Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-07 15:42:17    
Xidi na Hongcun

cri
Mlima Huangshan wa China unajulikana nchini na duniani, hivyo kila mwaka watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali nchini China na nchi za nje huenda huko kutalii. Lakini kama tukizungumzia vijiji viwili Xidi na Hongcun vilivyoko chini ya Mlima Huangshan, labda watu wengi hata wa nchini China hawaelewi hali ya vijiji hivyo viwili vya makazi ya kale. Katika vijiji hivyo viwili, kuna makazi yaliyobaki kikamilifu, vijiji hivyo viwili vikiwa vinawakilisha makazi ya kale mkoani Anhui, China vimeorodheshwa kuwa mali za urithi duniani miaka 6 iliyopita.

Vijiji vya Xidi na Hongcun vyote viko katika sehemu iliyo karibu na Wilaya Yi, ambapo ukipanda gari kutoka Mlima Huangshan utafika kwenye vijiji hivyo baada ya saa moja tu. Na Kijiji cha Xidi kiko umbali wa kilomita 8 tu kutoka mji wa Wilaya Yi. Kijiji hiki kina urefu wa mita 700 toka mashariki hadi magharibi, na upana wa kutoka kusini hadi kaskazini ni mita 300. Kwenye kando ya Kijiji cha Xidi kuna mto mmoja unaotiririka kutoka mashariki hadi magharibi, kijiji hiki kilikuwa kituo cha kupeleka barua katika zama za kale, hivyo kilipewa jina la Xidi, Xi, maana yake ya kichina ni magharibi, Di, maana yake ya kichina ni kupeleka. Katika Kijiji cha Xidi kuna nyumba zaidi ya 200 zilizojengwa katika Enzi za Ming na Qing ambazo zinabaki kikamilifu, na nyumba kadhaa miongoni mwao zimekuwa na historia ya miaka 600.

Fremu za milango ya nyumba nyingi za kale za wakazi wa Kijiji cha Xidi zilijengwa kwa marmar za rangi nyeusi, na madirisha ya mbao ya nyumba hizo ni ya wazi yenye michongo ya kisanii. Vijito viwili vyenye maji safi vinapita kwenye Kijiji cha Xidi, nyuma ya makazi zinazoegemeana za kijijini humo zinapatana na mandhari ya mto na milima, watalii wakiingia kijijini watajihisi kama wameingia kwenye sehemu yenye mandhari nzuri mithili ya ile iliyochorwa kwenye picha.

Mwongozaji wa Shirika la utalii wa kimataifa la China Bi. Gao Liwen alijulisha kuwa, katika Kijiji cha Xidi kuna vichochoro 99, nyumba zaidi ya 200 za makazi ya kale zenye ukuta mrefu zimetapakaa ndani ya vichochoro hivyo, watalii wakifika kwenye kijiji hicho kwa mara ya kwanza, wanaweza kujihisi kama wanaweza kupotea njia kila wakati. Alisema:

Katika Kijiji cha Xidi kuna nyumba nyingi za makazi ya kale, lakini hivi sasa nyumba hizo za makazi kati ya 12 na 13 zilizobaki kikamilifu zimefunguliwa kwa watalii, watalii wanaweza kutembelea nyumba hizo za makazi. Nyumba hizo ni safi, ndani ya nyumba hizo safi, samani na vyombo hata mapambo ya michoro na maandiko ya kichina vyote vinaonesha hali asilia ya mitindo ya Enzi za Ming na Qing, samani nyingi ni zile zilizotengenezwa katika enzi hizo mbili.

Kwenye kumbukumbu za historia imeandikwa kuwa, wakati wa karne ya 7, mtoto mmoja wa mfalme wa China alitorokea kwenye sehemu hiyo kutokana vurugu za vita, akabadilisha jina lake na kuishi katika sehemu hiyo. Baadaye watu wengi waliohamia sehemu hiyo waliongezeka siku hadi siku, sehemu hiyo ikawa kijiji. Baada ya karne ya 14, wasomi kadhaa wa kijiji hicho walianza kujishughulisha na biashara, wakawa matajiri, wakajenga nyumba, mahekalu, njia na madaraja, kijiji hicho kikajengwa kuwa cha kifahari sana.

Mtaalamu wa elimu ya ujenzi wa China Bwana Yang Hongxun anaona kuwa, mtindo pekee wa nyumba za makazi ya kale katika kijiji cha Xidi ni mapambo ya michongo ya matofali, mawe na mbao. Alisema:

Nyumba za makazi ya Kijiji cha Xidi zinatofautiana na zile za sehemu nyingine kwa idadi yake kubwa, ambapo nyumba nyingi za makazi ya kale ziko katika kijiji hicho; tena michongo ya matofali, mawe na mbao ni yenye kiwango cha juu, na mapambo hayo yanayopendeza yanaonekana wazi.

Na sasa tunapenda kuwaelezea hali kuhusu Kijiji cha Hongcun. Kijiji cha Hongcun kina eneo la hekta 19, ambacho kiko kwenye sehemu yenye umbali wa kilomita 11 kutoka mji wa Wilaya Yi. Kijiji cha Hongcun kina historia ndefu zaidi kuliko ile ya Kijiji cha Xidi. Hapo awali watu walipenda kujenga nyumba zao kwa kuegemea kijiji kimoja mbele ya mlima. Baadaye idadi ya watu iliongezeka siku hadi siku, nyumba za makazi zilizojengwa kwenye ardhi nyembamba na ndefu kando ya kijito ziliongezeka zaidi siku hadi siku, kiasi ambacho mara familia moja ikikumbwa na maafa ya kuungua, majirani zake hakika wanaweza kuathiriwa, hata kijiji kizima kinaweza kukumbwa na balaa. Ili kuepusha maafa ya moto, wakazi wa Kijiji cha Hongcun waliamua kuyafanya maji ya kijiji yapite kwenye kila nyumba kijijini hapo.

Wakazi wa kijiji hicho walijenga mfereji na kuingiza maji ya kijito kilichoko mbele ya mlima hadi mbele ya kila nyumba ya kijiji hicho, wakazi walitumia mpangilio asilia wa kijiografia, kuyafanya maji yaliyoko kwenye mfereji yatiririke siku zote, na kuweka mlango wa mfereji kwenye sehemu ya juu, ili kudhibiti wingi wa maji yanayotiririka, na kuyawezesha maji yarudi tena kwenye sehemu ya chini ya kijito.

Mtaalamu wa ujenzi wa China Bwana Yang Hongxun alisema, usanifu huo wa mfumo wa maji wenye mtindo maalum katika Kijiji cha Hongcun si kama tu unasifiwa sana na wataalamu wa ujenzi wa China, bali pia unafuatiliwa na wataalamu wa Japan, Marekani na Ujerumani. Usanifu huo wa mfumo wa maji unastahiki kusifiwa kuwa ni mwujiza katika usanii wa ujenzi wa kijiji cha China katika zama za kale. Alisema:

Kijiji cha Hongcun kilitumia vizuri mazingira na hali ya kijiografia ya kijiji hicho. Wachina wanaheshimu sana dunia ya maumbile tangu enzi na dahari, na wanatumia hali ya maumbile kwa kufuata hali halisi, nyuma ya nyumba zao inaegemea mlima, na mbele inakabiliana na kijito, lakini walipata njia rahisi ya kupata maji na kumwagilia maji mashambani kwa njia rahisi ambayo inastaajabisha watu.

Katika Kijiji cha Hongcun kuna nyumba za makazi zaidi ya 300 zilizojengwa katika enzi za Ming na Qing, miongoni mwake Jumba la Chengzhitang linajulikana zaidi. Jumba hilo lilikuwa makazi ya mfanyabiashara mkubwa wa chumvi aitwaye Wang Dinggui. Jumba lenyewe lilijengwa kwa mbao, ndani ya jumba kuna michongo mingi ya matofali, mawe na mbao, michongo hiyo ililipamba jumba hilo kuwa jumba lenye fahari kubwa. Inasemekana kuwa, michongo iliyo ndani ya jumba hilo ilifanywa na wafanyakazi 20 kwa miaka minne.

Mtalii wa Beijing aliyewahi kutembelea Jumba la Chengzhitang alisema:

Ndani ya jumba hilo michongo yote kama vile ya binadamu iliyochongwa kwenye mbao, au maua na ndege iliyochongwa kwenye vioo au juu ya ukuta wa matofali yote inaonekana kama ina uhai. Nakumbuka sana michongo ya wavulana 100 iliyochongwa kwenye mlango mmoja wa mbao, wavulana hao 100, baadhi yao walicheza ngoma, wengine wanapiga pato, kurusha fataki na fashifashi, wengine wanapiga tarumbeta na kutembea kwa mironjo, sura zao za aina mbalimbali zinapendeza sana.

Bwana Li Jin anaona kuwa katika vijiji vya Xidi na Hongcun, mipangilio mizuri ya kupendeza na nyumba za makazi ya kale zilizojengwa kwa mitindo pekee, vyote hivyo vinaonekana kuwa na umaalum wa vijiji viwili hivyo vidogo, mandhari ya maumbile ya huko iliyo ya utulivu inawavutia sana watu.

Mtaalamu wa ujenzi wa China Bwana Yang Hongxun alisema, mandhari nzuri ya vijiji hivyo viwili inaweza kuwavutia watalii wengi zaidi kutoka nchini na nje. Alisema:

Kijiji cha Xidi na Kijiji cha Hongcun vimeonesha utamaduni wa jadi wa aina mbalimbali kote duniani, vijiji hivyo viwili vimeonesha hali ya historia ya Enzi za Ming na Qing. Watalii wa nchini na kutoka nje wakitembelea huko wanaweza kuona sanaa nzuri za China zinazohifadhiwa vizuri ambazo zina thamani kubwa.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-07