Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-01 15:10:49    
Barua 0730

cri

Msikilizaji wetu Mary D. Ndunguru wa S.L.P 8145, Arusha, Tanzania katika barua yake kwanza ametoa shukrani zake kwa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kuendelea kumkumbuka na kumtumia kalenda ya mwaka 2006. Alisema hakosi kusikiliza vipindi vya Kiswahili vya Radio China Kimataifa kupitia KBC, lakini bado hajaanza kusikiliza kupitia wimbi la FM.

Bibi Ndunguru anaona vipindi vya CRI vinatosheleza mahitaji ya walengwa. Na anapendekeza tuangalie ni vipindi gani viongezwe ili viwavutie wasikilizaji wengi zaidi. Anadhani kungekuwa na kipindi cha hadithi za wasikilizaji, yaani msikilizaji atunge hadithi ya kubuni na kuitumia Idhaa ya Kiswahili ili tuangalie ikifaa tuisome radioni.

Bibi Ndunguru pia anasema Kipindi cha Daraja la Urafiki kati ya China na Afrika kinamvutia sana. Kweli China ni nchi yenye ukarimu na urafiki wa kweli. Pia kipindi cha nyimbo za Kichina vile vile kinamvutia. Katika barua hiyo Bibi Ndunguru pia alitutumia shairi alilotunga yeye mwenyewe. Beti za shairihizo zinasema

Radio China Kimataifa, yastahili pongezi

Kiswahili chenye sifa, kama ua zuri

Watangazaji wenye sifa, wastahili pongezi

Radio China Kimataifa, wote twaisikiliza

Wamefungua vituo, Kenya na nchi jirani

Wasikilizaji wenye vyeo, nao wapo hewani

Kusikiliza idhaa yao, ichanuanayo kama thamani

Shime tusikilizeni, Radio China Kimataifa

Mimi pia sibanduki, muanzapo matangazo.

Huwa kama mkuki, uwapo kwenye nguzo.

Hata niwe na kazi lukuki, huko kama nguzo.

Pongezi watangazaji, kutuandalia vipindi.

Mheshimiwa Rais wa China, Hu Jintao Karibu kwetu.

Jamii zetu wa ndugu, Ifurahie Kenya yetu.

Kwa shangwe tunakulaki, Sisi Wakenya tunakuheshimu.

Tunatambua mengi hisani, Shukrani kwa serikali ya Uchina.

Misaada twaipokea, elimu twanufaika nayo.

Biashara inashamiri, utamaduni twabadilishana.

Mazingira twafundishana, habari za China twazipokea.

Utalii umeimarika, Yote twajivunia.

Wakenya shukrani uzipokee.

Mwisho nafikia kikomo, kwa kumpongeza balozi.

Na ubalozi juhudi mmefanya uhusiano sasa umeimarika.

Heko balozi heko ubalozi, natoa mwito wangu Wakenya.

Tuzidishe juhudi zetu, Uhusiano tuimarishe

Tupanue biashara zetu, na utaalamu tubadilishane

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mary D. Ndunguru kwa barua yake na shairi lake alilotutumia, kweli tumetiwa moyo sana. Maoni yake kuhusu wasikilizaji waandike hadithi na kututumia ili tuisome, hayo ni maoni mazuri, zamani wasikilizaji wetu wengi wa Tanzania waliwahi kututumia hadithi nyingi. Tunaona kwa kuungwa mkono na wasikilizaji wetu wengi, hakika tutaboresha zaidi vipindi vyetu ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Philip M. Machuki wa S.L.P 646 Kisii, Kenya ametuandika barua akitoa pongezi kwa uzinduzi wa kituo cha FM huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya. Anasema hii ni kama tuzo kubwa sana kwa wasikilizaji ambayo wamepewa na mkuu wa Radio China kimataifa. Na ingawa yeye na wasikilizaji wengine wengi hawakuweza kukutana na mkuu wa RadioChina kimataifa huko Nairobi kwa sababu za kimasomo, lakini wale ambao waliwawakilisha wasikilizaji wengine huko kwa kweli walikuwa na furaha isiyo kifani wakati wa uzinduzi wa kituo hicho.

Anaona bila shaka wasikilizaji wa Radio China kimataifa huko Kenya wataongezeka. Anasema muda wa matangazo ya idhaa ya Kiswahili yaani saa tatu kwa siku ni bora sana, na bila shaka wasikilizaji wengi watapata muda wa kusikiliza matangazo hayo. Pia anapenda kuifahamisha Radio China kimataifa kuwa matangazo haya huwa hayasikiki mjini Nairobi peke yake, huwa pia yanapokelewa na miji inayozunguka mji wa Nairobi. Yeye na wasikilizaji wa Nyankware wamegundua hilo wakati walipoamua kuyachunguza katika usikilizaji wa Radio China kimataifa kwenye maeneo yalio karibu na Nairobi.

Anasema shughuli hii iliwachukua siku mbili, na pia walipata kukusanya maoni ya baadhi ya watu wa miji hiyo, ambao wengi waliokutana na Bw Machuki walipongeza matangazo ya Radio China Kimataifa, na wengine wachache walisema bado hawajawahi kusikiliza matangazo haya, lakini lilikuwa ni jukumu lao kuwaelezea juu ya kituo cha FM cha Radio China kimataifa, nao waliitikia wito wa Bw. Machuki na kuanza kusikiliza matangazo hayo pamoja. Pia anatarajia kuwa kadri siku zinavyosonga mbele, ndivyo matangazo ya Radio China Kimataifa kwa njia ya FM yatakuwa na umaarufu zaidi huko Afrika mashariki.

Tunamshukuru sana Bwana Machuki kwa juhudi zake za kutusaidia kupata maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wetu, ambayo yanaweza kutusaidia kuboresha vipindi vyetu, sisi tutaendelea kuchapa kazi ili kuboresha zaidi matangazo yetu.

Na msikilizaji wetu wa Kenya Mwalimu Wabwire ametuletea barua pepe akitoa maoni yake juu ya vipindi vyetu vya burudani za muziki, anasema si vizuri kurudiarudia burudani za muziki, yeye anatushauri tujitahidi kupiga muziki tofauti na sio kurudia mara kwa mara.

Tunakushukuru kwa dhati kwa barua yake pepe ambayo imetoa maoni mazuri. Kutokana na maandalizi ambayo hayakuweza kufanywa ipasavyo, kuna dosari kadha wa kadha zinazoweza kuonekana katika matangazo yetu, ingawa hayo yanatokana na hali ambayo kwenye idhaa yetu hivi sasa nguvu kazi siyo ya kutosha, watangazaji na watayarishaji wenye uwezo wa kufanya kazi ya kutafsiri bado ni wachache, na kila siku tunapaswa kurusha hewani matangazo ya saa moja moja, lakini kwenye maktaba yetu ya muziki hakuna muziki mwingi wa kiafrika, hivyo baadhi ya wakati kweli tulirudia matangazo yetu. Hapa tunaomba radhi, na pia tunaomba wasikilizaji wetu mtuvumilie tena kwa siku chache, tutafanya chini juu ili kurekebisha vipindi vyetu. Asante sana, ni matumaini yetu kuwa mwalimu ataendelea kutuletea barua na kutoa maoni na mapendekezo yake. Kweli ni wachache wanaoweza kutoa maoni kwa unyoofu namna hii, inatuonesha kuwa wewe ni msikilizaji wetu mzuri, tunakushukuru kwa dhati.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-01