Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa usiku wa tarehe 5 mwezi huu walifanya mjadala wa kwanza kuhusu mswada wa azimio linalohusu mgogoro kati ya Lebanon na Israel. Israel na nchi kadhaa za magharibi zimeeleza kuufurahia mswada huo, lakini Lebanon na baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati na mashirika ya kanda hiyo zimeeleza kuupinga.
Mswada huo uliotolewa na Marekani na Ufaransa unazitaka pande zinazopambana ziache kabisa vitendo vya uadui, ukisisitiza kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo kutoka kwenye chanzo chake, ikiwa ni pamoja na kuwaachia huru wanajeshi wa Israel bila masharti. Mswada huo unahimiza juhudi za kutatua suala la Walebanon wanaoshikiliwa na Israel, pia umeweka masharti kadhaa katika kufanikisha usimamishaji vita wa kudumu na kupatikana kwa ufumbuzi wa kisiasa wa muda mrefu wa tatizo hilo.
Baada ya mjadala wa tarehe 5 Agosti, balozi wa Ghana ambayo ni nchi mwenyekiti wa zamu wa baraza hilo kwa mwezi Agosti katika Umoja wa Mataifa Bw Effah-Apenteng, alisema kwa ujumla mabalozi wa nchi mbalimbali wameeleza kufurahia kutolewa kwa mswada huo, ambao wanaona unapaswa kuchukua hatua kwa haraka ili kumaliza mapambano. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Li Zhaoxing tarehe 6 mwezi huu alipozungumza na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan kwa njia ya simu alisema, baraza la usalama linapaswa kuchukua hatua kwa haraka iwezekanavyo na kuzuia kuongezeka kwa mapambano. Habari zinasema kuwa baraza la usalama litakuwa na mjadala mwingine kuhusu mswada huo, na kuupigia kura katika siku kadhaa zijazo.
Marekani na Ufaransa zinataka mswada huo zilizoutoa upitishwe na baraza la usalama. Uingereza na Ujerumani pia zimeeleza bayana msimamo wa kuunga mkono mswada huo. Israel haijatoa jibu rasmi kuhusu mswada huo, lakini waziri wa sheria wa nchi hiyo Bw. Haim Ramon tarehe 6 Agosti alipohojiwa alisema, mswada huo unaisaidia Israel, hata hivyo Israel bado haijatimiza lengo lake la kijeshi kwa hiyo itaendelea na mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa kundi la Hezbollah la Lebanon. Kwa upande wa Lebanon, imeukataa katakata mswada huo. Tarehe 6 mwezi huu Lebanon ilitoa ombi rasmi kwa baraza la usalama, ikitaka mswada huo urekebishwe, na kuongezwa maneno kuhusu kuitaka Israel iondoe jeshi lake nchini Lebanon.
Katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu Bw Amr Moussa ameukosoa mswada huo kwa kutaka tu kumaliza kwa vitendo vya uadui na hautoi mwito wa kusimamisha vita mara moja. Bw. Moussa ameliomba baraza la usalama liweke bayana msimamo wake kuhusu vitendo vya kijeshi vya Israel. Katibu mkuu wa Baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba Bw. Abdul Rahman al-Attiya tarehe 6 mwezi Agosti alitoa taarifa, akisema azimio litakalopitishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lazima lihusishe usimamishaji wa vita mara moja na kulitaka jeshi la Israel liondoke kabisa kutoka ardhi ya Lebanon inayoikalia na kurudi nje ya mstari wa kibluu. Bw. Al-Attiya alisisitiza kuwa, mswada wa azimio uliotolewa na Marekani na Ufaransa haulingani na maslahi ya watu wa Lebanon, wala hauwezi kutatua tatizo la sasa. Iwapo mswada huo utapitishwa na baraza la usalama, basi hali itazidi kuwa mbaya.
Waziri wa mambo ya nje wa Syria Bw. Walid Mualem alisema mswada wa Marekani na Ufaransa unamaanisha kukubali vita vinavyoendelea, jambo ambalo si haki kwa Lebanon. Na Iran imesema azimio lolote kuhusu Lebanon litakalopitishwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kuwa la haki.
Wachambuzi wanaona mswada huo kushindwa kuzingatia ufuatiliaji wa Lebanon ni chanzo cha kusababisha kuwepo kwa malalamiko kutoka pande husika. Kutokana na maoni tofauti ya pande mbalimbali, watu wana mashaka kama mswada huo unaweza kupitishwa na baraza la usalama au la, na hata kama ukipitishwa na kuwa azimio, kuna mashaka kama azimio hilo litatekelezwa kabisa.
Idhaa ya Kiswahili 2006-08-07
|