Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-14 16:36:25    
Mkutano kuhusu ugonjwa wa Ukimwi duniani wafunguliwa Toronto

cri

Mkutano wa 16 kuhusu ugonjwa wa Ukimwi duniani ulifunguliwa tarehe 13 huko Toronto, nchini Canada. Wataalamu, wasomi na maofisa watapao zaidi ya elfu 20 kutoka sehemu mbalimbali duniani wanahudhuria mkutano huo, wakijadili kwa pamoja masuala yanayohusu kinga na tiba ya Ukimwi.

Kauli mbiu ya mkutano huo ni "wakati wa kuchukua vitendo", ambapo inalenga kuifanya kazi ya kinga na tiba ya ukimwi iweke mkazo katika kinga, utafiti wa chanjo na kuharakisha kuwapatia wagonjwa dawa husika. Mwenyekiti wa mkutano huo Dr. Mark Wainberg alisema:

"Tutajadili matokeo ya kisayansi yaliyopatikana katika utafiti kuhusu Ukimwi, na kutoa dawa mpya zenye uwezo wa kuboresha afya ya wagonjwa wa Ukimwi. Lengo letu lingine ni kuhimiza usawa. Mgonjwa yeyote wa Ukimwi ana haki ya kupewa tiba bila kujali uwezo wake wa kulipa gharama za matibabu."

Tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita, Ukimwi umekuwa ukienea kwa kasi sana duniani, hadi leo umesababisha vifo vya watu milioni 25 duniani. Kutokana na makadirio ya shirika la afya duniani WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi UNAIDS, hivi sasa watu milioni 40 duniani wameambukizwa virusi vya Ukimwi, mwaka jana watu milioni 4.1 waliambukizwa virusi vya Ukimwi na wengine milioni 2.8 walikufa kutokana na Ukimwi. Japokuwa idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi katika nchi kadhaa za Caribbean na Afrika imepungua kiasi, lakini kwa siku watu elfu 11 duniani wanakufa kutokana na Ukimwi.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa UNAIDS Bwana Peter Piot alisema, ni lazima kuchukua hatua mwafaka za kupambana na Ukimwi, yaani kuhimiza utafiti wa kisayansi, kuwafahamisha binadamu ujuzi kuhusu Ukimwi, na kuondoa unyenyepa dhidi ya wagonjwa wa Ukimwi. Akisema:

"Mapambano dhidi ya Ukimwi yatachukua muda mrefu na hata vizazi kadhaa. Kama hatutachukua hatua ya dharura ya kukinga ugonjwa huo, watu watakaoambukizwa virusi vya Ukimwi wataongezeka mwaka hadi mwaka, na tatizo la Ukimwi litakuwa mzigo mkubwa sana kwa binadamu katika siku zijazo."

Bw. Piot alisema UNAIDS itasimamia hali ya matumizi ya mfuko wa kinga na tiba ya Ukimwi duniani ili fedha hizo zisifujwe. Pia alizihimiza serikali za nchi zitunge sera husika za kutilia maanani kinga na tiba ya Ukimwi na kuondoa unyenyepa dhidi ya wagonjwa wa Ukimwi.

Msichana mwenye umri wa miaka 24 wa Indonesia Frika Chia Iskandar, anafahamu vizuri unyenyepa dhidi ya wagonjwa wa Ukimwi. Hivi sasa Bi. Frika ameteuliwa kuwa mshauri wa shirika la mtandao wa Internet wagonjwa wa Ukimwi wa sehemu ya Asia na Pasifiki, ambapo anatoa ushauri na upendo kwa wagonjwa wa Ukimwi, ili wapambane na hali ya unyenyepa dhidi ya wagonjwa wa Ukimwi. Alisema:

"Watu wengi waishio vijijini hushindwa kupata tiba baada ya kuambukizwa virusi vya Ukimwi, kwa sababu hawana pesa za kwenda hospitali."

Habari zinasema mwaka jana fedha zilizotumiwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi duniani zilifikia dola za kimarekani bilioni 8, lakini kutokana na makadirio ya UNAIDS, kutoa tiba pekee kunahitaji dola za kimarekani bilioni 15 kwa mwaka. Mbali na Ufaransa, michango iliyotolewa na nchi nyingine za kundi la Nchi Nane hazikufikia kiwango kilichotazamiwa kwa mfuko wa kinga na tiba ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria duniani.

Wataalamu wanachukulia kuwa, shughuli za kinga na tiba ya Ukimwi zinatakiwa kulenga kuwaelimisha wanawake na watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja. Hivi sasa nusu ya wagonjwa wa Ukimwi na walioambukizwa virusi vya Ukimwi ni wanawake. Katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa Sahara, wanawake walioambukizwa virusi vya Ukimwi wanachukua asilimia 60 ya jumla ya watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi.

Wanaohudhuria mkutano huo wanaona kuwa, nchi mbalimbali zinapaswa kupambana na Ukimwi kwa mtizamo wa maendeleo, kutilia maanani kukinga, kutibu, kutunga sera husika na kuimarisha ufahamu wa jamii kuhusu Ukimwi.