Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-04 16:13:20    
TAZARA-Reli ya Urafiki kati ya watu wa China na Tanzania

cri

Reli ya TAZARA imechangia sana kukuza uhusiano wa kirafiki kati ya China na Tanzania. Tanzania ina Reli mbili ambazo zilijengwa katika vipindi tofauti, ujenzi wa reli hizo ambao uliwashirikisha watu wengi wa China sasa zimekuwa njia muhimu za usafirishaji wa abiria na shehena nchini humo. Lakini hali ya ujenzi wa reli hizo mbili ni tofauti.

Mwishoni mwa Karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20, vibarua mia kadhaa wa China walilazimishwa na wakoloni wa Ujerumani kushiriki kwenye ujenzi wa reli iliyoanzia Dar es Salaam hadi Moshi, baadhi yao walipoteza maisha yao. Wazee wa Tanzania wanaoishi katika kijiji walichoishi vibarua hao chini ya safu za milima ya Usambara bado wanaweza kuwakumbuka.

Katika miaka ya 60 hadi 70 ya karne iliyopita, baada ya Tanzania na Zambia kujipatia uhuru kutoka kwa utawala wa kikoloni?mafundi na wahandisi elfu kumi kadhaa wa China waliitikia mwito wa serikali ya China kwenda barani Afrika kusaidia ujenzi wa reli kati ya Tanzania na Zambia, baadhi yao walipoteza maisha yao nchini humo.

TAZARA ni ufupisho wa reli ya Tanzania na Zambia, neno hilo limekuwa ni alama ya urafiki wa dhati kati ya nchi tatu China, Tanzania na Zambia uliojengwa kwa damu na maisha.

Reli ya TAZARA ni mradi mkubwa kabisa uliojengwa kwa msaada wa serikali ya China katika nchi za nje. Inaanzia Dar es Salaam, mji maarufu wa Tanzania, na kuishia Kapri Mposhi, mkoa wa katikati wa Zambia, urefu wake ni kilomita 1860. Kazi zote za ukaguzi na usanifu wa reli hiyo zilifanywa na wahandisi na wataalamu wa China.

Zifuatazo ni baadhi ya tarehe muhimu katika ujenzi wa reli ya TAZARA. Tarehe 15 Mei mwaka 1968, upimaji wa reli hiyo ulianza kufanywa nchini Tanzania. Tarehe 26 Oktoba mwaka 1970, ujenzi wa reli hiyo ulianza nchini Tanzania. Tarehe 22 Oktoba mwaka 1975, reli ya TAZARA ilizinduliwa kwa majaribio. Tarehe 23 Julai mwaka 1976, reli ya TAZARA ilianza kufanya kazi rasmi.

Katika mchakato wa ujenzi wa reli ya TAZARA, serikali ya China kwa jumla iliwatuma wataalamu, wahandisi na wafanyakazi elfu 50 kushiriki kwenye ujenzi huo, na miongoni mwao, wachina 65 walijitolea mihanga nchini Tanzania na Zambia. Watu hao walizikwa kwenye makaburi ya wataalamu wa China yaliyoko umbali wa kilomita 24 kusini magharibi mwa Dar es Salaam, kando ya reli ya TAZARA. Mkuu wa kikundi cha wataalamu na wahandisi cha China Bwana Du Jing alifahamisha kuwa, miongoni mwa watu hao, asilimia 30 walikufa kazini, asilimia 40 walikufa katika ajali na asilimia 30 wengine walifariki dunia kutokana na magonjwa ya maambukizi kama vile malaria na kipindupindu.

Waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alipofanya ziara nchini Tanzania mwezi Juni mwaka huu alikwenda sehemu yenye makaburi ya wachina kuweka shada la maua kwa heshima.

Baada ya reli ya TAZARA kukamilika, serikali ya China inaendelea kutekeleza makubaliano ya ushirikiano wa kiufundi, na kutuma kikundi kimoja baada ya kingine cha wataalamu na wahandisi kusaidia utunzaji wa reli hiyo ili kuhakikisha reli hiyo inafanya kazi vizuri, na katika muda huo wachina watano wengine walijitolea mihanga kazini. Baadhi ya Wachina wamefanya kazi kwenye reli ya TAZARA kwa miaka 18 hadi walipostaafu.

Ujenzi wa Reli ya TAZARA umebadilisha mtindo wa maisha ya wakazi waishio kando ya reli hiyo.

Hadi leo reli ya TAZARA kwa jumla imesafirisha abiria zaidi ya milioni 39, na shehena zaidi ya tani milioni 24, reli ya TAZARA imekuwa njia muhimu ya usafirishaji kwenye sehemu ya kusini mashariki mwa Afrika.

Ujenzi wa reli hiyo si kama tu umeongeza thamani ya mazao ya kilimo yaliyozalishwa katika sehemu zilizoko kando ya reli hiyo, bali pia umewawezesha wakazi waishio kando ya reli kwenda kwa urahisi sehemu nyingine kupata ajira. Reli ya TAZARA imefikisha mbegu bora, mbolea, dawa za kuua wadudu na vifaa vya kumwagilia mashambani kwa wakulima waishio kando ya reli hiyo, na pia imesaidia kupeleka dawa na matibabu kwa wakazi wa sehemu zilizo kando ya reli hiyo.

Mtaalamu wa historia wa Marekani mwenye asili ya Afrika Bwana Jamy Monson aliwahi kusema, reli ya TAZARA iliyojengwa kwa msaada wa China itaonesha umuhimu wake halisi katika mchakato wa kupunguza umaskini kwa nchi za Afrika Mashariki. Ujenzi wa reli hiyo umesifiwa sana na viongozi wa Tanzania na Zambia. Rais wa zamani wa Tanzania Mwalimu Nyerere aliwahi kusema:

"Ujenzi wa reli ya TAZARA ni mchango mkubwa uliotolewa na serikali ya China kwa watu wa Afrika. Tukiangalia historia, watu wa nchi nyingine walijenga reli barani Afrika kwa ajili ya kunyang'anya mali zetu, lakini Wachina wametusaidia ili kustawisha uchumi wetu."

Na rais wa kwanza wa Zambia Dkt. Keneth Kaunda alisema:

"Akufaaye wakati wa dhiki ndiye rafiki. Wakati tulipokumbwa na matatizo ya kiuchumi, ni watu wa China waliotuunga mkono."

Watu wa Tanzania na Zambia na watu wa Afrika nzima wanaisifu TAZARA kuwa ni reli ya uhuru, ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya kusini na kusini.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-04