Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-07-31 20:40:00    
Uchaguzi mkuu Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wafanyika katika hali ya shwari nchini

cri

Uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ulifanyika tarehe 30, huu ni uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia kufanyika nchini humo tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1960. Siku hiyo wananchi wa nchi hiyo walimiminika kwenye vituo vya kupigia kura wakiwa na matarajio makubwa juu ya demokrasia na amani ya nchi hiyo katika siku za usoni, wakipiga kura kumchagua rais na bunge la taifa la nchi hiyo.

Upigaji kura ulianza saa 12 asubuhi na kumalizika saa 11 jioni siku hiyo ya saa za huko, ingawa baadhi ya wapinzani waliosusia uchaguzi huo walifanya shughuli kadhaa za uharibufu, lakini kwa ujumla kazi ya upigaji kura ulifanyika kwa utaratibu.

Huko Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, mpiga kura mwanaume aliyevaa nguo ya sikukuu alisema, uchaguzi huo ni tukio kubwa. Mwaka huu nimetimiza umri wa miaka 44, lakini hii ni mara yangu ya kwanza kupata fursa ya kupiga kura, nataka kuchagua serikali yetu mpya na viongozi wetu hodari. Katika sehemu ya mashariki ya nchi hiyo, mpiga kura mwanamke mwenye umri wa miaka 60 alisema, tumechoshwa na vita, nina matumaini kuwa nchi yetu itakuwa nchi yenye usalama.

Ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika bila matatizo, Umoja wa Mataifa ulituma kikosi cha kulinda amani chenye watu elfu 17 kwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kutuma walinzi wengi namna hii kwenye nchi moja. Aidha Umoja wa Ulaya pia ulituma kikosi cha kulinda amani kilichoundwa na watu 2,400 kutoka nchi 21 za Ulaya.

Katika uchaguzi huo mkuu, wagombea wa urais wamefikia 33 akiwemo rais wa mpito wa nchi hiyo Bw Joseph. Wakati huo huo wagombea wapatao 9,700 wamegombea viti 500 kwenye baraza la chini la bunge la nchi hiyo. Hivi sasa Bwana Kabila anaongoza kwa asilimia 35 ya kura za maoni ya raia, lakini kiasi hiki ni chini sana cha kile cha asilimia 50 kinachotakiwa ili apate ushindi katika duru la kwanza la upigaji kura. Mgombea mwingine mwenye nguvu wa pili ni makamu wa rais wa sasa Bwana Jean Pierre Bemba kutoka "Chama cha ukombozi wa Congo". Kutokana na katiba ya nchi hiyo, kama hakuna mgombea atakayeshinda katika duru la kwanza la upigaji kura, basi wagombea wawili waliopata kura nyingi zaidi kuliko wengi watagombea tena katika duru la pili la upigaji kura. Tume huru ya uchaguzi ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ilisema, matokeo ya duru la kwanza la upigaji kura yatajulikana ndani ya wiki tatu.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo iko katikati ya Bara la Afrika, inajulikana kwa jina lake lingine "moyo wa Afrika". Nchi hiyo ina maliasili nyingi za madini, lakini vurugu za vita zilizodumu kwa miaka mingi zimeiletea nchi hiyo balaa kubwa. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilitokea nchini humo mwaka 1998, katika miaka minne baada ya hapo, watu milioni 2 na laki 5 wa nchi hiyo walikufa katika vita, na watu laki 4 walikuwa wakimbizi. Kutokana na juhudi kubwa za usuluhishi za jumuiya ya kimataifa, pande zilizopambana za nchi hiyo zilisaini makubaliano ya kusimamisha vita mwaka 1999, lakini makubaliano hayo hayakutekelezwa vizuri, na migogoro ilitokea mara kwa mara. Mwezi Aprili mwaka 2003, Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na makundi mbalimbali vilifikia maoni ya pamoja kuhusu ugawaji wa madaraka katika kipindi cha mpito. Mwezi Juni mwaka huo, serikali ya mpito ya nchi hiyo ilianzishwa, na Bwana Joseph Kabila alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo katika kipindi cha mpito.

Mchunguzi wa kijeshi wa tume maalum la Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo alisema, katika siku ya uchaguzi mkuu, hazikutokea shughuli nyingi za kimabavu katika sehemu ya kitongoji cha mashariki cha Kinshasa ambapo ni sehemu yenye wapinzani wengi zaidi, hali ya usalama ni shwari kwa ujumla huko Kinshasa. Kufanyika kwa uchaguzi huo mkuu bila matatizo kumeonesha kuwa, wananchi wa nchi hiyo wana kiu juu ya amani, na jumuiya ya kimataifa inatarajia uchaguzi huo utafanikiwa, na nchi hiyo itafuata njia ya amani na maendeleo kuanzia hapo.