Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-01 15:28:22    
Kununua nyumba kiungani kwa ajili ya mapumziko

cri

Ni jambo la kawaida kwa watu wenye mali nyingi kiasi wa nchi za magharibi kununua nyumba katika viunga kwa ajili ya mapumziko. Mtindo huo wa maisha ulikuwa ni tarajio lisiloweza kutimizwa na wachina katika miaka zaidi ya kumi iliyopita. Lakini hivi sasa kutokana na kuongezeka kwa pato na kuinuka kwa ubora wa maisha ya watu wa China, kununua nyumba viungani kumekuwa ni mtindo mpya wa maisha ya starehe nchini China.

Kuondoka mjini na kujaribu maisha ya vijijini, kufanya kazi za shambani, kula chakula kutoka kwa wakulima, kuwepo kwenye mazingira halisi ya kimaumbile ni maisha yanayotarajiwa sana na wakazi wa mjini wanaokabiliwa shinikizo kubwa la kazi. Hivi sasa mtindo huo wa kupumzika kwenye mazingira halisi ya kimaumbile unafuatiliwa sana na wakazi wa sehemu ya pwani yenye maendeleo makubwa ya kiuchumi nchini China.

Mkoa wa Zhejiang ni mmoja kati ya mikoa yenye watu wanaopenda maisha ya namna hiyo. Mwezi Oktoba mwaka uliopita, kampuni ya teknolojia ya sayansi ya kilimo ya Siji ya mji wa Hangzhou mkoani Zhejiang, ilianzisha mradi wa "Kijiji cha Mapumziko cha Anji". Habari zinasema hili ni shamba la kwanza na la binafsi ya klabu ya wanachama. Katika shamba hilo la klabu, mwanachama anamiliki nyumba ndogo ya mbao pamoja na hekta 0.06 ya shamba la michai au mboga kwa miaka 30.

Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Xie Wei alisema, mradi wa kipindi cha kwanza uliagizwa wote na watu ndani ya siku mbali baada ya kutolewa.

"Hivi sasa tuna nyumba za aina tatu, aina ya kwanza ni kwa ajili ya familia yenye watu 3 yenye choo, sebule, chumba kimoja pamoja na kibaraza. Aina ya pili ni kwa ajili ya familia yenye watu wengi kidogo, ikiwa na vyumba viwili, na sebule moja. Aina nyingine ni yenye vyumba vinne, sebule mbili, vyoo viwili na sehemu ya jiko."

Habari zinasema nyumba hizo za shambani zinakodiwa kwa Yuan kati ya elfu 90 na laki 1, na bei zake zinatofautiana kidogo kutokana na ukubwa wa nyumba na mahali zilipo. Bw. Xie Wei alisema, faida zinazopatikana kutokana na kodi za nyumba za wanachama ni za wanachama. Wakati wenyewe wasipoishi katika nyumba hizo za mbao, wasimamizi wa shamba la michai wanaweza kuwasaidia kupangisha nyumba zao, na pato kutokana na kodi za nyumba ni la wanachama wenye nyumba.

Bw. Chen Ming na mke wake Bibi Zhang Li ni wateja wa kampuni ya teknolojia ya sayansi ya kilimo ya Siji. Mmoja alikuwa ni mwalimu na mwingine alikuwa ni mfanyakazi wa kampuni moja ya utalii. Walistaafu mwaka 2000. Bw. Chen na mkewe wana nyumba yao mjini Hangzhou, mazingira ya makazi ni mazuri, lakini wanataka kuishi maisha ya shambani ili waweza kupanda wenyewe maua na mboga. Si siku nyingi zilizopita, walivutiwa na mradi huo wa kampuni ya Siji katika matangazo ya magazeti na televisheni, walifurahi na walikwenda kufanya uchunguzi huko. Bw. Chen alisema,

"Tulifanya uchunguzi mara mbili, mara ya kwanza ilinyesha mvua, hapo baadaye tulichagua siku nzuri kwenda huko tena, tumevutiwa na mazingira ya aina zote mbili, hususan yenye mvua, shamba lenye michai ya rangi ya kijani lilituvutia sana."

Bw. Chen Ming na mkewe waliamua kununua nyumba ya mbao yenye eneo la mita za mraba 67, siyo kwa ajili yao wenyewe, bali pia walikuwa na mpango wa kuwaalika marafiki zao. Hivi sasa wanasubiri kuhamia huko mara tu baada ya ujenzi kukamilika, huko wanapata hewa safi ya mlimani na kula mboga wanazopanda wao wenyewe. Kila mara wanapofikiria mambo hayo wanafurahi sana. Ni hakika kwamba katika siku za baadaye, wataishi huko kwa muda mrefu zaidi. Bw. Chen Ming na mkewe walisema, kununua nyumba sehemu ya shambani sio kununua nyumba peke yake, bali pia amenunua afya.

Watu wengi wana wazo kama la Bw. Chen Ming, hususan wazee waliostaafu. Naibu meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Zhang Yonggui alisema, kiasi cha 90% ya wateja wao ni wakazi wa mjini waliostaafu au ambao wako karibu kustaafu.

"Karibu wote wako katika hali ya namna hiyo, ingawa baadhi yao hawajastaafu, lakini watastaafu baada ya miaka michache, kwa mfano mhadhiri wa chuo kikuu cha Zhejiang Bw Li alisema, atafika hapa kufuga kuku baada ya kustaafu. Siku ile alikuja pamoja na mtoto mmoja, mtoto yule alifurahi sana na kukimbia huku na huko, mwalimu Li na mkewe pia walifurahi sana."

Habari zinasema hivi sasa wilaya na miji mingi ya mkoa wa Zhejiang imetoa miradi inayofanana na makazi ya mashambani au nyumba za ghorofa. Ikilinganishwa na mashamba binafsi, nyumba za ghorofa za sehemu yenye mandhari nzuri ya mlima wa Tianmu ya kampuni ya kilimo ya Lianzhong ya mji wa Hangzhou ingawa siyo nzuri kama zile nyumba za mashamba ya michai, lakini bei yake ni ya kuvutia watu zaidi, ambapo mtu akituamia Yuan elfu kumi kadhaa anaweza kupata nyumba yenye mita za mraba 50 hivi kwa miaka 30. Meneja mkuu wa kampuni ya Lianzhong Bw. Yu Xuebing alisema, mradi wao huo ni kujenga upya makazi ya wakulima kwa kufanya ushirikiano na wanakijiji wa huko. Bw. Yu alisema hivi sasa nyumba zote za ghorofa zilizoko kwenye mlima wa Tianmu zimeuzwa. Alipozungumzia mafanikio ya mradi huo, Bw. Yu Xuebing alisema, mafanikio hayo yanatokana na kupamba moto kwa utalii wa sehemu za vijijini za mkoa wa Zhejiang katika miaka ya karibuni. Alisema katika miaka ya karibuni utalii wa sehemu za vijiji unapendwa na watu, hata kufikia kiwango cha kushindwa kukidhi mahitaji ya watalii. Wakulima wengi wanataka kushiriki katika shughuli hizo isipokuwa wanakosa fedha za kutosha kujenga upya nyumba zao. Hivyo kampuni yao ilikuwa na wazo la kuwasaidia wakulima kujenga upya makazi ya wakulima na kujenga nyumba za ghorofa. Wanakijiji walikuwa na juhudi kubwa ya kushiriki na kuwekeza katika ukarabati wa makazi yao. Baada ya ujenzi mpya, sura za vijiji vingi zimebadilika, si kama tu mazingira ya kuishi wakulima yameboreshwa, bali pia pato lao limeongezeka. Kwa makadirio wastani wa ongezeko la familia ya mkulima unaongezeka kwa Yuan elfu 20 kwa mwaka.

Ujenzi wa miradi kadhaa ya kampuni ya Lianzhong kwenye Mlima wa Tianmu na ziwa la Qiandao hivi sasa bado unaendelea, Bw. Yu Xuebing ana imani kubwa kuhusu mauzo ya nyumba hizo. Alisema ili kuvutia wateja, hivi sasa licha ya kujenga nyumba, kampuni inawasiliana na idara husika za huko kuhusu namna ya kuboresha zana zinazoambatana na makazi, zikiwemo hospitali, majengo ya mazoezi ya mwili na maktaba. Wamenuia kujenga sehemu ya huko kuwa mahali pazuri pa kuishi penye huduma za aina mbalimbali, ambapo wakazi hawataona shida yoyote wakati wa kununua vitu vya mahitaji pamoja na kwenda kuwaona madaktari.

Bw. Hu Jian ambaye anafanya kazi katika kampuni moja ya Hangzhou, mji mkuu wa mkoa wa Zhejiang. Alisema amenunua nyumba huko kutokana na kuvutiwa na hewa safi na mazingira ya huko ya kupendeza.

Bw. Hu alisema hivi sasa watu wengi wanapenda kupumzika katika sehemu ya vijiji, endapo mtu anapanga nyumba ya mkulima anatakiwa kulipa kiasi cha Yuan 30. Ikiwa analipa kwa mara moja, kama anaitumia kwa miaka 30, basi gharama yake ni kiasi cha Yuan 200 kwa mwezi, hivyo ni nafuu kwake.

Lakini Bw. Hu alisema hivi sasa hakai sana katika nyumba yake iliyoko sehemu ya mlima wa Tianmu isipokuwa siku chache za majira ya joto, atafikiria kukaa kwa muda mrefu huko baada ya ujenzi wa huduma kukamilishwa ukiwa ni pamoja na mawasiliano, hospitali na maduka. Bw. Hu Jian alisema hana wasiwasi kuhusu hasara ambayo amenunua nyumba na haitumii, kwani kampuni ya Lianzhong itamsaidia kukodisha nyumba yake kwa mtu mwingine ikiwa ni faida ya kuwekeza katika makazi ya sehemu ya vijiji.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-01