Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-15 21:09:33    
Barua 0815

cri

Wasikilizaji wapendwa, ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Leo kama kawaida tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Bw. Mogire O. Machuki wa S.L.P 646, Kisii, Kenya ametuandikia barua alitoa pongezi zake kwa wahusika wa Radio China Kimataifa kwa upande wa tovuti ambayo imepewa sura mpya. Alisema sasa hivi tovuti ya Radio China inaendelea kuwavutia zaidi wasikilizaji kadri siku zinavyozidi kusonga, anawaomba wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wakiwa na nafasi watembelee tovuti ya Radio China Kimataifa ana hakika kuwa wataridhika na taarifa kemkem ambazo zimechapishwa huko.

Pia alisema anafurahi kuwa mmoja miongoni mwa wasikilizaji wachache waliochaguliwa kutuzwa zawadi baada ya kukamilika rasmi shindano kuhusu "Taiwan-kisiwa cha hazina cha China". Ni matumaini yake kuwa itafikia siku njema ambapo kisiwa cha Taiwan kitarudi chini ya mamlaka ya China. Katika barua yake Bw. Mogire anapenda kumpongeza Rais wa China Bw. Hu Jintao na ujumbe wake kuitembelea Kenya mwezi Aprili mwaka huu. Anasema ziara ya Rais Hu nchini Kenya ilifanyika wakati ambao Kenya inakabiliwa na hali ngumu kiuchumi. Alipokutana na viongozi wa ngazi za juu wa Kenya, Rais Hu alizungumzia mambo kadha wa kadha, hasa kuhusu sekta ya uchumi ambayo Kenya itapata faida nyingi kutokana na kuwa na ushirikiano mzuri na China.

Bw. Mogire anasema ana imani kuwa mikataba iliyosainiwa kati ya Rais Hu Jintao na Rais Mwai Kibaki itachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza pato la Mkenya wa kawaida ambaye anaishi chini ya dola moja kwa siku. Uhusiano kati ya Kenya na China kama alivyoelezea Rais Hu Jintao ni wa jadi. Mwanamaji maarufu kutoka China Zheng He aliwahi kuongoza ujumbe wake wa merikebu hadi kufika pwani ya Kenya katika miaka 600 iliyopita. Aidha, uhusiano huu umejikikita na unaendelea kuimarika siku hadi siku.

Bw. Machuki anaona nchini Kenya sasa hivi vitega uchumi kutoka China vinaongezeka kwa kiasi kikubwa. Wakenya wanaendelea kuufurahia uhusiano wa kunufaishana kati ya Kenya na China, kwa vile zaidi ya asilimia 60 ya bidhaa wanazozitumia nchini Kenya zinatengenezwa China. Hivyo basi urafiki kati ya China na Kenya ni wa kipekee ila hofu iliyopo ni kuwa mataifa ya magharibi na Marekani huenda yatapinga uhusiano huu.

Bwana Machuki pia anasema Rais Hu Jintao wa China alipokuwa nchini Kenya alipata fursa ya kukutana na wanafunzi wa Chuo cha Confucius wanaojifunza lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya. Anasema alipigwa na butwaa na furaha pia, aliposikia kuwa kitivo cha Confucius kwenye Chuo Kikuu cha Nairobi ndicho cha kwanza kuanzishwa na serikali ya China kote barani Afrika. Pia anafurahia kwamba Radio China Kimataifa iliichagua Kenya kama eneo lake la kwanza la uzinduzi wa kituo cha kimataifa kinachosikika kwenye wimbi la FM. Alisema hizi ni baadhi tu ya faida ambazo Kenya imeridhika nazo kutoka kwa serikali ya China. Wakenya wengi walivutiwa sana na ziara ya Rais Hu Jintao nchini Kenya, na Radio China Kimataifa na vyombo vya habari vya Kenya vilitumia muda mwingi kutangaza habari kuhusu ziara hiyo na uhusiano kati ya mataifa mawili.

Tunamshukuru sana Bwana Mogire Machuki kwa barua yake ya kutuelezea mengi ya kufurahisha na kututia moyo, Tunaridhishwa kwa kutueleza mtazamo wako kuhusu ziara ya Rais Hu Jintao nchini China na jinsi vyombo vya habari vya Kenya vilivyotangazwa habari kuhusu ziara hiyo .

Msikilizaji wetu mwingine Ali Hamisi Kimani wa S.L.P 61 Othoro, Kenya ametuletea shairi aliyotunga lisemalo : Nuru ya tumaini FM 91.9 Radio China kimataifa Idhaa ya Kiswahili, Shairi lake linaanza kwa kusema

Wataalamu wenye kuunga,

Wamejitoa mhanga

Kutafuta dawa tosha,

Ya mawimbi kuvizia.

Katika zao shughuli

Wanasema kuna suluhisho

Kuyaimarisha mawimbi

Ya FM 91.9 Radio China

Hivyo wanatushauri

Tusifanye papara

Tuende na wakati

Vipindi kusikiza

Ukiyapata mawimbi

Nuru yenye tumaini

Kwa wasikilizaji duniani

Ahueni kutokea

Kuna nuru ya thamani

Nuru yenye tumaini

Wasikilizaji Afrika Mashariki

Anza leo kusikiliza

Msikilizaji wetu Edward Kavai Abuogi wa P.O. Box 838 Kitale, Kenya katika barua yake aliyotuandikia amejibu maswali kadhaa ya makala ya pili ya chemsha bongo kuhusu Mimi na Radio China kimataifa. Edward yuko sehemu ya kaskazini mwa bonde la ufa yaani mkoani Rift Valley katika kijiji cha Bimuda huko Kitale, Kenya.

Anaomba awe mgeni maalum wa Radio China kimataifa na tumwalike aje Beijing, na kuitembelea China mnamo mwezi wa Desemba. Anasema yeye anasikiliza matangazo ya Radio China kila Jumapili kuanzia saa nane hadi saa tisa mchana wakati anapopumzika. Katika barua yake pia anasema angependa apate rafiki wa barua awe wa kike au wa kiume kutoka China ili wawasiliane kwa njia ya barua, anaomba tumtumie kijitabu kinachoelezea jiografia, mambo ya ardhi na picha za China, utalii na mambo mengineyo. Na mwisho anatoa shukurani kwa vipindi vya Radio China Kimataifa na kipindi cha daraja la urafiki kati ya China na Afrika.

Tunamshukuru Bw Edward Kavai Abuogi kwa jibu lake, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza vipindi vyetu, kutoa maoni na mapendekezo yake ili kutusaidia kuboresha vipindi. Pia tunapenda kumuarifu kuwa kushiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo si tiketi ya moja kwa moja ya kupata tuzo maalum ya kualikwa kuja kutembelea Beijing, China, kwani wasikilizaji wetu wengi wanashiriki kwenye mashindano hayo, na kila mwaka, kwa jumla ni wasikilizaji wachache tu wa idhaa mbalimbali za Radio China kimataifa wanaoweza kupata tuzo maalum na kualikwa kuja China. Labda mwaka huu idhaa yetu ya Kiswahili atajitokeza tena msikilizaji mmoja atakayepata tuzo maalum. Tusubiri bahati hiyo.