Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-08 10:30:29    
Teknolojia ya mawasiliano ya habari yachangia maendeleo ya sehemu ya vijiji nchini China

cri

Zaidi ya watu milioni 800 kati ya jumla ya watu bilioni 1.3 wa China wanaishi katika sehemu za vijijini, hivyo kuendeleza kilimo na kuinua kiwango cha maisha ya wakulima kunachukuliwa kuwa ni mkazo unaowekwa katika kazi za serikali. Katika miaka ya hivi karibuni, teknolojia ya mawasiliano ya habari imeendelezwa na kutumika katika sekta mbalimbali, ambayo inachangia maendeleo ya sehemu za vijijini. Habari kutoka vijiji vilivyoko kwenye sehemu za pembezoni mwa Beijing zinasema, hivi sasa kampuni na viwanda vingi vinajitahidi kupeleka teknolojia na zana mpya huko na kuwasaidia wakulima kupata maendeleo makubwa zaidi.

Mwishoni mwa mwaka jana, Beijing ilizindua mradi wa ujenzi wa vituo vya mawasiliano ya habari ili kuinua kiwango cha mawasiliano ya habari ya sehemu hizo. Mradi huo umenuia kujenga vituo kiasi cha 300 vya mawasiliano ya habari, kutoa huduma za mawasiliano ya habari na kuwarahisishia maisha wakazi wa sehemu za vijijini. Mkazi wa kijiji cha Shangzhen, wilaya ya Pinggu, Beijing, bibi Liu Guiying alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi sasa wanakijiji wanaweza kupata habari nyingi kuhusu uzalishaji mali na shughuli za biashara kwenye Internet,

"Katika upande wa uzalishaji mali, kwa mfano mkulima anataka kuuza matunda ya pichi, habari moja nzuri inaweza kuleta manufaa kwake. Vituo vya utoaji huduma wa habari vinaweza kutoa habari za masoko kwa wakulima, ambazo zingeleta faida kwa wakulima. Pengine mkulima anataka kununua mashine ya kusindika mazao ya kilimo, basi anaweza kutafuta mashine ya aina hiyo kwenye tovuti. Mfano mwingine ni kwamba mkulima mmoja wa eneo letu aliweza kununua mashine ya kukaanga walnut baada ya kupata habari husika kwenye tovuti ya kituo cha utoaji huduma ya habari."

Bibi Liu Guiying alisema, hivi sasa wakazi wa kijiji chao wanaweza kulipia simu, umeme na baadhi ya malipo mengine ya maishani mwao kwa kupitia vituo vya huduma ya mawasiliano ya habari. Na vituo hivyo vya huduma za habari vinatoa mafunzo ya kazi ya aina mbalimbali, kuweka baadhi ya software za masomo katika kompyuta za wakulima kwa ajili ya manufaa yao, hatua ambayo imehimiza maendeleo ya uchumi ya huko.

Kampuni ya huduma za mawasiliano ya habari ya Hengxintong ni kampuni iliyokabidhiwa jukumu la kujenga vituo vya utoaji huduma za mawasiliano ya habari kwenye sehemu za vijijini za Beijing, hivi sasa kampuni hiyo imejenga vituo 36 kwenye sehemu hiyo, ambapo wakulima wanaweza kusaidiwa na wafanyakazi wa vituo hivyo kutafuta habari wanazohitaji. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Fu Bin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi sasa pato la wakulima limeongezeka zaidi baada ya kuanza kutumia vituo hivyo vya huduma za habari, kwani baada ya kupata habari husika wanaweza kuuza mazao yao ya kilimo moja kwa moja.

"Tunawasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa kuwapa habari kuhusu masoko. Hapo awali mazao ya wakulima yaliuzwa kwa kupitia mawakala wa ngazi mbalimbali. Hivi sasa tunawapa wakulima mfumo wa kuuza mazao yao moja kwa moja kwa kutumia vituo vyetu vya huduma za habari."

Kwa kuweko soko kubwa la Beijing, viwanda vidogo vidogo vya sehemu za vijijini vilivyoko pembezoni mwa mji wa Beijing, vimekuwa na mazingira bora ya maendeleo. Katika miaka ya hivi karibuni, viwanda hivyo vinazingatia umuhimu wa bidhaa bora. Hivyo baadhi ya kampuni za software zimetengeneza mfumo wa kutambua sifa za bidhaa kwa ajili ya viwanda vya sehemu za vijijini, ambao wanunuzi na wasimamiaji wa ubora wa bidhaa wanaweza kufahamu kwa urahisi habari kuhusu wazalishaji wa bidhaa, hatua hiyo licha ya kuweza kuondoa wasiwasi wa wanunuzi, jambo lililo muhimu zaidi inalinda sifa za bidhaa za viwanda bora. Meneja wa kampuni ya teknolojia ya chakula ya Zhongshi ya Beijing bibi Wei Wei alisema,

"Ninachukua mfano wa nguruwe, nguruwe anawekwa alama kwenye sikio lake wakati anapozaliwa, hivyo habari zote kuhusu ukuaji wake, magonjwa aliyoyapata, hali ya uchinjaji na usindikaji zinahifadhiwa kwenye kompyuta."

Licha ya kutoa habari wanazohitaji wakulima, baadhi ya kampuni za teknolojia zinapanua matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya habari ya sehemu za vijijini hadi kwenye bidhaa zenye nyongeza kubwa ya thamani. Kampuni ya Hengxintong sasa imekuwa na ushirikiano na sehemu za vijijini za Beijing kuhusu shughuli za utalii wa mila na jadi za wenyeji. Kampuni hizo zinawafahamisha wakazi wa mji wa Beijing habari kuhusu utalii wa mila na desturi za jadi za wakulima wa sehemu za vijiji za Beijing kwa njia ya kuweka habari hizo kwenye tovuti, na kutuma ujumbe katika simu za mkononi, ili kuwavutia kushiriki matembezi na mapumziko kwenye sehemu za vijijini, na kuongeza pato la wakulima. Meneja wa idara ya shughuli za kampuni Bw. Wang Fenglei alisema, "Kuwapa wakazi wa mijini habari kuhusu mahali wanapoweza kufanya matembezi na kupumzika, wakazi wa mijini wakifanya matembezi na kupumzika huko wanaweza kuchangia ongezeko la pato la wakulima."

Habari zinasema kutokana na uungaji mkono wa teknolojia ya mawasiliano ya habari, utalii wa utamaduni wa mila ya wakulima umepata maendeleo ya haraka, sehemu mbili za utalii wilayani Pinggu, ambazo zilitangazwa mwanzoni mwa mwaka huu kwenye tovuti, zilipokea watalii karibu 9,000 katika kipindi cha likizo la siku kuu ya Mei mosi, na pato la utalii lilizidi Yuan laki 2.4.

Katika mchakato wa kupanua matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya habari katika sehemu za vijijini nchini China, kutoa mafunzo mwafaka kwa wakulima ni moja ya kazi muhimu, lengo lake ni kuwawezesha wakulima wafahamu teknolojia ya mawasiliano ya habari na kuboresha kazi za uzalishaji mazao na shughuli za biashara. Mtaalamu wa kituo cha utafiti wa teknolojia ya uhandisi ya mawasiliano ya habari za kilimo cha taifa nchini China Bw. Yang Baozhu alisema, hivi sasa kiwango cha elimu katika sehemu za vijijini nchini China bado ni cha chini, uendelezaji wa matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ya habari unatakiwa kusukumwa mbele kwa njia za aina nyingi. Alisema, "Toka uzalishaji mali wa kilimo hadi viwanda vya sehemu za vijijini, habari za aina mbalimbali zinatolewa kwa wakulima kwa njia tofauti, ambazo ni pamoja na Internet na simu, ili kutoa uungaji mkono kamili kwa ujenzi wa vijiji vipya."

Bw. Yang Baozhu alisema katika miaka mitano ijayo, serikali ya China itawekeza Yuan bilioni kadhaa kwa sehemu za vijijini ili kuboresha miundo mbinu ya mawasiliano ya habari na kutoa mafunzo kwa wahandisi. Alidokeza kuwa vijiji vya China vya siku zijazo vitahimiza maendeleo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa teknolojia ya mawasiliano ya habari, kuinua kiwango cha teknolojia cha sehemu za vijijini na kufanya usimamizi wa demokrasia kwenye sehemu za vijijini.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-08