Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-02 19:42:53    
Daktari wa hospitali ya Kenyatta azumgumzia maambukizi wa Ukimwi kutoka mama kwenda kwa watoto

cri

Kutokana na takwimu zilizotolewa na wizara ya afya ya Kenya, akina mama milioni 1.5 nchini Kenya wanapata uja uzito, na kati ya hao, moja katika kumi wana virusi vya Ukimwi. Utafiti unaonesha kwamba kuna uwezekano mkubwa kiasi cha asilimia 30 hadi 40 kwa kina mama wajawazito hao kuwaambukiza virusi vya Ukimwi watoto watakao wazaa. Je, kina mama wajawazito wenye virusi vya Ukimwi wanaweza kujifungua watoto wenye afya nzuri? Je kina Mama hao wanaweza kuepusha vipi kuwaambukiza watoto wao virusi vya Ukimwi kabla hawajazaliwa na baada ya kuzaliwa? Mwandishi wetu wa habari alitembelea Hospitali ya Kenyatta, jijini Nairobi, na kumhoji Daktari Kizito Lubano, ambaye anashughulikia mambo ya uzazi, na kuwasaidia akina mama waja wazito wenye virusi vya Ukimwi wasiwaambukize watoto watakao wazaa.

Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu huku wakiumia kisirisiri, sasa kina mama waja-wazito ambao wana virusi vya Ukimwi, wanaweza kufurahia hali zao za kiafya kwa kujifungua salama bila kuwaambukiza virusi vya Ukimwi watoto wao.Hayo yanatokana na juhudi za utafiti zilizofanywa na madaktari duniani.

Takwimu kutoka wizara ya Afya nchini Kenya, zinaonesha kuwa kati ya idadi ya watu milioni 34 nchini humo, kina kuna kina mama milioni 1.6 wanaokuwa wajawazito. Na kati ya hao wanawake laki 1.5 wameambukizwa virusi vya Ukimwi, nao watoto wapatao elfu 60 huzaliwa kila mwaka wakiwa wameambukizwa virusi vya Ukimwi. Wengi wa kina mama hao waja-wazito huwaambukiza watoto hao wakati wa kujifungua au wakati wa kuwanyonyesha. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka jana pekee, karibu watoto laki saba walio chini ya umri wa miaka 15 waliambukizwa virusi vya Ukimwi duniani. Kati ya idadi hiyo, asilimia 90 kati yao wako barani Afrika.

Lakini hivi sasa serikali ya Kenya inafanya juhudi za kukabiliana na ongezeko la watoto wanaozaliwa wakiwa wameambukizwa virusi vya Ukimwi na mama zao. Vituo vya afya kama elfu 1 vimefunguliwa kote nchini Kenya ili kuwapa kina mama wajawazito ushauri na dawa mpya za kuwa kinga dhidi ya maambukizi ya Ukimwi.

Radio China Kimataifa ilitembelea hospitali Kenyatta nchini Kenya, na kuzungumza na daktari wa maradhi ya kina mama Bw Kizito Lubano, ambaye alidokeza kuwa wizara ya afya ya Kenya sasa inakabiliana na tatizo hilo sugu kwa kutumia dawa mpya za Nevirapine, Ziduvodine, Lamividine, Septrine na Multi-vitamin. Alisema 'Dawa nyingine kama multi-vitamin, lamividine, septrine zinamkinga mama mja-mzito dhidi ya magonjwa yanayomkumba mgonjwa wa virusi vya Ukimwi. Kina mama hao pia wanapewa dawa nyingine zinazoweza kuwakinga dhidi ya maradhi ya ngozi, kifua kikuu.'

Hata hivyo Dr. Lubano amedokeza kuwa hata kina mama wenye virusi vya Ukimwi, wanaweza kuwanyonyesha watoto wao kwa muda wa miezi sita bila kuwapa watoto vyakula vingine vyovyote.

Inapotimia miezi sita, basi kina mama hao wanapaswa kuacha kuwanyonyesha watoto wao na badala yake kutumia maziwa mengine pamoja na vyakula vinginevyo maalum vya watoto wachanga.

Ili kampeni ya kukabiliana na janga hilo iweze kufaulu, wanaharakati wa kupambana na maradhi ya Ukimwi wamewataka hata wazazi wa kiume wajihusishe, na sio kudhani tu kuwa ni kina mama pekee wanaoathirika.

Dawa hizo za kukabiliana na maambukizi hayo ya Ukimwi zapatikana katika vituo vya afya bila malipo. Kwa mujibu wa Dr. Lubano ni kuwa wamewaweka wahudumu maalumu katika vituo vya afya. Wajibu mkubwa wa wahudumu hao ni kutoa ushauri kwa kina mama na watu wengine wenye virusi vya Ukimwi.