa pwani, hivyo baadhi ya wataalamu wanasema, ni jambo la haraka na lazima kwa nchi hiyo kujenga mfumo kamili wa tahadhari ya maafa.