Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-25 15:07:47    
Barua 0723

cri
 Msikilizaji wetu Franz Manko Ngogo wa sanduku la posta 71 Tarime Mara Tanzania ametuletea barua pepe akisema, kwa heshima yake anapenda kutujulisha kuwa ametuma majibu yake ya chemsha bongo juu ya "Mimi na Radio China kimataifa", ingawa kwa kiasi fulani amechelewa kidogo kutokana na sababu za kifamilia ambazo hazikuweza kuzuilika, na tatizo la kitaifa la kukatika kwa umeme vile vile lilileta shida. Hata hivyo anashukuru mungu kwa kumwezesha kutujulisha alivyolipokea shindano hili na maoni yake.

Anasema kwa wao wasikilizaji kushiriki kwenye shindano hilo ni kitu muhimu zaidi maishani na wala siyo kushinda. Anatushukuru sana kwa zawadi yetu aliyopata baaada ya kuwa mshindi wa nafasi ya kwanza mwaka jana, zawadi pamoja na cheti vimemfikia salama, pia ile ya mwaka juzi iliyoshindwa kufikishwa na Bwana Wambwa, anasema hilo liko mikononi mwetu bila shaka tunajua jinsi tutakavyomfikishia.

Bwana Ngogo kwenye barua yake pia anatoa mwito kwa wana-Kemogemba wote, ili wamwunge mkono apate nguvu ya kusaidiana na Radio China kimataifa, kudumisha urafiki.

Tunamshukuru sana Bwana Ngogo kwa barua yake, tunapenda kumwambia kuwa asiwe na wasiwasi, na zawadi ya mwaka juzi imekuwa na tatizo kidogo kutokana na kusafirishwa njiani, hivyo tunataka kutafuta njia nyingine rahisi ya kumfikishia zawadi yake, ni matumaini yetu kuwa Bwana Ngogo ataendelea na juhudi bila kulegea, tuna imani kuwa urafiki kati yetu hakika utadumu daima.

Na Bwana Ngogo anaomba salamu zake za heri na baraka ziwafikie marafiki zake kama wafuatao: Mogire O Machuki, Kepher Gichana, Mbarouk Msabah, Jim Mwanyama, Onesmo Mponda, Ghulam H. Karim, Steven Magoye Kumalija, Emmanuel Kapella, Emmanuel Ngogo, Deborah Bhoke, Rehema Otaigo, Philip Mang'enyi, Mama Nyanswi Ngogo na watoto Esta, Elizah na Eduard wote wa Kemogemba.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff wa sanduku la posta 172, Bungoma Kenya ametuletea barua akisema kuwa, katika ulimwengu huu, yeye ana matarajio makubwa kwa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, ni kwa nini? Anasema hii idhaa ni bora na nzuri kwa uaminifu wake kwa wasikilizaji wa mataifa kadha wa kadha. Mfano, idhaa ya Kiswahili ya CRI inaendelea kuvuma kama upepo hapo kijiji cha Lwanda, tarafa ya Sang'alo, magharibi-Kanduyi, wilaya ya Bungoma magharibi mwa Kenya kutokana na kuwa na wasikilizaji wengi.

Anasema kwa niaba ya wasikilizaji wenzake anatoa pongezi kwa Radio China kimataifa kwa juhudi za kutangaza matokeo ya shindano la chemsha bongo la mwaka jana bila kucheleweshwa. Na kwa juhudi hizi wasikilizaji walioshinda kama vile Ras Franz Manko Ngogo wa Tarime Tanzania wamepata nafasi ya kwanza, pongezi tele. Bwana Ayub Mutanda Sariff na Mogire Machuki wa Kisii Kenya wamepata nafasi ya pili, bila kusahau wengine wote waliofuata, tafadhali twasema hongera, na wanashukuru idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa msaada wake, wasikilizaji wa klabu yao wataendelea na juhudi ili kutia fora .

Anasema kipindi cha sanduku la barua cha Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa ni kipindi ambacho kina sifa kubwa, kwani kinawapatia fursa wasikilizaji kutoa mapendekezo, maombi, pamoja na matakwa yao kama alivyosema Bwana David Ngoya ambaye ni mmoja kati ya walimu wakuu wa wilaya ya Bungoma Kenya, anasema Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa inasoma barua kutoka kwa wasikilizaji wake, hii inawafurahisha wasikilizaji.

Anasema, wanaomba kama kuna uwezekano kuongeza muda wa kipindi cha sanduku la barua katika siku mbili Jumamosi na jumapili ambapo wanafunzi na walimu pamoja na wafanyakazi wengine waweze kupata fursa ya kusikiliza kwa makini.

Pia anasema kutokana na malalamiko waliyokuwa nayo mwaka jana, Bwana Telly Wambwa alisema kwa kweli Radio China kimataifa ina wafanyakazi wachache na kazi alizoziona ni nyingi huenda hiyo inaweza kuwa moja ya sababu za kucheleweshwa kwa barua za wasikilizaji.

Tunashukuru Bwana Mutanda Ayub Shariff kwa barua yake pamoja na maoni hata malalamiko yake, tutachapa kazi zaidi ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu, kwani utiifu wao unatutia moyo, tuna imani kuwa siku hadi siku, chini ya juhudi za wasikilizaji wetu, kazi yetu itaboreshwa.

Msikilizaji wetu Xaxier Telly Wambwa wa sanduku la posta 2287 Bungoma Kenya ametuletea barua akianza kwa kutusalimu kutoka huko Bungoma Kenya, ni matumaini yake kuwa sisi sote tu wazima, na wao wanaendelea kutegea masikio matangazo ya Radio China kimataifa. Barua yake hiyo ina lengo la kutushukuru wafanyakazi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa jinsi tunavyoendelea kupanga na kuchapa kazi ya kuvutia, wasikilizaji wote wanafurahia.

Anasema hii inatokana na masimulizi ya Bwana Ayubu Mutanda aliyosikia tulipokuwa tunamhoji huko Nairobi wakati wa kuzinduliwa rasmi kwa matangazo ya CRI 91.9 FM Nairobi Kenya, wakati Mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gennian alifanya ziara huko. Bwana Ayub alifurahi sana alipokutana na dada Du Shunfang kwa mara ya pili na Bwana Alley kwa mara ya kwanza. Alipata fursa hii kutokana na kitabu cha Radio China kimataifa alichopewa kama zawadi aliporudi Kenya kutoka China baada ya kupata ushindi katika shindano la chemsha bongo la mwaka 2004.

Yeye alimweleza dada Du Shungfang kuhusu yeye alipotaka kujua alipo na hali yake. Kwa hiyo Bwana Telly Wambwa alishukuru sana Bwana Ayub alipowawakilisha wasikilizaji hao wa Bungoma Kenya akiwa karani, naye Wambwa akiwa mwenyekiti wa vilabu vyote vya idhaa ya Kiswahili ya CRI huko Bungoma Kenya, wataendelea kushirikiana naye na wenzao kwa pamoja bila matatizo.

Pia anawashukuru Bwana Alley na dada Du Shunfang kwa salamu zao walipomtuma Bwana Mutanda kumletea yeye na wasikilizaji wa Bungoma Kenya. Na mwisho anapenda kutueleza kuwa wanafurahia kipindi cha utamaduni cha kinachowaelezea michezo ya kuvutia, na anajaribu sana kufuatilia sanaa ya ngonjera ya kuchekesha.

Msikilizaji wetu Okongo Okeya wa sanduku la posta 381 Iganga Uganda ametuletea barua akisema, anachukua fursa hii kutoa pongezi zake nyingi na kutoa shukrani kwa watu wote ulimwenguni wanaofanya kazi kwa bidii zaidi na uvumbuzi zaidi katika karne hii ya 21. Na kuwashukuru watu wote wanaofanya kazi inayoleta manufaa kwa wanadamu na kuhifadhi mazingira ya viumbe. Anasema mazingira tunayoishi yanastahiki kuhifadhiwa, kwani tangu enzi ya dahari mababu zetu waliishi katika dunia hii. Tukitunga sheria za kulinda mazingira yetu, siku za mbele ndipo tutakapoweza kwenda sambamba na matakwa kwa kila zama, na tunaweza kujiendeleza vizuri vizazi kwa vizazi.

Bwana Okongo Okeya anasema, yeye mwenyewe ana njia moja tu ya kusikiliza Radio China kimataifa ambayo ni kipenzi chake cha radio, yeye hana televisheni wala kompyuta, lakini anasikiliza vipindi ananufaika sana na matangazo yetu, anaona polepole ndio mwendo. Anasema heshima kwa watangazaji na watayarishaji wa Radio China kimataifa kwa kazi zao, tumepata vipindi mbalimbali kutokana na sauti ya watangazaji wa Radio China kimataifa, kutokana na usikilizaji wa matangazo tumepata urafiki kutoka kwao, anasema udumu urafiki kati yetu na Radio China kimataifa.

Tunamshukuru Bwana Okongo Okeya kwa barua yake, kweli anatutia moyo sana, kila mara anatuletea barua akiandika maneno mengi ya kuwapongeza na kuwasifu wachina wenye werevu na bidii, tutachapa kazi zaidi ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-25