Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-10 16:07:45    
Wageni wafurahia uzinduzi wa reli ya Qinghai-Tibet

cri

Reli ya Qinghai-Tibet iliyoko kwenye uwanda wa juu wenye mwinuko mkubwa kabisa duniani ilizinduliwa tarehe mosi Julai mwaka huu, jambo hilo lilimaliza historia ya mkoa unaojiendesha wa Tibet, kutokuwa na reli inayoiunganisha na mikoa mingine ya China. Reli hiyo pia inafuatiliwa na watu wengi duniani. Baadhi ya wageni wanasema reli ya Qinghai-Tibet si kama tu itawaletea Watibet heri na baraka na kuwaletea urahisi wa kuwasiliana na sehemu zilizo nje ya mkoa wa Tibet, bali pia itawanufaisha watu wa nchi za nje watakaokwenda Tibet kufanya biashara au kutalii.

Huko Lhasa, mji mkuu wa mkoa wa Tibet, barabara ya Barkor inafahamika sana kwa watalii. Duka la bidhaa za dhahabu liitwalo Syamukapu ambalo liko kando ya barabara hiyo lilianzishwa miaka mingi iliyopita, mwenye duka hilo Bw. Ratna Kumar Tuladhr mwenye umri wa miaka 45, ni raia wa Nepal.

Siku moja mwishoni mwa mwezi Juni mwandishi wetu wa habari alipotembelea duka hilo, alikuta pilika pilika za ukarabati wa duka. Mwenye duka Bw. Tuladhr alieleza kuwa, huu ni ukarabati mkubwa wa duka hilo tangu lianzishwe, umefanyika kwa zaidi ya mwezi mmoja na kugharimia Yuan laki 1 na elfu 50, sawa na dola za kimarekani elfu 20. Alisema "Naona baada ya kuzinduliwa kwa reli hiyo, biashara ya duka langu itapamba moto zaidi kwani watu wengi zaidi watakuja Tibet, wataitembelea Lhasa na duka langu. Kwa hiyo napaswa kufanya maandalizi hivi sasa."

Bw. Tuladhr amefanya biashara mjini Lhasa kwa miaka 22. Hivi sasa anaishi mjini Lhasa na kuendesha duka lake la bidhaa za dhahabu, na kila baada ya miezi kadhaa anarudi nchini Nepal kwa ajili ya kununua bidhaa. Lakini katika miongo kadhaa iliyopita, iliwabidi wafanyabiashara wa Nepal wasafirishe mizigo kwa farasi kati ya Lhasa na mji mkuu wa Nepal Kathmandu. Wakati huo huko Tibet kulikuwa hakuna umeme wala barabara.

Bw. Tuladhr alisema  "Hili ni jambo zuri kwa Tibet na Nepal. Tuna matarajio makubwa kutokana na kuzinduliwa kwa reli ya Qinghai-Tibet, kwani kwa kupitia reli hiyo bidhaa za China zitaweza kusafirishwa kutoka Qinghai hadi Lhasa, na bei za usafirishaji hakika zitapungua, na baadaye tutaweza kusafirisha bidhaa kutoka China hadi Nepal na kutoka Nepal hadi nchini China. Njia hiyo ya mawasiliano itasaidia biashara yetu, nafurahi sana."

Hivi sasa bado kuna wafanyabaishara wachache wa Nepal wanaoishi mjini Lhasa, wengi wao wanajishughulisha na sekta ya huduma, kama vile mikahawa na saluni. Kwa mujibu wa makadirio ya Bw. Tuladhr, kutokana na kuzinduliwa kwa reli na kuboreshwa kwa barabara kati ya Lhasa na kituo cha mpakani cha Zhangmu, watu wengi zaidi wa Nepal watakwenda Tibet kufanya biashara.

Mwandishi wetu wa habari aliendelea na matembezi kufuata barabara ya Bakor. Katika mkahawa uitwao Makye Ame wa chakula cha Kitibet, alimkuta Bibi Vivian MacDonald kutoka Scotland na watoto wake. Alipotoa maoni yake kuhusu reli ya Qinghai-Tibet, Bibi MacDonald alisema  "Kwa watu wa Tibet, bidhaa nyingi zaidi zitaweza kuingia huko, jambo ambalo litaboresha na kuleta urahisi kwa maisha yao. Baada ya kuzinduliwa kwa reli hiyo, naona watalii wengi zaidi watakuja kuitembelea Tibet kutokana na bei nafuu ya tiketi ya garimoshi. Zamani iliwabidi wasafiri kwa ndege, na safari hiyo ni ya gharama kubwa. Lakini reli itawapa fursa nzuri zaidi watu wanaotaka kutembelea Tibet."

Mbali na bei nafuu ya tiketi, kusafiri kwa njia ya reli pia ni chaguo zuri kwa watalii wanaovutiwa na mandhari nzuri ya uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet. Binti wa Bibi Macdonald, Dada Catnona alikuwa na hamu ya kusafiri kwa njia ya reli hiyo inayojulikana kama reli yenye mandhari nzuri kabisa duniani. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, anatumai kuwa safari ijayo ataweza kwenda Tibet kwa garimoshi. Alisema "Nikitumia garimoshi safari yenyewe itakuwa ndefu, lakini hakika nitaweza kuburudishwa na mandhari kando ya reli, ambayo ni nzuri zaidi kuliko niliyoona kupitia madirisha ya ndege. Naona watalii wataipenda reli. Safari ijayo tutakuja hapa kwa garimoshi, tutakaa kwa muda mrefu zaidi na kutembelea sehemu mbalimbali za Tibet, hata labda tutakwenda kuangalia kilele cha Qomolangma."

Kijana kutoka Israel Hagay Onn aliyekuwa karibu pia alitoa maoni yake kuhusu reli ya Qinghai-Tibet. Alisema "Itakuwa rahisi zaidi kuja Tibet na kuitafiti. Kwa Tibet, watu wa huko watapata fursa nyingi zaidi za kujitambulisha kwa dunia. Watu wengi wa nchi za kimagharibi watakuja kutalii."

Mbali na watu wapatao milioni 2 wa mkoa unaojiendesha wa Tibet, watu wa sehemu nyingine duniani pia wana matumaini kuhusu reli ya Qinghai-Tibet iliyoko kwenye uwanda wa juu wenye mwinuko mkubwa kabisa duniani.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-10