Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-24 17:45:35    
Israel yakabiliwa na mashinikizo makubwa ya kijeshi na kisiasa

cri

Hadi kufikia tarehe 24 mwezi huu, mapigano kati ya Lebanon na Israel yameingia siku ya 13. Kampeni kubwa ya kijeshi bado haijapata ufanisi dhahiri, hivyo Israel inakabiliwa mashinikizo makubwa ya kijeshi na kisilaha kadiri siku zinavyokwenda.

Hivi karibuni, pamoja na hali ya uwanja wa vita kubadilika kuwa na matatizo mengi, tarajio jema la vyombo vya habari nchini Israel kuhusu kampeni ya kijeshi linapungua hatua kwa hatua. Tokea kulipuka kwa vita tarehe 12 mwezi huu, jeshi la Israel lilidondosha mabomu mengi dhidi ya uwanja wa ndege, barabara na madaraja nchini Lebanon pamoja na vituo, maghala ya silaha na risasi na makao makuu ya chama cha Hezbollah. Jeshi la Israel lilitangaza kuwa limeteketeza 40% hadi 50% ya nguvu za jeshi la chama cha Hezbollah siku chache zilizopita, lakini hadi hivi leo bado haijaonekana dalili ya kudhoofika kwa uwezo wa kushambulia wa chama cha Hezbollah, ambapo kila siku jeshi la chama hicho linarusha wastani wa makombora zaidi ya 100 dhidi ya sehemu ya kaskazini mwa Israel. Wachambuzi wa Israel wanasema, vituo vya uongozi na zana nyingi za kijeshi za chama cha Hezbollah zilijengwa chini ya ardhi, hivyo ikiwa jeshi la Israel halina habari sahihi kabisa ni vigumu sana kwake kupata ufanisi mzuri kwa kutumia ndege kudondosha mabomu, kwa hiyo ni hakika kuwa litapeleka askari wa ardhini kufanya mashambulizi.

 

Ukweli ni kwamba katika siku chache zilizopita kulikuwa na askari elfu kadhaa waliofanya mashambulizi madogo kwenye sehemu ya mpaka kati ya Lebanon na Israel. Lakini wachambuzi wanasema, jeshi la Israel litakabiliwa na hatari kubwa zaidi likitumia jeshi la ardhini. Chama cha Hezbollah kikiwa kama ni jeshi la wanamgambo (guerilla), kimekuwa na mazingira bora zaidi. Katika siku nyingi zilizopita jeshi la chama cha Hezbollah lilipigana na jeshi la Israel kwa kutumia mbinu ya kuchanganya askari wake na wakazi wa huko na kutumia milima mingi ya sehemu ya kusini mwa Lebanon, ingawa jeshi la Israel limezatitiwa kwa silaha bora, lakini halikupata mafanikio makubwa. Mkuu wa majeshi wa jeshi la Israel Bw. Dan Halutz tarehe 22 alikiri kuwa watatumia muda wa wiki kadhaa kabla ya kutimiza lengo lao la kijeshi, tena Israel haina uwezo wa kuzuia kabisa mashambulizi ya makombora ya chama cha Hezbollah ila tu kupunguza ukali wa silaha za chama cha Hezbollah kwa kusonga mbele kwa upande wa kaskazini, na kupeleka ndege nyingi kudondosha mabomu na kushambulia chama cha Hezbollah hadi litakapoona kuwa hakiwezi tena kufanya mashambulizi.

 

Licha ya kutatizwa na mambo ya kijeshi, Israel pia inakabiliwa shinikizo kubwa la duniani. Hadi hivi sasa walebanon zaidi ya 350 wamepoteza maisha katika mapigano kati ya Lebanon na Israel. Habari kuhusu Israel kudondosha mabomu dhidi ya miundo-mbinu ya Lebanon na wakimbizi wengi wa Palestina kukimbia makwao zinafahamika kote duniani, jambo ambalo jumuiya ya kimataifa inaona ni vigumu kuvumilia. Makala moja iliyochapishwa katika gazeti la "Haaretz" nchini Israel ilisema, tukio lolote linaloleta vifo na majeruhi mengi kwa raia wa litaweza kuwa kosa kubwa litakaloifanya Israel ishindwe kabisa. Mchambuzi mmoja alisema, pamoja na ziara inayofanywa waziri wa mambo ya nje wa Marekani bibi Condoleezza Rice tarehe 24, shughuli husika za usuluhishi zitakarakishwa, ambapo mchakato wa kumaliza harakati za kijeshi kwa Israel pia utaanza.

Aidha, kuhusu mapambano kati ya Lebanon na Israel, wazo la muda mrefu la Israel siyo kuteka tena sehemu ya kusini mwa Lebanon, bali ni kutumai kuwa serikali ya Lebanon inabeba jukumu la kulinda usalama wa sehemu ya mpakani kati ya nchi hizo mbili na kudhibiti ipasavyo sehemu hiyo. Endapo Israel itafanya mashambulizi kupita kiasi na kuathiri hadhi ya utawala ya serikali ya Lebanon, basi wazo la Israel la kutokomeza tishio la sehemu ya mpakani wa kaskazini mwa nchi yake kwa kupitia hatua za kisiasa na kidiplomasia litashindwa kutekelezwa.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Israel vimesema, hatimaye mgogoro huo kati ya Lebanon na Israel utatatuliwa kwa njia ya mazungumzo, na matokeo ya vitendo vya kijeshi yatahusika moja kwa moja matokeo ya mazungumzo ya kidiplomasia ya siku za baadaye, lengo halisi la Israel ni kukidhoofisha Chama cha Hezbollah, lakini haina mbinu nzuri ya kutimiza lengo hilo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-07-24