Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-25 18:40:36    
Mazungumzo ya duru la Doha yasimamishwa bila kikomo

cri

Baada ya kufanya mazungumzo kwa zaidi ya siku 1, mawaziri husika au wawakilishi wa ngazi ya juu wa nchi 6 wanachama muhimu wa Shirika la Biashara Duniani, WTO, ambazo ni Marekani, Umoja wa Ulaya, Japan, Australia, Brazil na India, walitangaza tarehe 24 huko Geneva kushindwa kabisa kwa jitihada za mwisho za kukwamua mazungumzo ya duru la Doha. Katibu mkuu wa WTO Bw. Pascal Lamy alitoa pendekezo kwa nchi zote wanachama kusimamisha mazungumzo ya duru la Doha bila kikomo, ambapo hawakuwa na chaguo lingine ila tu kukubali pendekezo hilo.

Sababu muhimu ya kushindwa kwa mazungumzo hayo ya pande 6 ni Marekani na Umoja wa Ulaya kukataa kupunguza masharti kwa kiwango cha kuridhisha kuhusu upunguzaji wa utoaji wa ruzuku ya kilimo na ushuru wa kilimo. Mwakilishi wa Brazil ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Celso Amorim alisema, kushindwa kwa mazungumzo tunaweza hata kusema ni maafa. Lakini mwakilishi wa biashara wa Marekani Bibi Susan Schwab na mwakilishi wa biashara wa Umoja wa Ulaya Bw. Peter Mandelson walilaumiana. Hivyo Bw. Pascal Lamy aliitisha mkutano wa dharura wa wajumbe wote wa WTO. Alisema utatuzi wa masuala hayo ungeweza kupatikana ili mradi kuwe na nia ya kisiasa. Tatizo lililopo ni kwamba nia hiyo ya kisiasa sasa haipo. Pendekezo alilotoa la kusimamisha mazungumzo ya duru la Doha ni kutaka pande husika zitafakari kwa makini.

Mazungumzo ya duru la Doha yamekwama mara kadhaa tangu yalipoanza mwaka 2001. Kutoka Doha hadi Cancun na kutoka Hong Kong hadi Geneva, mazungumzo ya duru la Doha yalikwenda mrama katika miaka 5 iliyopita, na lengo la kumaliza mazungumzo hayo kabla ya mwishoni mwa mwaka 2004 liliahirishwa hadi mwishoni mwa mwaka huu. Kutokana na uamuzi uliofikiwa kwenye mkutano wa mawaziri mwishoni mwa mwaka uliopita huko Hong Kong, nchi wanachama wa WTO zingepanga kwa hatua ya mwanzo mazungumzo ya kilimo na utaratibu wa uidhinishaji kwa bidhaa zisizo za kilimo kuingia sokoni kabla ya mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, ili kubuni mpango wa kupunguza masharti kabla ya mwezi Julai. Lakini tokea mwanzoni mwa mwaka huu, mazungumzo yote yaliyofanyika hayakupata maendeleo halisi.

Misimamo ya pande muhimu za washiriki wa mazungumzo ni kama ifuatavyo: Umoja wa Ulaya unaihimiza Marekani itangulie kupunguza masharti yake katika upunguzaji wa utoaji ruzuku ya kilimo, ni kufanya hivyo tu, ndipo Umoja wa Ulaya utaweza kulegeza msimamo wake; Marekani inataka Umoja wa Ulaya upunguze zaidi ushuru kwa mazao ya kilimo, ikidai hilo ni sharti la kwanza kwa Marekani kukubali usuluhisho; mbali na mchuano huo kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya, sasa pande hizo mbili zimeshirikiana kutoa shinikizo kwa nchi zinazoendelea zikitaka nchi zinazoendelea zipunguze masharti kwa bidhaa zisizo za kilimo kuingia katika masoko yao; Nchi zinazoendelea zinaona Marekani na Umoja wa Ulaya zinatakiwa kufikiria msimamo wa nchi zinazoendelea na kutangualia kupunguza masharti. Ni mvutano huo wa pande tatu, ambao umekwamisha mazungumzo ya duru la Doha.

Tukichunguza kwa undani chanzo cha mgogoro wa mazungumzo ya duru la Doha, tutaona kuwa chanzo muhimu zaidi ni nchi zilizoendelea kukosa nia ya kisiasa ya kupunguza ruzuku ya kilimo na ushuru wa mazao ya kilimo. Hadi hivi sasa Marekani bado haijamaliza kurekebisha muundo wa ajira wa nchi yake, ambao unafanya watu wengi wa Marekani kutoweza kukabiliana na mkumbo unaoletwa na soko huria, na kuleta upinzani dhidi ya utandawazi. Hususan ni kwamba uchaguzi wa kipindi cha kati nchini Marekani utafanyika mwaka 2007, hivyo Marekani hivi sasa haitaki kupunguza kihalisi utoaji ruzuku ya kilimo. Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zinapinga kufanya usuluhisho zaidi katika suala la kilimo, na Ufaransa ilimshutumu mara kwa mara mjumbe wa biashara wa Umoja wa Ulaya kufanya usuluhisho mkubwa katika suala hilo.

Idhaa ya Kiswahili 2006-07-25