Tarehe 15 Agosti, waziri mkuu wa Japan Bw Junichiro Koizumi alifikia hatua ya kwenda tena kwenye hekalu la Yasukuni bila kujali upinzani wa watu wengi wa nchini Japan na duniani, na kutoa heshima kwa mizimu ya wahalifu wa kivita. Tokea ashike wadhifa wa waziri mkuu wa Japan mwezi Aprili mwaka 2001, Bw Koizumi ameshikilia kwenda kwenye Hekalu la Yasukuni kwa miaka 6 mfululizo, kitendo chake cha ukaidi si kama tu kimedhuru vibaya hisia za wananchi wa China waliovamiwa na wavamizi wa kijeshi wa Japan, bali pia kimeharibu sura ya Japan duniani.
Bw Koizumi aliwahi kujitetea kuwa anakwenda kwenye hekalu la Yasukuni kutokana na "hisia" zake binafsi, lakini je, anatambua hisia walizo nazo mamia na maelfu ya watu waliodhuriwa katika vita vilivyoanzishwa na Japan? Alijitetea mara kwa mara kuwa kusudi lake ni kuwaombea watu waliokufa katika vita, na kusisitiza nia ya kutoanzisha vita. Lakini je amekwenda kwenye hekalu gani mara kwa mara? Hekalu la Yasukuni ni alama ya uvamizi na upanuzi wa Japan katika nchi za nje, na pia ni kumbukumbu ya wababe wa kivita, miongoni mwa vibao vya wahalifu wa kivita vilivyowekwa kwenye hekalu hilo, kuna vibao 14 vya wahalifu wa kivita wa ngazi ya A ambao waliwahi kuanzisha na kuongoza vita vikuu vya pili vya dunia akiwemo Hideki Tojo. Bw Koizumi anakwenda kwenye hekalu hilo kutoa heshima mara kwa mara, kitendo hiki kinawadhalilisha wananchi wa nchi mbalimbali za Asia waliowahi kukandamizwa na wavamizi wa kijeshi wa Japan.
Kama raia wa kawaida wa Japan wanakwenda hekalu kuwaomboleza jamaa zao waliokufa katika vita, hizi ni hisia za watu wa kawaida, hatuwezi kuwalaumu, kwani raia sio waanzishaji wa vita, tena raia wengi kabisa wa Japan pia walidhuriwa katika vita. Lakini Bw Koizumi ni waziri mkuu wa Japan, maneno na vitendo vyake vinaiwakilisha serikali ya Japan. Kitendo chake cha kwenda kwenye Hekalu la Yasukuni si kama tu kinamaanisha mtizamo wake wenye makosa kabisa kuhusu historia, bali pia kinamaanisha kuwa serikali ya Japan si kama tu haijikosoi kwa kina kutokana na historia yake ya uvamizi, bali pia inajaribu kuficha ukweli wa mambo wa historia, na kujitetea chini juu kuhusu ubabe wake wa kijeshi.
Miaka mitano iliyopita tangu Bw Koizumi ashike wadhifa wa waziri mkuu wa Japan, kutokana na suala la kwenda kwenye Hekalu la Yasukuni, maendeleo ya kawaida ya uhusiano kati ya Japan na nchi majirani zake yameharibiwa vibaya. Tarehe 14 mwezi huu waziri mkuu wa Korea ya kusini Bibi Han Myung-sook amedhihirisha kuwa, kitendo cha Bw Koizumi kimezuia maendeleo ya siku za usoni ya uhusiano kati ya Korea ya kusini na Japan.
Hivi karibuni maofisa na wasomi wa Marekani ambayo ni nchi mshirika wa Japan pia wameeleza wasiwasi wao kuhusu kitendo cha Bw Koizumi na kukikosoa. Mkurugenzi wa idara ya utafiti ya Asia ya mashariki ya Marekani Bwana Kent Calder alisema, kama wamarekani wakielewa undani wa Hekalu la Yasukuni hakika wataweza kutoa shutuma kali zaidi.
Uhusiano kati ya China na Japan unakabiliwa na matatizo kutokana na Bw Koizumi kwenda kwenye Hekalu la Yasukuni kutoa heshima kwa mizimu ya wahalifu wa Japan, hili si jambo zuri kwa nchi hizo mbili. China imefanya juhudi kadiri iwezavyo ili kuboresha uhusiano kati yake na Japan. Tatizo sugu katika uhusiano kati ya China na Japan ni kitendo cha Bw Koizumi kwenda kwenye hekalu la Yasukuni. China imeeleza wazi sana namna ya kutatua tatizo hilo sugu, kama Bw Koizumi ataacha kwenda kwenye hekalu la Yasukuni, mazungumzo na mawasiliano kati ya viongozi wa China na Japan yanaweza kufufuliwa.
Bw Koizumi anashikilia ukaidi wake bila kujali juhudi za upande wa China. Lakini wananchi wa Japan wameona wazi kitendo chake. Uchunguzi wa maoni ya raia uliofanyika hivi karibuni nchini Japan umeonesha kuwa, wananchi wa Japan wanaopinga kitendo cha waziri mkuu huyo kwenda Hekalu la Yasukuni wamefikia asilimia 60, na wanaomwunga mkono wamepungua na kufikia asilimia 20 tu. Kitendo cha Koizumi kimemfanya Bw Koizumi apoteze uungaji mkono wa wananchi, na jambo la kuhuzunisha zaidi ni kuwa, kitendo chake kimeharibu sura ya Japan ya nchi ya amani duniani iliyoienzi katika miaka 61 iliyopita baada ya vita vikuu vya pili vya dunia. Kitendo cha Bw Koizumi kimeleta hasara kubwa kwa mambo ya kidiplomasia ya Japan na kuacha ukurasa wa aibu katika historia ya Japan.
|