Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-11 17:44:35    
Dawa za kutibu ugonjwa wa malaria zilizotengenezwa nchini China zafaa kwa Afrika

cri

Waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alipofanya ziara katika nchi saba za Afrika mwezi Juni mwaka huu alikwenda na zawadi iitwayo "Cotefu", ambayo ni dawa mpya ya kutibu malaria iliyotafitiwa na kutengenezwa maalum na kampuni ya dawa ya China kwa nchi za Afrika.

Kampuni iliyotengeneza dawa hiyo inaitwa Huali, iko mjini Hanzhou, kusini mashariki mwa China. Msemaji wa kampuni hiyo Bwana Zhao Jianghua alisema, hivi karibuni kampuni hiyo imetengeneza aina mbalimbali za dawa aina ya "Cotecxin" ya kutibu malaria, na tayari dawa hiyo imesajiliwa katika nchi 28 za Afrika na Asia kusini mashariki.

Hivi sasa dawa hiyo mpya ya "Cotefu" inafanyiwa majaribio hospitalini kwa kufuata vigezo vya shirika la afya duniani. Mwanzoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, watafiti wa China walifaulu kupata "Artemisinin" kutoka kwenye miti shamba, ambayo imethibitishwa na shirika la afya duniani kuwa ni dawa pekee yenye ufanisi mzuri ya kutibu malaria.

Malaria ni ugonjwa mkali wa kuambukizwa ambao bado unaenea sana katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara. Takwimu zilizotolewa na shirika la afya duniani zimeonesha kuwa, kwa wastani kila mwaka watu milioni 500 kutoka nchi zaidi ya 100 duniani wanaambukizwa malaria. Katika nchi za Afrika, kila mwaka watu milioni 3 hivi wanakufa kutokana na kuugua ugonjwa wa malaria, na kati yao zaidi ya nusu ni watoto wasiozidi umri wa miaka mitano.

Hivi sasa China ina kampuni kubwa tatu zinazotengeneza na kusafirisha nje dawa zinazohusiana na "artemisinin", kampuni ya Huali iliyoanzishwa miaka 12 iliyopita ni moja kati ya kampuni hizo. Kampuni hiyo inatafiti na kutengeneza dawa ya kutibu malaria kwa uvumbuzi wa kujitegemea, na kuzisafirisha dawa hizo barani Afrika. Kampuni hiyo ina mstari mzima wa kuotesha mbegu bora, kulima majani ya "Artemisia annua", kutafiti dawa mpya, kuchukua rasilimali ya "artemisinin", kutengeneza dawa na kutafuta soko la kimataifa. Hivi sasa asilimia zaidi ya 70 ya rasilimali ya "artemisinin" inayohitajiwa duniani inazalishwa na kampuni hiyo.

Kuanzia mwaka 2004, kampuni ya Huali imeanzisha matawi yake au ofisi zake katika nchi za Kenya, Tanzania, Nigeria, na Uganda na nchi nyingine barani Afrika. Mwezi Aprili mwaka 2006, kampuni ya Huali ilianzisha kituo cha usambazaji cha Afrika Mashariki huko Kenya, na kutengeneza dawa hizo barani Afrika. Kampuni ya Huali pia imeanzisha mfuko wa udhamini wa Huali wa masomo ya matibabu katika Chuo Kikuu cha tiba cha Kenya, ili kusaidia kutoa mafunzo ya ujuzi wa matibabu kwa watu wa huko.

"Artesumate" inayotengenezwa na kampuni ya dawa ya kusini ya Guilin ya China ilithibitishwa mwaka 2006 na shirika la afya duniani kuwa ni dawa muhimu ya kuwatibu wagonjwa wenye malaria sugu.

Ofisa mkuu mtendaji wa kampuni ya dawa ya kusini ya Guilin ya China Bwana Yan Xiaohua alisema, kwa kuwa watu wengi wa Afrika wanaougua malaria ni watu wasio na uwezo kifedha, tunaweza kusema kuwa dawa ya "artesumate" ni dawa kwa ajili ya watu maskini, wachina hawakusudii kujipatia faida kubwa kutokana na dawa hiyo, hivyo bei ya "artesumate" inayotengenezwa na kampuni hiyo inayouzwa barani Afrika ni asilimia 60 tu ya bei ya dawa zinazotengenezwa na nchi za magharibi.

Bw. Yan Xiaohua alisema hivi sasa shirika la afya duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, chama cha msalaba mwekundu cha kimataifa na shirika la Umoja wa Mataifa la utoaji msaada yananunua moja kwa moja "artesumate" kutoka kwa kampuni ya dawa ya kusini ya Guilin. Licha ya mashirika ya kimataifa, dawa za kutibu malaria zilizotengenezwa na kampuni hiyo pia zinanunuliwa kwa wingi na serikali na wakala binafsi, kama vile Sudan, Msumbiji, Jamhuri ya Kongo.

Bw. Yan Xiaohua alisisitiza kuwa, "artesumate" iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya kusini ya Guilin ilithibitishwa kuwa na sifa ya GMP na shirika la afya duniani. Ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa, kuanzia mwaka 2004 kampuni hiyo imeanzisha mstari kamili wa kutengeneza dawa ya kutibu malaria, kuanzisha mashamba makubwa ya kulima majani ya "artemisia", na kusindika rasilimali ya "artemisinin".

Imefahamika kuwa hivi sasa dawa zaidi ya 40 za kutibu malaria zilizotengenezwa na nchi mbalimbali duniani zimethibitishwa na shirika la afya duniani, na makampuni yote yanaagiza rasilimali ya "artemisinin" kutoka China. Hivi sasa dawa za kutibu malaria zilizotengenezwa na kampuni ya Guilin zimesajiliwa na kuuzwa katika nchi 34 duniani.

Bw. Yan Xiaohua alisema hivi sasa mahitaji ya dawa ya kutibu malaria duniani yanaongezeka kwa haraka. Takwimu zilizotolewa na shirika la afya duniani zinaonesha kuwa, kila mwaka kuna wagonjwa milioni 300 hadi 500 wa malaria duniani, baada ya kuchaguliwa kuwa kampuni inayotoa dawa moja kwa moja kwa shirika la afya duniani, kampuni ya dawa ya kusini ya Guilin inatumia mstari wake kamili wa kutengeneza "artesumate", ili kupunguza gharama kwa shirika la afya duniani, na kuwapatia wagonjwa wa malaria duniani dawa yenye bei nafuu na yenye ufanisi mzuri.