Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-27 18:04:15    
Mkutano wa kimataifa wa suala la Lebanon na Israeli haujapata mafanikio makubwa

cri

Mkutano wa kimataifa uliofanyika kwa siku 1 huko Rome ulifungwa tarehe 26 mwezi huu. Ingawa washiriki wa mkutano walitoa taarifa ya pamoja mwishoni mwa mkutano ya kuhimiza pande mbili zinazopambana za Israel na Lebanon zimalize haraka iwezekanavyo mapigano ya kisilaha na makabiliano ya kiuhasama, kutimiza usimamishaji mapigano na kuomba kupeleka huko jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa, lakini vyombo vya habari vinaona kutokana na tofauti kubwa kati ya misimamo ya washiriki wa mkutano, mkutano huo haukuweka ratiba kamili kuhusu usitishaji wa mapigano hayo, utoaji misaada ya kibinadamu na upelekaji wa jeshi la kulinda amani, kwa hiyo vinaona, mkutano huo haukupata mafanikio makubwa.

Mkutano huo wa kimataifa kuhusu suala la Lebanon na Israel ulifanyika kutokana na pendekezo la Italia na Marekani kwa pamoja, ili kutatua baadhi ya masuala ya kimsingi ya mapambano kati ya Israel na Lebanon yakiwemo kuhimiza pande mbili kusimamisha mapigano, kuweka jeshi la kulinda amani sehemu ya kusini mwa Lebanon na kutoa misaada ya kibinadamu kwa sehemu iliyokumbwa na mgogoro. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na maofisa kutoka Italia, Marekani, Lebanon, Saudi Arabia, Misri, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Russia, na Uturuki pamoja na wajumbe wa Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya walishiriki kwenye mkutano huo. Taarifa iliyotolewa wakati wa kufungwa kwa mkutano inasema, jumuiya ya kimataifa itachukua hatua kamili na kuendelea kujitahidi kuleta amani katika sehemu yenye mgogoro. Lakini vyombo vya habari vinasema, sababu za mkutano huo kutofikia makubaliano kuhusu masuala halisi ni kama zifuatazo:

Kwanza mgogoro kati ya Lebanon na Israel umesababishwa na mambo mengi ya kihistoria na ya siku za karibuni. Hivi sasa masuala muhimu yanayohusiana mgogoro ni pamoja na kusimamisha mapigano; Kuwaachia huru askari waliotekwa; Kupanga jeshi la kudumisha amani kusini mwa Lebanon; Chama cha Hezbollah kuvunja jeshi lake na serikali ya Lebanon kuimarisha udhibiti katika nchi nzima. Kuzuka na kutatuliwa kwa masuala hayo kunahusiana pamoja, katika hali ya namna hiyo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan anapinga kuchukulia moja ya masuala yaliyotajwa kuwa sharti la kwanza kwa utatuzi wa suala lingine, anataka pande zote mbili zichukue hatua kwa wakati mmoja, la siyo utatuzi wake hautapatikana. Lakini waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleezza Rice aliyeshiriki kwenye mkutano huo aliendelea kushikilia kuwa ni lazima Chama cha Hezbollah kitangulie kuvunja jeshi lake. Msimamo wa Marekani umeongeza shida kwenye utatuzi wa masuala hayo.

Pili pande muhimu zinazopambana za Lebanon na Israel zote hazikushiriki kwenye mkutano huo, licha ya hayo Syria na Iran, ambazo zinachukuliwa kuwa na uhusiano mkubwa na Chama cha Hezbollah cha Lebanon, pia hazikushiriki kwenye mkutano huo. Bw. Kofi Annan alisema, ni lazima kuzishirikisha Iran na Syria katika jitihada za kisiasa za utatuzi wa mgogoro kati ya Lebanon na Israel, lakini Bi Rice aliendelea kuilaani Syria na Iran kuharibu hali ya utulivu ya mashariki ya kati.

Tatu, kuhusu suala la kupeleka jeshi la kulinda amani katika sehemu ya kusini mwa Lebanon, ni dhahiri kuwa pande zote husika zina wasiwasi wake binafsi. Hivi sasa Marekani inayoiunga mkono Israel, imesema haitashiriki kwenye harakati za kulinda amani; msemaji wa jumuiya ya NATO hivi karibuni alisema, suala la kupeleka jeshi la kulinda amani halijawekwa katika ajenda ya mkutano wa NATO; wachambuzi wanasema, tofauti ya maoni kati ya nchi za magharibi kuhusu suala la kupeleka jeshi la kulinda amani safari hii inahusiana sana na mafunzo ya kihistoria. Katika kipindi cha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Lebanon mwaka 1982, Marekani, Ufaransa na nchi nyingine zilipeleka askari kushiriki kwenye jeshi la Umoja wa Mataifa na kuingia nchini Lebanon. Katika mwaka uliofuata Chama cha Hezbollah kilifanya mashambulizi ya kujitolea muhanga dhidi ya kambi za jeshi la Marekani, ambapo askari 241 wa jeshi la Marekani na askari 58 wa Ufaransa waliuawa.

Habari zinasema pande husika zitashiriki kwenye mkutano utakaofanyika wiki ijayo mjini New York kuhusu kupeleka jeshi la Umoja wa Mataifa. Mbali na hayo, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya pia watakuwa na mkutano maalumu wiki ijayo kuhusu mgogoro kati ya Lebanon na Israel.

Idhaa ya Kiswahili 2006-07-27