Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-16 19:43:38    
Hali ya sasa na matumaini ya kupatikana kwa chanjo ya Ukimwi

cri

Utafiti wa wanasayansi kuhusu chanjo ya ugonjwa wa Ukimwi ulianza miaka 20 iliyopita. Mwaka 1987 chanjo ya kwanza ya Ukimwi duniani ilifikia hatua ya kutumika kwa binadamu, lakini hadi hivi leo hakuna aina moja kati ya aina zaidi ya elfu moja za chanjo za Ukimwi, inayoweza kukinga maambukizi ya Ukimwi. Lakini kwanini ni vigumu sana kudhibiti virusi vya Ukimwi? Mwenyekiti wa harakati ya chanjo ya Ukimwi duniani Bw. Seth Berkley alieleza matatizo waliyokutana nayo katika utafiti husika.

"Virusi vya Ukimwi vinabadilika mara kwa mara, licha ya hayo virusi hivyo vina gene za aina nyingi tofauti. Pili, virusi vya Ukimwi vinaweza kudanganya mfumo wa kinga ya mwili wa binadamu, na kujificha mwilini mwa mgonjwa, na siyo rahisi kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili. Aidha tunapofanya utafiti kuhusu chanjo za magonjwa ya aina nyingine, mara kwa mara tunapata fununu kutokana na mtu aliyeambukizwa ugonjwa na kisha kurejewa nguvu za kinga za mwilini, lakini bado hatujasikia kuwa mgonjwa wa Ukimwi anaweza kurejewa nguvu za kukinga virusi vya Ukimwi."

Hivi sasa "tiba ya cocktail" inachukuliwa kuwa tiba yenye ufanisi zaidi miongoni mwa aina mbalimbali za dawa za Ukimwi. Hivi karibuni mamlaka ya usimamizi wa chakula na dawa nchini Marekani iliidhinisha dawa ya ugonjwa wa Ukimwi inayotumika "tembe moja kwa siku", lakini inashidwa kuua kabisa virusi vya Ukimwi mwilini, ila tu kutuliza hali ya mgonjwa au kuahirisha mwendo wa ugonjwa.

Shirika la utoaji misaada la Bill Clinton, rais wa zamani wa Marekani, siku zote linajitahidi kuhusu udhibiti wa ugonjwa wa Ukimwi duniani. Bw. Clinton alisema tukitaka kuona dunia isiyo na Ukimwi, basi ni lazima kuwa na chanjo ya Ukimwi.

"Tusiache, tunatakiwa kuendelea kuunga mkono utafiti wa chanjo za Ukimwi duniani, na kutoa misaada ya fedha kwa utafiti unaofanyika katika nchi mbalimbali. Nilipokuwa rais, tulidhani tungeweza kupata chanjo baada ya miaka 10, lakini sasa tunaona siyo jambo baya, kama tutaweza kuwa na chanjo zake baada ya miaka 10 mingine."

Hata hivyo habari nzuri kuhusu utafiti zilisikika mara kwa mara. Katika muda wa siku 6 wa mkutano wa ugonjwa wa Ukimwi duniani wa mwaka huu, wanasayansi watatangaza mafanikio 4,500 ya utafiti, ambayo yanaonesha maendeleo mapya kabisa ya utafiti wa chanjo za Ukimwi pamoja na matokeo ya upimaji wa mgonjwa aliyepewa aina mpya ya tiba ya Ukimwi, tiba hiyo inahamasisha mfumo wa kinga wa mgonjwa kugundua na kuua virusi vya Ukimwi. Chanjo za aina hiyo zinafanya mfumo wa kinga mwilini kuwa na chembechembe zenye uvimbe, mfano wa mti kuwa na mafundo yanayojitokeza, chembechembe hizo ni kama "wauaji" wa virusi vya Ukimwi. Imekadiriwa kuwa chanjo ya aina hiyo inatazamiwa kuingia hatua ya kufanya majaribio mwishoni mwa mwaka huu. Mbali na hayo, chanjo ya aina moja ya Ukimwi iliyotengenezwa na kampuni ya dawa ya Merck pharmaceuticals hivi sasa inafanyiwa majaribio ya kipindi cha mwisho kwa watu 500 waliojitolea wa nchi za Amerika ya kusini na sehemu ya Caribbean, na takwimu za mwisho zinatazamiwa kutolewa mwaka 2007, hiyo ni chanjo yenye matumaini makubwa zaidi kwa hivi sasa. Hivi sasa taasisi za Afya ya Marekani zinafanya majaribio ya chanjo kwa watu 500 waliojitolea wanaotoka Amerika ya kaskazini, Amerika ya kusini, Afrika na sehemu ya Caribbean. Harakati za utengenezaji wa chanjo ya Ukimwi duniani zinakadiria kuwa, aina moja ya chanjo ya Ukimwi hata kama ufanisi wake ni asilimia 40, inaweza kupunguza ongezeko la watu milioni 1 wanaoambukizwa virusi vya Ukimwi kwa mwaka kabla ya mwaka 2020.

Mwenyekiti wa harakati za kutafuta chanjo ya Ukimwi duniani Bw. Seth Berkley anaona kuwa, chanjo ya Ukimwi itakayouzwa inatakiwa kuzinufaisha nchi zinazoendelea. Alisema "muundo wetu wa utafiti unasaidiwa na fedha za shirika la utoaji misaada, kwa hiyo tutazungumza na kampuni za dawa, kuzishawishi kwa mafanikio ya utafiti, tunazitaka kuwekeza kwa uzalishaji chanjo na kukubali masharti ya kuuza chanjo kwa bei rahisi, na kutoa chanjo kwa nchi zinazoendelea kwa idadi, bei na wakati za mwafaka. Endapo kampuni hizo zitabadilisha nia, basi tuna haki ya kutafuta kampuni nyingine za kutengeneza chanjo za aina hiyo."