Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-09 16:46:36    
China yajitahidi kupunguza idadi ya vifo vya akina mama wajawazita wa kwenye sehemu zilizo nyuma kiuchumi

cri

Idadi ya vifo vya akina mama wajawazito ni kigezo muhimu cha kiwango cha maendeleo ya jamii na ustaarabu wa sehemu au nchi fulani. China ni nchi yenye eneo kubwa, na maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanatofautiana kwenye sehemu mbalimbali. Kwenye sehemu za kati na za magharibi nchini China zilizo nyuma kiuchumi, wanawake wajawazito wengi wanakufa wakati wa kujifungua. Kuanzia mwaka 2000, serikali ya China ilianzisha mradi unaolenga kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito. Hivi sasa mradi huo umepata maendeleo. Hivi karibuni, mwandishi wetu wa habari alitembelea sehemu zilizo nyuma kiuchumi mkoani Sichuan.

Wilaya ya Muchuan iliyoko kusini mwa mkoa wa Sichuan ni wilaya iliyoko milimani ambayo iko nyuma kiuchumi. Tulifika kwenye sehemu moja ya mlimani kutoka wilayani humo baada ya kusafiri kwa gari kwa dakika 40 kwenye barabara mbovu. Mwanakijiji Bi. Li Yunzhen anaishi kwenye sehemu ya kati ya mlima huu.

Tulifika kwenye nyumba ya Bi. Li Yunzhen baada ya kutembea mlimani kwenye njia yenye matope kwa nusu saa. Bi. Li Yunzhen ana umri wa miaka 40. Kuanzia mwaka 1990, alizaa watoto wanne kwa nyakati tofauti, kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, alilazimika kujifungua nyumbani, watoto watatu kati ya wanne walikufa wakati wa kujifungua, na maisha yake mwenyewe pia yalikuwa hatarini. Mwaka 2000, alipata uja uzito wa tano. Baada ya kufanyiwa upimaji, aliambiwa kuwa mtoto wake amekaa vibaya tumboni, kwa hiyo ni lazima akajifungulies hospitali. Hali hiyo ilimtia wasiwasi Bi. Li Yunzhen. Alisema:

"madaktari wa kijiji walinitaka niende kujifungulia hospitalini. Lakini mimi sikuwa na pesa za kutosha, niliona nalazimiaka kujifungulia nyumbani. Madaktari hao walishikilia kunitaka nikalazwe hospitalini. Waliniambia kwamba kama sina pesa naweza kulipa baadaye. Kwa hiyo nilijifungulia kwenye hospitali hiyo. Nawashukuru madaktari hao, kama nisingekuwa na msaada wao, huenda maisha ya mtoto wangu wa tano pia yangekuwa hatarini."

Kwa mujibu wa sera za huko, wakazi wa huko wenye matatizo ya kiuchumi kama Bi. Li Yunzhen anapewa ruzuku kadhaa kutoka kwa serikali wanapokwenda kujifungua kwenye hospitali, na pia si lazima kulipwa mara moja kwa malipo ya hospitalini yanayobaki.

Katibu wa kamati ya chama cha kikomunisti ya wilaya ya Muchuan Bw. Ye Sanqiang alieleza, kuanzia mwaka 2000, wajawazito zaidi ya 1300 wa wilaya hiyo wamepewa misaada ya fedha yuan laki 1.9 kwa jumla. kutokana na misaada hiyo, asilimia 70 ya wajawazito wanajifungua kwenye hospitali. Ingawa kiwango hicho bado ni chini, lakini maendeleo makubwa yamepatikana kuliko zamani. Hali hiyo imepunguza idadi ya vifo vya wajawazito katika mwaka 2005 kufikia asilimia 25 ya ile ya mwaka 1999.

Mbali na kutoa misaada kwa wajawazito wenye matatizo ya kiuchumi, wilaya hiyo pia ilitenga fedha kununua vifaa na dawa za lazima kwenye vituo vya huduma za afya vya tarafa na wilaya, na kutoa mafunzo kwa madaktari wa vijiji. Kutokana na wilaya hiyo kuwa kwenye sehemu ya milimani, wajawazito wengi wanaishi milimani ambako magari hayawezi kufika, hivyo wilaya hiyo pia ilianzisha kikundi cha wabeba machela kwa ajili ya wajawazito. Mkurugenzi wa idara ya afya ya wilaya hiyo Bi. Wen Li alisema:

"kutokana na kuwa wilaya yetu iko kwenye sehemu yenye milima, tulianzisha kikundi cha wabeba machela kwa ajili ya wajawazito wanaoishi milimani. kikundi hicho kinawapeleka wajawazito kwenye vituo vya huduma za afya wakati wanapokutwa na hali ya dharura. Kama tatizo lao haliwezi kushughulikiwa kwenye vituo hivyo, watahamishwa kwenye hospitali ya umma ya wilaya kwa kutumia magari ya wagonjwa."

Licha ya wilaya ya Muchuan, mradi wa kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito pia unatekelezwa kwenye wilaya ya Ebian, Jinkouhe, na Mabian zilizoko karibu. Hasa kwenye sehemu za makazi ya makabila madogomadogo na sehemu zilizoko nyuma kabisa kiuchumi, desturi na njia ya zamani ya kujifungua bado zinaendelea kutumika. Hivyo idara husika pia zilianza kutoa mafunzo ya afya ili kubadilisha mtizamo wa zamani wa kujifungua. Kwa mfano desturi ya zamani ya watu wa kabila la Yi wanaoishi kwenye wilaya ya Mabian, ni kuwa wajawazito ni lazima wajifungulie nyumbani, wakijifungua nje ya nyumba basi watoto si wao. Kutokana na juhudi za miaka ya hivi karibuni, waYi wengi wamebadilisha mtizamo huo wa zamani. Mjamzito mmoja wa kibila la Yi Bi. Tian Qiong aliyekuwa anataka kujifungulia hospitali alisema:

"ni afadhali kujifungulia kwenye hospitali, kwa kuwa hospitali ina vifaa bora. Sina wasiwasi kujifungulia hospitalini."

Imefahamika kuwa, serikali ya China ilianza kutekeleza mradi wa kupunguza vifo vya wajawazito kuanzia mwaka 2000, hivi sasa mradi huo unatekelezwa katika wilaya 1000, ambazo zipo kwenye sehemu za kati na za magharibi zilizo nyuma kiuchumi. Katika miaka 6 iliyopita, serikali ya China peke yake ilitenga yuan milioni 440 katika mradi huo, ambao ni mradi wa huduma kwa afya ya akina mama na watoto uliowekezwa fedha nyingi kabisa na serikali tangu kuanzishwa kwa China mpya. Msemaji wa wizara ya afya ya China Bw. Mao Qun'an alieleza, sehemu mbalimbali za China zimetumia fedha za mradi huo katika kutoa misaada kwa wajawazito wenye matatizo ya kiuchumi, pamoja na kueneza ufahamu husika, kununua vifaa na dawa, na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa vijiji. Hatua hiyo imepata mafanikio makubwa. Bw. Mao Qun'an alisema:

"hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005, idadi ya vifo vya wajawazito kwenye mikoa 23 iliyotekeleza mradi huo imepungua kwa 56.4/100,000, ikiwa imepungua kwa asilimia 25.8 kwa wastani kuliko mwaka 2001."

Bw. Mao Qun'an alisema, mradi huo utaenezwa zaidi kote nchini China. Aidha, China pia itaanzisha utaratibu kamili kwenye sehemu mbalimbali na kuchukua hatua halisi kuzingatia afya ya wajawazito.