Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-08-17 16:08:45    
Siku ya wapendanao ya China yasaidia kueneza utamaduni wa jadi wa kimapenzi

cri

Siku ya wapendanao ya China, ambayo kwa Kichina inaitwa siku ya Qixi, ni siku ya tarehe 7 ya mwezi wa 7 kwenye kalenda ya Kichina. Sikukuu hiyo inatokana na hekaya moja ya China kuhusu mvulana aliyekuwa anachunga ng'ombe aitwaye Niulang na binti wa mfalme wa peponi aitwaye Zhinu, wapenzi hao wawili walifunga ndoa kisirisiri, lakini baadaye walitenganishwa na malkia, wakalazimishwa kwenda kuishi katika nyota mbili za Altair na Vega zilizo kando mbili kilimia. Na kila ifikapo tarehe 7 mwezi wa 7 kwenye kalenda ya Kichina, wapenzi hao wawili hukutana kwa kupitia daraja linalojengwa kwa ndege aina ya magpie.

Mwandishi maarufu wa vitabu wa China Bw. Feng Jicai alisema, "Siku ya Qixi inaonesha vitu vinavyozingatiwa kuhusu uhusiano wa kimapenzi katika utamaduni wa jadi wa China, vitu hivyo ni wapenzi wanapaswa kuishi kwa pamoja mpaka mwisho na kuwa waaminifu bila kujali matatizo gani yanayowakabili."

Katibu mkuu wa Shirikisho la wasanii wa fasihi na sanaa za jadi ya China Bw. Huo Shangde alisema hivi sasa idadi ya talaka nchini China inazidi kuongezeka, ambapo ndoa za sasa zinaonekana kuwa ni dhaifu na zinavunjika upesi. Akichambua alieleza sababu mbili kuwa, upande mmoja wa wanandoa, ama mume au mke wanakiuka msingi wa maadili na kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa, na sababu nyingine ni tofauti kubwa kati ya mume na mke katika kazi na uwezo wa kiuchumi, hali ambayo inasababisha kupotezwa kwa mambo yanayofuatiliwa nao kwa pamoja.

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Wizara ya mambo ya kiraia ya China zinaonesha kuwa, mwaka 2005 ndoa zipatazo milioni 1.785 zilivunjika, kiasi ambacho ni asilimia 2.73 kati ya familia zote nchini China, ambalo ni ongezeko la asilimia 0.17 kuliko mwaka 2004.

Bw. Huo Shangde alisema utamaduni wa siku ya Qixi unatokana na hadithi ya mapenzi kati ya Niulang na Zhinu, uhusiano wa jadi wa kimapenzi unasaidia kuhimiza masikilizano ndani ya familia. Alieleza maoni yake kuwa, kueneza utamaduni huo wa jadi ni hatua yenye ufanisi ya kubadilisha hali ya kuongezeka kwa idadi ya talaka nchini China. 

Je, utamaduni wa siku ya Qixi maana yake ni nini? Mtaalamu mwingine wa China Bw. Wang Chuguang alisema utamaduni huo unahusiana na familia, na unaonesha uhusiano imara wa kimapenzi. Katika hadithi hiyo, vijana hao wawili walipendana kwa moyo wa dhati, ambapo msichana Zhinu alikiuka nidhamu ya peponi akaolewa na mvulana wa duniani. Wao waliweka mfano wa kuigwa kwa watu wote. Mtaalamu huyo alichambua akisema, kutokana na hadithi hiyo inafahamika kuwa mbali na kupata manufaa kutoka kwa uhusiano wa kimapenzi, watu pia wanapaswa kutoa mchango wao. Aidha hadithi hiyo inasifu sana uhusiano wa kimapenzi unaodumu, kwani ingawa vijana hao wawili walitenganishwa na kukutana mara moja tu kila mwaka, uhusiano wa kimapenzi kati yao haukubadilika hata kidogo.

Ilipokaribia tarehe 31 Julai, ambayo ilikuwa siku ya Qixi kwa kalenda ya Kichina mwaka huu, harakati mbalimbali zilifanyika nchini China kuadhimisha siku hiyo.

Mjini Nanjing jumla ya ndege 770,000 zilizotengenezwa kwa karatasi za rangi mbalimbali zilitumika kupamba lango ya Zhonghua, ambayo ni lango maarufu ya kale mjini humo, ili kuutakia mji huo bahati njema katika mambo ya kimapenzi.

Huko Chengdu, mji mkuu wa mkoa wa Sichuan, kusini magharibi mwa China, vijana 40 waliovaa nguo za jadi za enzi ya Han ya China waliadhimisha siku ya Qixi tarehe 30 Julai.

Kwa mujibu wa kalenda ya Kichina, mwaka huu tunapitia mwezi wa 7 kwa mara mbili, kwa hiyo siku ya Qixi mwaka huu ni siku mbili za tarehe 31, Julai na tarehe 30, Agosti.

Idhaa ya kiswahili 2006-08-17