Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-02 19:33:00    
Matangazo ya kitarakimu ya televisheni yawaburudisha watazamaji

cri

Nchi 101 za Ulaya, Afrika na Mashariki ya Kati zimepanga kusimamisha matangazo ya analog ya televisheni kabla ya mwaka 2015, na kuanza kutumia matangazo ya kitarakimu kikamilifu. China pia ina mpango unaofanana wa kueneza matangazo ya kitarakimu ya televisheni. Hivi sasa watumiaji wa televisheni zaidi ya milioni 4 wa China wanaburudishwa kwa matangazo ya kitarakimu ya televisheni, pia wanaweza kuagiza vipindi, kununua vitu, kujiandikisha hospitali au kununua hisa kupitia huduma hiyo.

Matangazo ya televisheni ya kitarakimu yanaoneshwa kwa picha safi na sauti bora, vipindi vyingi zaidi kuliko matangazo ya kianalog ambayo yanatumika sana hivi sasa. Mbali na hayo, matangazo ya kitarakimu pia yamebadilisha tabia ya kutazama televisheni, kwa sababu watazamaji wanaweza kuchagua kuangalia vipindi wanavyovipenda. Jambo linalovutia zaidi ni kwamba televisheni ya kitarakimu pia inaweza kufanya baadhi ya kazi za kompyuta, na kuwaletea watu urahisi katika maisha ya kila siku.

Mzee Wang Qinpu anayeishi mjini Hangzhou ana umri wa miaka 77. Televisheni imekuwa ni chombo muhimu kinachomburudisha maishani. Mwaka mmoja uliopita, mzee huyo alipata televisheni ya kitarakimu. Mzee Wang Qinpu alisema, hivi sasa si kama tu anaweza kutamaza vipindi vingi zaidi vya televisheni, bali pia anaweza kununua vitabu anavyovipenda kwa kupitia televisheni hiyo. Mzee Wang alisema:

"tunatazama ordha ya vitabu vinavyonunuliwa kwa wingi kwenye televisheni hiyo, kama nikiona vitabu ninavyovipenda, nitavinunua papo hapo kwa kupitia televisheni. Huduma hii ni rahisi sana"

baada ya maendeleo ya miaka ya hivi karibuni, hivi sasa kazi za kukusanya, kuhariri, kutangaza na kurusha matangazo ya televisheni nchini China zimekuwa za kitarakimu, lakini televisheni nyingi zinazopokea matangazo hayo bado ni za kianalog. Hivi sasa televisheni za kitarakimu zimeanza kuenezwa katika miji mingi nchini China. Naibu meneja wa kampuni ya matangazo ya televisheni ya kitarakimu ya mji wa Hangzhou Bw. Zheng Xiaolin alieleza, hivi sasa njia ya kupokea matangazo ya kitarakimu ni kutegemea kuweka zana ya ubadilishaji wa matangazo ya kitarakimu kwenye televisheni ya kianalog. Alisema,

"Tofauti na televisheni ya kianalog, televisheni ya kitarakimu ina njia pana zaidi ya kusafirisha vipindi vya televisheni, zamani kwenye matangazo ya kianalog vipindi kumi kadhaa tu viliweza kuoneshwa kwenye televisheni, lakini kwenye matangazo ya kitarakimu vipindi mia kadhaa vinaweza kuoneshwa kwa watazamaji, tena ubora wake kusafirisha matangazo umeinuliwa. Televisheni ya kitarakimu inafanya kazi kama kompyuta ndogo, lakini kuiendesha ni rahisi zaidi. Zamani watu walipokea matangazo ya televisheni, hivi sasa wanaweza kuchagua na kuagiza vipindi vya televisheni. "

Kwa mujibu wa mpango wa kueneza matangazo ya televisheni ya kitarakimu uliowekwa na serikali ya China, China pia itasimamisha matangazo ya kianalog kabla ya mwaka 2015, na kuyafanya yawe ya kitarakimu kote nchini China. Naibu mkurugenzi wa idara ya teknolojia katika idara kuu ya radio, televisheni na filamu ya taifa ya China Bw. Wang Lian alisema:

"tumeweka mpango wa kuendelea matangazo ya televisheni ya kitarakimu kwa vipindi vinne na sehemu tatu yaani sehemu ya mashariki, ya kati na ya magharibi, na tunajitahidi kutimiza lengo hilo kabla ya mwaka 2015."

Mpaka hivi sasa, zaidi ya watu milioni 4 nchini China wnatumia televisheni ya kitarakimu, ambapo si kama tu wanaweza kutamaza vipindi mbalimbali vya televisheni vyenye picha safi na sauti nzuri kama DVD, pia wanaweza kupata huduma mbalimbali na taarifa za habari zikiwemo taarifa kuhusu utamaduni na elimu, taarifa ya moja kwa moja ya mawasiliano barabarani.

Kwa mfano wa mjini Hangzhou, idara husika ya huko imeanzisha huduma mbalimbali kupitia televisheni ya kitarakimu. Ofisa wa kampuni ya televisheni ya kitarakimu ya Hangzhou Bi. Tang Yu alisema:

"tumeanzisha huduma mbalimbali zenye kulata urahisi kwa maisha ya watu. Kila siku watu zaidi ya laki 8.7 wanapata huduma yetu kupitia televisheni ya kitarakimu."

Mkazi wa mji wa Hangzhou Bw. Chen Hong ana kazi nyingi kila siku, na mtoto wake bado ni mdogo. Bw. Chen Hong alisema, huduma kwenye televisheni ya kitarakimu zinawapunguzia kazi ndogo za maisha zikiwemo kununua mchele na mafuta ya kupikia.

Mkazi mwingine Bibi Chu Mei amezoea kutumia huduma za televisheni ya kitarakimu: kila asubuhi kabla ya kwenda nje kufanya mazoezi, anasoma utabiri wa hali ya hewa kwenye televisheni, pia anaweza kuagiza vipindi mbalimbali anavyovipenda. Kinachomridhisha zaidi ni kwamba kupitia televisheni ya kitarakimu anaweza kuona maoni ya walimu wa shule anayosoma mtoto wake, mazoezi ya nyumbani ya mtoto wake na matokeo ya mitihani yake. Aidha mihadhara inayotolewa na walimu mashuhuri kila baada ya muda pia inamsaidia mtoto wake. Alisema:

"ni jambo zuri kwa watoto kusikiliza mihadhara ya walimu mashuhuri, lakini hakuna fursa nyingi kama hiyo. Hivi sasa kipindi hiki cha mihadhara ya walimu mashuhuri kinawafanya wanafunzi wengi zaidi waweze kunufaika na raslimali bora ya elimu. Naona ni kipindi kizuri sana."

Imefahamika kuwa, televisheni ni chombo cha upashanaji wa habari kinachotumiwa na watu wengi zaidi nchini China. Kiwango cha kumiliki televisheni ya rangi kwenye familia nchini China ni asilimia 130 mijini na asilimia 75 kwenye sehemu za vijiji. Habari kutoka idara kuu ya radio, televisheni na filamu ya taifa ya China zinasema, kazi ya kueneza matangazo ya televisheni ya kitarakimu hivi sasa inaendelea hatua kwa hatua kwenye sehemu ya magharibi ya kati ya China na sehemu zilizo nyuma kiuchumi, watu wengi zaidi si kama tu wataweza kuburudishwa na vipindi mbalimbali vya kitarakimu, bali pia wataichukulia televisheni kuwa msaidizi hodari kwenye maisha yao.