Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-04 18:40:58    
Jumuiya ya nchi za kiislamu yalaani vitendo vya uvamizi vya Israel

cri

Nchi kadhaa wanachama wa Jumuiya ya nchi za kiislamu tarehe 3 mwezi huu zilifanya mkutano wa dharura huko Putrajaya, Malaysia, baadaye zilitoa taarifa zikilaani vikali vitendo vya uvamizi vya Israel.

Marais, viongozi wa serikali, mawaziri wa mambo ya nje au wawakilishi wao kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za kiislamu Malaysia, Indonesia, Iran, Palestina, Lebanon na Syria walihudhuria mkutano huo wa siku moja.

Mkutano huo ulitoa taarifa kuhusu hali ya Lebanon ikisema, vitendo vya Israel vya kuishambulia Lebanon vimekiuka vibaya ukamilifu wa ardhi na mamlaka ya nchi ya Lebanon. Taarifa hiyo inasema Israel inapaswa kubeba lawama zote juu ya matokeo ya vitendo vyake vya uvamizi. Washiriki wa mkutano huo pia wametaka uchunguzi wa kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita wa Israel nchini Lebanon ufanyike.

Taarifa hiyo inalihimiza Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litekeleze jukumu lake la kulinda amani na utulivu duniani, na kuchukua hatua za kutimiza mara moja na kwa pande zote usimamishaji vita kati ya Lebanon na Israel. Taarifa hiyo inapendekeza kuwekwa kwa jeshi la kulinda amani la nchi nyingi ambalo litakabidhiwa madaraka na Umoja wa Mataifa na nchi za kiislamu zinaweza kujiunga na jeshi hilo. Nchi za Malaysia, Indonesia na Brunei zimekubali kutuma askari wao kushiriki kwenye harakati za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

Aidha watu waliohudhuria mkutano huo wameeleza kuunga mkono mapendekezo 7 yaliyotolewa hivi karibuni na serikali ya Lebanon kuhusu kusimamisha vita mara moja na kwa pande zote kati ya Lebanon na Israel. Mapendekezo hayo yanahusu Lebanon na Israel kubadilishana mateka wa kivita na wafungwa, na jeshi la Israel lirudi kwenye "mstari wa buluu" yaani mpaka wa muda kati ya pande hizo mbili.

Waziri wa mambo ya nje wa Lebanon Bwana Fawzi Salloukh aliyehudhuria mkutano huo alisema, Lebanon italinda mamlaka ya ardhi yake chini ya uungaji mkono wa jumuiya ya kimataifa. Aidha ameitaka Kamati ya sheria ya kimataifa ifanye uchunguzi juu ya uhalifu wa jeshi la Israel wa kushambulia sehemu ya kusini mwa Lebanon na kusababisha vifo vya raia, na kuwawezesha wakimbizi wa Lebanon warudi nyumbani kwao mapema iwezekanavyo. Baada ya mkutano huo kumalizika, Bwana Salloukh aliwaambia waandishi wa habari kuwa, taarifa iliyotolewa na mkutano huo wa dharura wa Jumuiya ya nchi za kiislamu imetoa "sauti kubwa yenye nguvu" kwa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Katibu mkuu wa Jumuiya ya nchi za kiislamu Bwana Ekmeleddin Ihsanoglu amelaani nchi fulani kutekeleza "vigezo viwili" juu ya mgogoro kati ya Lebanon na Israel. Waziri mkuu wa Bangladesh Bibi Khaleda Zia alieleza wasiwasi wake kuhusu mgogoro kati ya Israel na Lebanon ambao huenda utaifanya dunia ya kiislamu iwe na siasa kali zaidi.

Rais Mahmoud Ahmedinejad ametoa mwito wa kuzitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za kiislamu ziungane, alisema Marekani na Uingereza ziliishawishi Israel iishambulie Lebanon, hivyo zinapaswa kulipia fidia kwa hasara za Lebanon.

Waziri mkuu wa Malaysia ambayo ni nchi mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya kiislamu Bwana Abdullah Ahmad Badawi tarehe 3 mwezi huu aliwaambia waandishi wa habari kuwa, tarehe 4 Agosti atamwandikia barua rais Bush wa Marekani kuitaka Marekani itumie nguvu yake ya ushawishi kuhimiza Lebanon na Israel zitimize usimamishaji vita mara moja. Amedhihirisha kuwa, mbali na Marekani na Uingereza, nchi nyingine zilizo za wajumbe wa kudumu wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan wote wamekubali kuzitaka Lebanon na Israel zisimamishe vita mara moja. Lakini kutokana na msimamo wa Marekani na Uingereza, Israel inashambulia Lebanon bila hofu yoyote. Bwana Badawi alisema, hili ni jambo linalosikitisha sana.

Mkutano huo wa dharura uliitishwa na Malaysia ambayo ni nchi mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya nchi za kiislamu.