Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-01 18:27:37    
"Sehemu kubwa ya mashariki ya kati" na "sehemu mpya ya mashariki ya kati" inayotarajia Marekani

cri

Tangu kuzuka mapigano ya kisilaha kati ya Israel na jeshi la chama cha Hezbollah nchini Lebanon, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice amefanya usuluhisho mara mbili kwenye sehemu ya mashariki ya kati. Jambo linalostahili kutupiwa macho ni kuwa bibi Rice hakuihimiza Israel kusimamisha vitendo vya kijeshi, wala hakubali kusimamisha mapigano mara moja, bali alitoa wazo la "sehemu mpya ya mashariki ya kati". "Sehemu mpya ya mashariki ya kati" ina tofauti gani na ule "mpango wa sehemu kubwa ya mashariki ya kati" uliotolewa na Marekani hapo awali? Na kwanini Marekani inatoa wazo hilo la "sehemu mpya ya mashariki ya kati"?

Baada ya kutokea kwa tukio la "Septemba 11", ugaidi ulienea duniani. Ili kupambana na ugaidi, Marekani ilinuia kutoa mpango wa mageuzi ya demokrasia ya sehemu kubwa ya mashariki ya kati kabla na baada ya vita ya Iraq mwaka 2003, ambao ulitolewa rasmi na rais Bush katika taarifa ya hali ya nchi ya mwaka 2004. Mpango huo unazihusisha nchi 22 za kiarabu zikiwemo Israel, Uturuki, Iran, Afghanistan na Pakistan. Marekani inatumai kufanyika mageuzi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, kuhimiza sehemu ya mashariki ya kati kufuata utaratibu unaojulikana wa demokrasia na kutokomeza msingi wa ugaidi. Hali halisi ni kutaka "kurekebisha" mashariki kwa mbinu ya "demokrasia" na kutimiza "amani inayoongozwa na wamarekani" kwenye sehemu ya mashariki ya kati ili kuhakikisha manufaa ya Marekani mkakati na mafuta ghafi ya petroli katika sehemu ya mashariki ya kati.

Ili kuhimiza utekelezaji wa mpango huo, Marekani inajaribu kuweka mfano mpya wa demokrasia kwenye mashariki ya kati. Kwanza kabisa Marekani iliangusha utawala wa Saddam Hussein, kisha inaunga mkono utawala unaoiunga mkono Marekani, lakini demokrasia hiyo ya jina tu haikuweza kuondoa migongano iliyoko kati ya makundi mbalimbali ya ndani ya serikali ya Iraq. Hadi hivi sasa hali ya nchini Iraq bado ni yenye mgogoro, mapambano kati ya madhehebu yanaongezeka, wanamgambo wanaoipinga Marekani wanaendelea kuleta matata, na Marekani imenaswa katika matatizo nchini Iraq. Nchi moja tu ya Iraq imefanya Marekani ikabiliane na shida, sembuse kurekebisha Iran na Syria, ambazo zinaichukiza sana Marekani, kwa hiyo mpango wa Marekani wa "sehemu kubwa ya mashariki ya kati" umepatwa matatizo mengi.

Mgogoro ulioko hivi sasa kati ya Lebanon na Israel umezidisha vurugu ya sehemu ya mashariki ya kati. Si kama tu Marekani inaiacha Israel iimarishe mashambulizi, bali pia ilipiga kura ya turufu kuhusu azimio la kulitaka baraza la usalama liamuru kusimamishwa kwa mapambano. Kwa kuwa Marekani inaona mgogoro kati ya Lebanon na Israel umeleta nafasi nzuri kwa utekelezaji wa "mpango wa sehemu kubwa ya mashariki ya kati". Marekani inatarajia mgogoro huo unaweza kuleta "sehemu mpya ya mashariki ya kati inayotofautiana na ile ya zamani", ambayo ni ile aliyotaja bibi Rice.

Kwa kufuata mpango wa "sehemu mpya ya mashariki ya kati", Marekani inataka kutimiza lengo la kutoa shinikizo kwa chama cha Hezbollah na kudhoofisha nguvu ya Syria na kuitenga Iran kwa kutumia mikono ya Israel, na kuondoa vikwazo muhimu hivyo kwenye njia ya kutekeleza "mpango wa sehemu kubwa ya mashariki ya kati". Marekani inaona, Israel kushambulia jeshi la chama cha Hezbollah, kwa upande mmoja kunaweza kudhoofisha nguvu ya Syria na Iran, ambazo zinakiunga mkono chama cha Hezbollah na kuleta nafasi kwa Marekani kuikabili Iran, kwa upande mwingine inaweza kuimarisha nguvu ya watu wanaoziunga mkono nchi za magharibi wa nchini Lebanon na kubadilisha hali ya kisiasa iliyopo hivi sasa nchini Lebanon.

Wachambuzi wanasema, mpango wa "sehemu mpya ya mashariki ya kati" ni sawa na "mpango wa sehemu kubwa ya mashariki ya kati", isipokuwa ni "mbinu yenye hatari" ya "mpango wa sehemu kubwa ya mashariki ya kati".