Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-03 16:52:46    
China yajenga maktaba ya kutoa huduma kwa wakulima wapatao milioni 900

cri

Bw. Huo Chengxi ni mkulima wa kijiji cha Zhuzhuiling mkoani Gansu, magharibi kaskazini mwa China. Hivi sasa akipata muda anakwenda "maktaba ya wakulima" ambayo ujenzi wake ulikamilika hivi karibuni katika kijiji chake. Sasa maktaba hiyo ndogo yenye eneo la mita 80 za mraba inawavutia sana wakulima wa kijiji hicho, ambao wanapumzika, kupiga gumzo, kusoma na kujifunza elimu ya kilimo kwenye maktaba hiyo.

Nchini China serikali inatekeleza mradi unaoitwa "maktaba ya wakulima" unaolenga kuondoa matatizo ya wakulima yanayohusu kusoma, kuazima na kununua vitabu. Kwa mujibu wa mradi huo, katika muda wa miaka mitano, maktaba laki 2 za wakulima zitajengwa katika vijiji vyenye wakazi wengi.

Hivi sasa nchini China wakulima wanakabiliwa na matatizo katika kusoma vitabu. Kwa upande mmoja bei za vitabu ni kubwa, kiasi ambacho kimezidi uwezo wa wakulima wengi, na kwa upande mwingine hakuna maktaba kwenye maeneo ya vijijini, hali ambayo inawafanya wakulima washindwe kuazima vitabu.

Kutokana na uwezo mdogo wa wakulima, vitabu vichache vinavyohusu wakulima, vijiji na kilimo vinapatikana kwenye soko la vitabu la China. Mkuu wa Mamlaka ya habari na uchapishaji ya China Bw. Long Xinmin alieleza kuwa, mwaka 2005 miongnoni mwa vitabu aina zaidi ya laki 2 vilivyochapishwa nchini China, aina ya vitabu vinavyohusu kilimo, wakulima na vijiji vilikuwa 3,800 tu.

Katika juhudi za kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo, kuanzia mwaka huu China ilianza kutekeleza mradi wa "maktaba ya wakulima". Ujenzi wa maktaba hiyo unagharamiwa na serikali, na wakulima wenyewe watabeba jukumu la kusimamia maktaba hiyo. Kila maktaba inapaswa kuhifadhi vitabu visivyopungua elfu moja, majarida yasiyopungua aina 30, na aina 100 za rekodi za sauti na picha za video.

Mkoa wa Gansu ni moja kati ya mikoa iliyotangulia kutekeleza mradi huo, hivi sasa maktaba za wakulima karibu 300 tayari zimeanzishwa mkoani humo. Mkulima wa kijiji cha Zhuzuiling Bw. Huo Chengxi alimwambia mwandishi wa habari kuwa, wakulima wenzake wengi wanajishughulisha na kilimo cha mboga na maua, wana hamu ya kujifunza teknolojia. Lakini hapo awali hakukuwa na maktaba, iliwabidi wakulima wajifunze kutoka kwenye vipindi vya mafunzo vya televisheni, hali ambayo iliwapa taabu. Mwanzoni mwa mwaka huu maktaba ya wakulima ilianzishwa, wakulima wanaweza kuyatumia wakati wa mapumziko wa mchana na jioni, ambapo wanasoma vitabu na kutazama video, wakijifunza ujuzi wa kilimo.

Maktaba hiyo ya wakulima ilipoanzishwa, ilikuwa na vitabu zaidi ya elfu 5 na diski 300. Baadhi ya vitabu na diski hizo zinahusu elimu ya kilimo inayowasaidia wakulima waondokane na umaskini kama vile ujuzi wa kilimo, ufugaji na utengenezaji wa mazao ya kilimo. Vitabu na diski nyingine ni kuhusu utamaduni, afya na sheria, pia kuna vitabu na diski zinazowahudumia watoto. Msimamizi wa maktaba hiyo alichaguliwa na wakulima wenyewe.

Bibi Jin Hongfang wa kijiji kingine mkoani Gansu alisema, "Hivi sasa wakulima wanaweza kusoma vitabu kwenye maktaba hiyo na kuviazima, na katika siku zijazo wataweza kununua vitabu kwenye maktaba hiyo." Mama huyo alitoa mchango wa chumba kimoja kikubwa cha nyumba yake ili kiwe maktaba ya wakulima, yeye mwenyewe alichaguliwa na wenzake kuwa msimamizi wa maktaba hiyo. Alisema "Wakulima hususan vijana wanafurahia sana maktaba ya wakulima. Mpaka sasa wanavijiji zaidi ya 300 walisoma vitabu kwenye maktaba hiyo, ambapo watoto wengi wanaitumia mara kwa mara katika likizo ya siku za joto."

Idhaa ya kiswahili 2006-08-03