Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-28 15:32:56    
Afrika imenufaika kutokana na uhusiano wa kiwenzi kati yake na China

cri

Katibu mtendaji mkuu wa Mfuko wa kuandaa uwezo wa Afrika (ACBF) aliyekuwa waziri mkuu wa Mali Bw. Soumana Sacko hivi karibuni alipohojiwa na mwandishi wa habari wa China huko Harare, makao makuu ya Mfuko huo alivikosoa vyombo vya habari vya nchi za magharibi kuhusu ati China inataka kuifanya Afrika iwe koloni lake, na alisema Afrika inanufaika kutokana na uhusiano na ushirikiano wa kiwenzi na China.

Bw. Sacko alisema usemi wa nchi za magharibi kuhusu China kutaka kuifanya Afrika iwe koloni lake hauna msingi hata kidogo, hakuna ushahidi wowote unaoweza kuthibitisha kuwa, nchi za Afrika zimepoteza kitu wakati wa kufanya mawasiliano na China, kinyume chake ni kuwa nchi za Afrika zimenufaika sana kutokana na uhusiano kati yake na China.

Bw. Sacko alisema vyombo vya habari vya nchi za magharibi vinakosoa kuwa, China kushughulikia ujenzi wa miundo mbinu katika nchi za Afrika ni kusafirisha nguvu kazi ya watu wanaopewa mishahara midogo tu barani Afrika, na hali hiyo imesababisha Waafrika wengi kukosa ajira. Lakini ukweli wa mambo ni tofauti kabisa, uwekezaji wa Wachina umeleta nafasi nyingi za ajira barani Afrika. Katika miaka ya karibuni nchi nyingi za Afrika zinaona kuwa, makampuni ya China yana uwezo mkubwa kwenye kugombea mikataba ya ujenzi wa miradi ya miundo mbinu iliyotolewa na serikali za Afrika. Tangu China ianze kuwekeza na kufanya biashara barani Afrika, imeleta bidhaa za aina mbalimbali zenye bei nafuu na sifa bora barani Afrika, na nchi za Afrika zinaweza kuagiza bidhaa za ngazi tofauti kutoka China kulingana na uwezo wa wakazi wake wa kununua bidhaa hizo.

Alipozungumzia uhusiano wa kiwenzi kati ya nchi za Afrika na China katika mambo ya siasa Bw. Sacko alisema, uhusiano mzuri kati ya China na Afrika umehakikisha kuwa maazimio yaliyopitishwa na mashirika ya kimataifa yanaweza kuzinufaisha nchi maskini, wala siyo nchi kubwa zilizoendelea. Katika mchakato wa kufanya mageuzi ya Umoja wa Mataifa, China na nchi za Afrika pia zina maslahi ya aina moja.

Bw. Sacko alisema nchi nyingi za Afrika zinaona China inaheshimu mamlaka ya nchi nyingine, kuziruhusu nchi nyingine zijitawale na kuchagua sera zao za kiuchumi kutokana na hali halisi za nchi hizo, na China haipendi kuzilazimisha nchi nyingine kukubali maoni yake. Ukweli wa mambo umeonesha kuwa China inaheshimu sana nchi za Afrika, inajitahidi kuziunga mkono kwa kuzipa msaada, wala siyo kwa njia ya kuzishinikiza kupokea maoni yake au kuziadhibu.

Bw. Sacko alisema baada ya Mali kupata uhuru katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, China iliisaidia nchi hiyo kuanzisha kiwanda cha kwanza. China kufanya hivyo siyo kutokana na kuinyonya nchi hiyo, bali kulitokana na kuisaidia Mali iimarishe uhuru wake wa kisiasa kwa kujiendeleza kiuchumi. Reli ya TAZARA ni mfano mwingine mzuri. Aidha, China imezisaidia nchi za Afrika kwa kutoa mafunzo kwa wataalam wake wengi wa sekta mbalimbali. China ilikuwa, na itaendelea kuwa rafiki mkubwa wa nchi za Afrika.

Bw. Sacko aliwahi kufanya ziara nchini China mwaka 1985, alitumai kupata fursa nyingine ya kuitembelea China, ili kuona kwa macho yake mwenyewe mabadiliko makubwa yaliyotokea nchini China. Alisema uzoefu mkubwa ilioupata China katika mageuzi ya kiuchumi na kuvutia uwekezaji wa nchi za nje, unastahiki kuigwa na nchi za Afrika. Uzoefu wa China bila shaka utazinufaisha nchi za Afrika zinazosumbuliwa na matatizo ya kiuchumi.

Mfuko wa kuandaa uwezo wa Afrika ulianzishwa mwaka 1991 huko Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, hivi sasa una wanachama 34. Kauli mbiu ya mfuko huo ni kuwapatia viongozi wa Afrika utaratibu wa kuandaa uwezo, kuhimiza maendeleo ya serikali na jamii ya Afrika, na kuhimiza maelewano na ushirikiano kati ya nchi wanachama kwa njia mbalimbali ili kuinua uwezo wa serikali za nchi za Afrika kuongoza nchi zao na uwezo wa kuleta maendeleo endelevu. Bw. Sacko ameshika madaraka ya katibu mtendaji mkuu wa Mfuko huo kuanzia mwaka 2000, yeye ni kiongozi mkuu wa mfuko huo.

Idhaa ya kiswahili 2006-07-28