Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-15 20:37:30    
Kasi mpya ya uchumi wa kando ya magharibi ya mlangobahari wa Taiwan

cri

Kwenye pwani ya kusini mashariki ya China kuna mkoa mmoja ambao ulikuwa wa kwanza kutekeleza sera za mageuzi na ufunguaji mlango zaidi ya miaka 20 iliyopita. Lakini baada ya hapo, kasi ya ongezeko la uchumi wa huko ilipungua, na mkoa huo ukatoka kwenye kikundi cha mbele kabisa katika maendeleo ya uchumi nchini China. Katika mpango wa maendeleo ya uchumi na jamii ya miaka mitano ijayo, mkoa huo umethibitishwa kuwa sehemu itakayopewa kipaumbele katika maendeleo ya uchumi. Katika kipindi cha leo, tunawaeleza jinsi mkoa wa Fujian, ulioko kando ya magharibi ya mlangobahari wa Taiwan ulivyoinuka tena kiuchumi.

Mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, baadhi ya mikoa ya pwani ya mashariki ya China ilitangulia kutekeleza sera za mageuzi na ufunguaji mlango. Wakati huo mkoa wa Fujian ukitumia ubora wa kijiografia wa kuwa karibu na Hong Kong, Macau na Taiwan, ulivutia uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka nje kiurahisi. Lakini baada ya miaka zaidi ya 20, maendeleo ya uchumi wa mkoa wa Fujian yamekuwa madogo sana ikilinganishwa na mkoa wa Guangdong, ambao ni jirani yake ulioanza kutekeleza sera za mageuzi na ufunguaji mlango karibu kwa wakati mmoja na mkoa wa Fujian. Katika mwaka 2005, pato la mkoa wa Guangdong lilifikia Yuan za Renminbi trilioni zaidi ya 2.1, ikilinganishwa na pato la mkoa wa Fujian, ambalo lilikuwa Yuan bilioni 650, na uwekezaji kutoka wafanyabiashara wa Taiwan pia ulikuwa mdogo ikilinganishwa na wa ule wa mkoa wa Guangdong.

Mkuu wa taasisi ya utafiti wa sayansi ya jamii ya mkoa wa Fujian, Bw. Yan Zheng alisema, hapo awali kitu kilichovutia uwekezaji kutoka kwa wafanyabiashara wa Taiwan, ni uhusiano ambao mababu wao walizaliwa katika mkoa wa Fujian, lakini kutegemea tu uhusiano huo hakutoshi kabisa.

"Mkoa wa Fujian uko karibu zaidi na Taiwan ikilinganishwa na mikoa mingine ya China bara, lakini kutokana na vizuizi vya utawala wa Taiwan, watu na mizigo haiwezi kufika moja kwa moja kwenye kando ya magharibi isipokuwa ni lazima izunguke kupitia Hong Kong, hivyo gharama zinaongezeka. Sehemu mpya iliyo nzuri zaidi kwa wawekezaji wa wafanyabiashara wa Taiwan ni mkoa wa Guangdong. Kwanza mkoa huo uko karibu, pili una mazingira bora ya viwanda kutokana na uwekezaji wa Hong Kong na Macau kwenye delta ya mto Lulu. Ilipofika mwishoni mwa miaka ya 90, makampuni makubwa ya Taiwan yalikuja China bara kuwekeza, Shanghai, ambayo ni kitovu cha uchumi wa China."

Bw. Yan zheng alsiema kutokana na upungufu wa ukamilifu wa sekta za uzalishaji mali na hali hafifu ya miundo-mbinu kasi ya ongezeko la uchumi wa mkoa wa Fujian ilipungua. Na kasoro hiyo ilikuwa wazi zaidi, wakati mikoa mingine ilijitahidi kuboresha mazingira ya uwekezaji.

Jambo linalofurahisha ni kuwa pamoja na ujenzi wa kando ya magharibi ya mlangobahari wa Taiwan kuwekwa katika mpango wa maendeleo ya uchumi na jamii wa miaka mitano ijayo, mkoa wa Fujian unakazana kujenga bandari kwenye kando ya magharibi ya mlango wa bahari wa Taiwan ili kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kando ya magharibi ya mlango wa bahari kwa ujenzi wa bandari. Mkoa wa Fujian una pwani yenye urefu wa kilomita zaidi ya 3,300 ukichukua nafasi ya pili nchini China, na mlangobahari wa Taiwan ulioko mkabala, ni moja ya njia muhimu za uchukuzi za baharini duniani. Hivi sasa magati yenye kina kirefu cha maji yanayoruhusu meli zenye uwezo wa kubeba tani laki 1 hadi 3 za mizigo kutia nanga, yanajengwa kwenye pwani ya mkoa wa Fujian. Habari zinasema katika miaka 5 ijayo, serikali ya mkoa wa Fujian itatenga Yuan zaidi ya bilioni 29 kwa ajili ya ujenzi wa bandari, ifikapo mwaka 2010, uwezo wa bandari za mkoa wa Fujian wa kushughulikia mizigo utazidi tani milioni 300.

Pamoja na harakati kubwa za ujenzi wa bandari, eneo la viwanda la Lingang limestawi. Bandari mpya ya Fuzhou ni bandari kubwa yenye kina kirefu cha maji inayofaa sana kwa meli za makontena, kiongozi wa ofisi ya usimamizi ya bandari hiyo Bw. Cai Fuyong alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, hivi karibuni wanajenga eneo lenye viwanda vingi na bandari ya kisasa vinavyoshughulikia kazi za nishati, kemikali na usambazaji bidhaa. Alipozungumzia manufaa ya kuendeleza kazi za viwanda alisema,

"Kama mjuavyo kwa viwanda vya kisasa, gharama kubwa ni ya usambazaji bidhaa licha ya gharama za mali-ghafi na nguvu-kazi. Gharama ya usafirishaji kwa njia ya baharini ni ya chini zaidi. Eneo la viwanda la Lingang linasafirisha bidhaa nyingi zinazokwenda nchi za nje na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, eneo letu la viwanda limepunguza sana gharama za uzalishaji kwa viwanda, hivyo tunataka kujenga vituo vya viwanda na vya sekta za usindikaji na biashara."

Ifikapo mwaka 2010, mkoa wa Fujian utakuwa na vituo kadhaa vya kazi za kemikali ya mafuta ya asili ya petroli, nishati, magari na matengenezo ya meli. Wakati huo pato la eneo la viwanda la Lingang kutokana na uzalishaji wa viwanda litazidi 45% ya pato la viwanda vya mkoa wa Fujian. Uboreshaji wa miundo-mbinu ikiwemo bandari, umevutia viwanda vingi vya Taiwan. Hivi sasa sekta za teknolojia za kisasa zikiwemo za mawasiliano ya habari ya elektroniki, dawa za viumbe na mitambo ya hali ya juu za Taiwan, zimejenga viwanda mkoani Fujian. Mwezi Februari mwaka huu, kampuni ya photoelectricity ya Youda ya Taiwan, ambayo inachukua nafasi ya 3 duniani kwa uzalishaji wa skrini za LCD, ilianza kujenga kiwanda kwenye eneo la ustawishaji wa teknolojia ya kisasa la mji wa Xiamen, mkoani Fujian, uwekezaji wake utafikia dola za kimarekani milioni 500. Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa eneo hilo Bw. Sun Dahai alisema, kufika kwa kampuni ya youda kumeongeza ushawishi na mvuto kwa sekta mbalimbali za uzalishaji wa bidhaa.

"Umuhimu wa mradi huo hauko katika mradi huo peke yake, bali ni kuleta viwanda kumi kadhaa vinavyohusika na kazi za kampuni hiyo. Kazi nyingine za kutoka taa za tube, kioo cha LCD hadi mabapa ya kukusanya mwangaza ni kazi kubwa, ambazo kampuni ya Youda haina uwezo wa kuzifanya, kazi za kampuni ya Youda ni kuziunganisha zana hizo tu. Uwezo wa uzalishaji wa mradi huo utafikia Yuan bilioni 40, na jumla ya uwezo wa uzalishaji wa viwanda vyote vinavyohusika ni Yuan bilioni 20 hadi 30."

Mbali na sekta za teknolojia za kisasa, hali ya hewa inayofanana kati ya Fujian na Taiwan pia imevutia wafanyabiashara wengi wa Taiwan kwenda kuwekeza katika kilimo mkoani Fujian. Mfanyabiashara wa Taiwan Bw. Xu Ciyan alianzisha kampuni ya maua ya orchid kwenye eneo la mashamba ya wakulima kutoka Taiwan la wilaya ya Zhangpu, kusini mwa mkoa wa Fujian. Bw. Xu alisema hivi sasa maua ya shamba lake yanauzwa sana katika masoko ya nchi za Ulaya, mwaka jana alisafirisha miche ya maua milioni kadhaa, na mwaka huu atasafirisha miche mingi zaidi. Mambo mbalimbali yanaonesha kuwa mkoa wa Fujian unajitahidi kutafuta nafasi na kuwania kasi kubwa ya maendeleo.