Tarehe 30 mwezi julai mwaka huu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliingia katika uchaguzi wake mkuu, ukiwa ni uchaguzi huru wa kwanza kufanyika katika nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 46 toka nchi hiyo ilipopata uhuru wake. Swali kubwa la kujiuliza ni, Je, baada ya hapo mambo yatakuwa shwari?
Umoja wa Ulaya uligharamia nusu ya gharama zote za uchaguzi huu, wa kihostoria nchini humo, uliogharimu takribani Euro millioni 180. Katika uchaguzi huo, Wagombea 33 walijitokeza kwenye kinyang'anyiro cha kiti cha urais wa nchi akiwemo rais wa serikali ya mpito inayoongoza Bw. Joseph Kabila huku watu 9,700 wakijitokeza kuwania viti 500 vya baraza la chini la Bunge la nchi hiyo ambapo wapiga kura 49,746 walijiandikisha. Kufanyika kwa uchaguzi huo wa kwanza huru kwa kipindi cha miaka 46 toka nchi hiyo ilipopata uhuru, ni matumaini kwa wananchi wake ambao hajawahi kuonja amani ya kweli toka wajikomboe kutoka mikononi mwa wakoloni.
Hata hivyo ikiwa bado matokeo rasmi ya uchaguzi kutolewa, tayari kumeanza kujitokeza hali ya kusigana baina ya wanasiasa, wababe wa kivita na taasisi za kijamii. Hali hiyo imetokana na watu hao kueleza waziwazi lengo lao la kupinga matokeo ya uchaguzi huo na kuingia tena msituni kupambana na majeshi ya serikali itakayoundwa na rais atakayetangazwa kushinda kwenye uchaguzi huo.
Mmoja wa watu waliotangaza rasmi dhamira ya kuingia tena msituni baada ya uchaguzi huo ni Jenerali Laurent Nkunda, aliyekuwa mmoja wa viongozi wa majeshi yaliyoshiriki kumpindua Rais Joseph Mobutu Seseseko.
Jenerali Kunda anayetafutwa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, amesema hatakuwa tayari kukamatwa na kushitakiwa kwa makosa hayo na kuwa yuko tayari kujadiliana na rais atakayeshinda katika uchaguzi huo juu ya jambo hilo likiwa kama sharti lake la kusitisha mapambano.
Katika madai yake Jenerali Kunda pia amesema atamtaka rais wa sasa akubali kuyaingiza majeshi yake katika kikosi cha majeshi ya serikali jambo ambalo kimsingi linaweza kukubaliwa, lakini likakwamishwa na sharti lake la kwanza la kutaka asishitakiwe kama mhalifu wa kivita sharti ambalo rais wa sasa wa serikali ya mpito, Bw. Joseph Kabila alikataa kulitimiza. Jenerali Laurent Nkunda amekuwa akishiriki kwenye vita ndani za nchi hiyo toka vita ya kumg'oa Mobutu mwaka 1998 na alikuwepo kwenye jeshi la serikali hadi alipoasi 2003.
Naye kiongozi mkongwe wa upinzani nchini humo, Jean-Pierre Bemba ambaye tayari ameonyesha dalili za wazi za kutoheshimu makubaliano ya uchaguzi huo yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa, yanayokataza mtu kujitabiria ushindi kabla ya matokeo kutolewa rasmi.
Bw Bemba aliitisha mkutano na waandishi wa habari siku moja toka kumalizika kwa upigaji kura na kutangaza kuwa matokeo ya mwanzo ya uchaguzi yaliyotolewa na mawakala wa chama chake walioshiriki kwenye kuhesabu kura yanaonyesha kuwa anaongoza katika majimbo sita kati ya majimbo 11 ya uchaguzi. Hata hivyo hesabu zilizotolewa na Bemba, mtu mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa katika eneo mashariki ya nchi hiyo lenye utajiri mkubwa wa madini, zinaonyesha kupingana na hesabu rasmi zilizotolewa katika baadhi ya vituo vya eneo hilo ambazo zinaonyesha kuwa rais wa serikali ya sasa ya mpito, Joseph Kabila ndiye anayeongoza.
Katika kampeni za uchaguzi kwenye eneo hilo Bemba alitumia mikutano na waandishi wa habari na kampeni za majukwaani kuilaani serikali ya Rais Kabila kwa kuingia mikataba mingi ya uchimbaji wa madini iliyo kinyume na sheria na amesema iwapo ataingia madarakani ataipitia upya. Bw Bemba, aliyeitumikia serikali ya mpito ya Rais Kabila kama makamu wa rais chini ya makubaliano ya amani yaliyositisha vita vya mwaka 1998-2003, ameshutumu mikataba 50 ya uchimbaji madini na kusema inapaswa kuangaliwa upya hasa mikataba inayohusu maeneo ya kusini mashariki ya jimbo la Katanga, ambayo ni ngome kuu ya rais Kabila.
Mbali na malalamiko kutoka kwa wanasiasa, raia wa kawaida wa Congo wamekuwa na mvuto mkubwa katika uchaguzi wa nchi hiyo kutokana na wengi wao kuishi katika hali ya umasikini mkubwa kutokana na rasilimali kubwa ya madini nchini mwao kushindwa kuwanufaisha kutokana na vita visivyokoma katika nchi yao. Jeshi la Umoja wa Mataifa lililopo nchini humo kwa upande wake limesema pamoja na kuwepo matukio ya ghasia za hapa na pale, uchaguzi ulifanyika kwa amani.
Idhaa ya Kiswahili 2006-08-11
|