Waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia Bw. Ali Mohamed Gedi tarehe 8 mwezi huu huko Baidoa, alikutana na watemi wa huko wenye nguvu na ushawishi ili kutafuta uungaji mkono wao kwa baraza jipya la mawaziri litakaloundwa. Wachambuzi wanasema hii ni sehemu ya juhudi za Bw. Gedi za kutatua msukosuko wa serikali ya mpito.
Kwa mujibu wa msemaji wa serikali hiyo, Bw. Gedi alifanya mazungumzo na watemi hao juu ya orodha mpya ya mawaziri, akilenga kukamilisha uundaji wa baraza la mawaziri ndani ya wiki moja. Rais wa muda wa Somalia Bw. Abdullahi Yusuf Ahmed tarehe 7 mwezi huu alipovunja baraza la mawaziri, alisema ili kupunguza ukubwa wa idara na kuongeza ufanisi, baraza jipya la mawaziri litakuwa na mawaziri 31 na manaibu mawaziri 44 badala ya mawaziri 42 na manaibu mawaziri 80.
Serikali ya mpito ya Somalia iliyovunjwa iliundwa mwaka 2004 huko Nairobi, Kenya ambayo ilikomesha hali ya nchi hiyo ya kutokuwa na serikali iliyodumu kwa miaka 13. Kutokana na usuluhishi wa jumuiya ya kimataifa, mwaka 2004 pande mbalimbali za Somalia ziliafikiana juu ya mswada wa marekebisho ya katiba ya mpito na kuunda serikali ya mpito. Mwezi Juni mwaka 2005 serikali ya mpito ya Somalia ilihamishia ofisi zake nchini Somalia kutoka nchini Kenya, lakini imekuwa inashindwa kudhibiti hali ya nchi hiyo kutokana na kukosa nguvu na mbinu. Kwa hiyo hali ya vurugu nchini Somalia haikubadilika, hata serikali hiyo ya mpito yenyewe ilishindwa kuingia kwenye mji mkuu Mogadishu kutokana na kushindwa kujilinda, na iliweza tu kuweka ofisi zake huko Baidoa, mji uliopo kilomita 250 kusini magharibi mwa Mogadishu.
Tokea mwanzoni mwa mwaka huu nguvu ya kundi la Kiislamu liitwalo muungano wa mahakama za Kiislamu iliimarika siku hadi siku, na lilipambana vikali na muungano wa wababe wa kivita huko Mogadishu. Hadi kufikia mwezi Juni muungano wa mahakama za Kiislamu ulidhibiti mji wa Mogadishu na kukalia sehemu kubwa ya kusini mwa Somalia, na kuwa kundi lenye nguvu kubwa kabisa nchini Somalia na tishio kubwa kwa serikali ya mpito.
Ingawa serikali ya mpito ya Somalia na muungano wa mahakama za Kiislamu zilisaini makubaliano ya kusimamisha vitendo vyote vya uhasama dhidi yao katikati ya mwezi Juni, na kuamua kufanya duru jipya la mazungumzo ya amani katikati ya mwezi Julai, lakini hapo baadaye serikali ya mpito ya Somalia iliulaani muungano huo kuwaua wafuasi wa serikali na raia, na kupewa misaada na makundi ya kigeni ya ugaidi, serikali hiyo ikaamua kutofanya mazungumzo ya amani na muungano wa mahakama za Kiislamu. Kufuatia uamuzi huo, muungano huo ulipeleka wanamgambo wengi katika sehemu zilizo karibu na mji wa Baidoa, na serikali ya mpito ya Somalia ikaiomba nchi jirani ya Ethiopia itume wanajeshi kuilinda. Jambo hilo liliifanya serikali ya mpito ikabiliwe na msukosuko mbaya.
Kutokana na hali hiyo kulitokea maoni tofauti ndani ya serikali ya mpito ya Somalia juu ya masuala ya kuingiza wanajeshi wa kigeni na kufanya mazungumzo na kundi la Kiislamu. Tokea mwishoni mwa mwezi Julai maofisa waandamizi wasiopungua 43 walijiuzulu na wabunge kadhaa wa bunge la mpito la Somalia waliomba ipigwe kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu Gedi. Ingawa kura hiyo haikupitishwa, lakini serikali ya mpito ilipata pigo kubwa kutokana na tukio hilo.
Ili kutokemeza hali ya vurugu kwenye serikali ya mpito ya Somalia, kutokana na usuluhishi wa Ethiopia tarehe 6 mwezi Agosti, Bw. Gedi alikubaliana na rais Yusufi na spika wa bunge la nchi hiyo Bw Sharif Hassan Sheikh Aden kuhusu kufanya mazungumzo na kundi la Kiislamu, ambapo walikubaliana kuwa na mshikamano na kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri. Tarehe 7 Agosti rais Yusufi alitangaza kulivunja baraza la mawaziri la serikali ya mpito, isipokuwa alimwacha waziri mkuu Bw. Ali Mohamed Gedi abaki na wadhifa huo.
Hivi sasa Bw. Gedi anakabiliwa na kazi ngumu ya kuunda serikali mpya itakayoridhisha pande mbalimbali ili kuikwamua serikali ya mpito kutoka kwenye matatizo. Wachambuzi wanasema uwezo wa uongozi wa Bw. Gedi unakabiliwa na mtihani mgumu.
Idhaa ya kiswahili 2006-08-09
|