Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-21 16:21:02    
Hali nzuri na mbaya kwa uchumi wa nchi zilizo nyuma kabisa kiuchumi duniani

cri

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya biashara tarehe 20 huko Geneva uliotoa "Ripoti kuhusu uchumi wa nchi zilizo nyuma kabisa kiuchumi duniani mwaka 2006" ikieleza kuwa, hali ya uchumi wa nchi 50 zilizo nyuma kabisa kiuchumi duniani ni nzuri na mbaya, na kusema kwamba kitu muhimu kabisa kwa nchi hizo kuweza kuendeleza uchumi na kupunguza umaskini ni kuimarisha uwezo wa kuzalisha mali.

Ripoti inaeleza kuwa, kwa wastani nchi hizo zilipata ongezeko la uchumi kwa 5.9% mwaka 2004, hili ni ongezeko la kasi kabisa katika muda wa miaka 20 iliyopita, thamani yake ni dola za Kimarekani bilioni 10.7, hata hivyo thamani hiyo ni 1.6% tu ya mitaji yote kutoka nchi za nje, na 60% ya mitaji kutoka nchi za nje iliwekezwa kwenye nchi sita zinazozalisha mafuta. Tokea mwaka 1999 hadi 2004 misaada ya nchi za nje kwa nchi hizo iliongezeka mara mbili na mwaka 2004 misaada hiyo ilikuwa mikubwa hadi kufikia dola za Kimarekani bilioni 24.9. Lakini misaada hiyo ya kiserikali kutoka nchi za nje haikutolewa kwa uwiano kwa kila nchi, bali karibu nusu ya nchi hizo zilipokea misaada kidogo zaidi badala ya kuongezeka.

Ripoti pia inasema, mwaka 2004 nchi hizo zilikuwa na hali nzuri kabisa katika biashara na nchi za nje, na thamani ya biashara hiyo ilifikia dola za Kimarekani bilioni 57.8, hili ni ongezeko la 26% kuliko mwaka 2003, lakini hata hivyo, thamani hiyo ilikuwa ni 0.6% tu ya thamani yote ya biashara ya kimataifa duniani, na ongezeko hilo la biashara lilipatikana zaidi katika nchi nne zinazozalisha mafuta.

Kuhusu madeni, ripoti inaeleza kuwa tokea mwaka 1999 jumuyia ya kimataifa ilipiga hatua kubwa katika juhudi za kuondoa au kupunguza madeni kwa nchi hizo, hata hivyo madeni ya nchi hizo bado ni makubwa. Mwaka 2003 madeni ya nchi hizo yalifikia hadi dola za Kimarekani bilioni 158.9 ambayo ni makubwa kabisa katika historia, na ni ongezeko la dola za Kimarekani bilioni 20.8 kuliko mwaka 2001. Idadi ya watu wa nchi 50 maskini kabisa duniani inachukua 11.3% ya watu wote duniani, lakini thamani ya bidhaa zilizozalishwa nchini humo inachukua 0.6% ya thamani yote ya bidhaa zilizozalishwa duniani.

Katika miaka ya karibuni nchi nyingi kati ya nchi hizo zilipata maendeleo ya haraka kuliko miaka yote iliyopita, na bidhaa zilizouzwa katika nchi za nje ziliongezeka kwa kiasi kikubwa, lakini maendeleo hayo hayakuweza kusaidia kupunguza umaskini na kuongeza huduma za jamii kwa wananchi. Kwa upande mwingine, ripoti hiyo inasema, ongezeko hilo litakuwa vigumu kuendelea, kwani ongezeko hilo linategemea zaidi bei ya malighafi yakiwemo mafuta. Ili kugeuza hali hiyo ripoti imependekeza kuwa nchi hizo zitilie mkazo kwenye kuimarisha uwezo wa uzalishaji na kutokana na ongezeko la uwezo huo zipunguze umaskini.

Ripoti inasisitiza kwamba kwa kupitia juhudi za kuimarisha uwezo wa uzalishaji, nchi hizo zitaweza kuendeleza uchumi siku hadi siku kwa kutegemea maliasili za nchini humo na kupunguza hali ya tegemezi na kupata mitaji binafsi katika mchakato wa maendeleo ya uchumi. Na kwa kupitia uimarishaji wa uwezo wa uzalishaji nchi hizo zinaweza kuachana na hali ya kusafirisha malighafi tu na kuzipatia bidhaa zao uwezo wa ushindani katika soko la kimataifa. Zaidi ya hayo, ili kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa nchi hizo zinapaswa kuzalisha mali nyingi, na ili kuzalisha mali nyingi ni lazima nchi hizo ziimarishe uwezo wa uzalishaji.

Mwishoni ripoti hiyo inasema kutokana na hali ya kuwa nyuma kiteknolojia, uchache wa raslimali na kwenda polepole kwa mageuzi, nchi hizo zitakumbwa na matatizo mengi katika juhudi za kuimarisha uwezo wa uzalishaji, lakini kama matatizo yakiweza kutatuliwa na kutumia vya kutosha maliasili na uwezo wote wa uzalishaji, nchi hizo zitapata maendeleo makubwa ya uchumi na umaskini utapunguzwa kwa kiasi kikubwa, na serikali za nchi hizo zitawajibika kabisa katika juhudi hizo, na bila shaka mazingira ya amani ni ya lazima na uungaji mkono wa kimataifa. Maendeleo ya uchumi wa nchi hizo sio tu yatanufaisha nchi hizo tu bali pia yatainufaisha dunia nzima.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-21