Wajumbe wa waalimu wa historia kutoka shule za sekondari na za msingi za China, Japan na Korea ya kusini hivi karibuni kwa mara ya kwanza wamefanya mkutano hapa Beijing, ambapo walibadilishana maoni kuhusu uzoefu wa mafunzo ya elimu ya historia, na kujadili masuala kadhaa yenye migongano kuhusu elimu ya historia katika nchi hizo tatu. Waalimu wa historia wa nchi hizo tatu wameona kwa kauli moja kuwa, elimu ya historia inapaswa kutolewa kwenye msingi wa kuelezea wazo la amani, na mafunzo ya historia ya zama za karibu katika nchi hizo tatu yanapaswa kutupia macho historia ya Asia ya mashariki.
Mkutano huo unalenga kupitia mafunzo mazuri ya amani yanayofuata hali halisi kuhusu historia kuzihimiza nchi hizo tatu zianzishe ushirikiano wa amani na kirafiki.
China, Japan na Korea ya kusini ni nchi jirani zenye mahusiano ya karibu ya kihistoria, kijiografia na kiutamaduni. Vita vya uvamizi vilivyoanzishwa na wababe wa kijeshi wa Japan katika muda kati ya karne ya 19 na 20 viliathiri vibaya usalama wa taifa, mamlaka ya nchi na ukamilifu wa ardhi wa China, Korea ya kusini na Korea ya kaskazini na kuleta athari ya kuangamiza kwa mambo ya uchumi na utamaduni wa nchi hizo za Asia.
Lakini katika miongo kadhaa iliyopita baada ya kumalizika kwa vita na kushindwa kwa Japan katika vita vikuu vya pili vya dunia, nguvu ya mrengo wa kulia ya Japan inafanya chini juu kukanusha na kupotosha historia na kujaribu kujitetea kwa vita vya kuzivamia nchi za nje.
Mwalimu wa historia wa Wilaya Tokushima ya Japan Bibi Mayumi Tomita ni mmoja kati ya waalimu wengi wa Japan wanaoshikilia jukumu la "kutowapeleka wanafunzi wao kwenye medani ya vita". Alisema, waziri mkuu wa Japan Bw Junichiro Koizumi mara kwa mara alikwenda kwenye hekalu la Yasukuni kutoa heshima kwa wahalifu wakuu wa vita vya pili vya dunia, kitendo chake hicho kinaweza kuwaelekeza vijana kwa makosa. Hivyo mwalimu huyo alisema, jukumu lake ni kuwaambia wanafunzi wake watoto ukweli wa mambo ya historia. Alisema:
Nataka kupitia mafunzo kuwawezesha wanafunzi waelewe ukweli wa mambo, hatupaswi kuficha ukweli wa mambo, bali tunapaswa kushikilia mafunzo hayo kwa miaka mfululizo ili wanafunzi waelewe ukweli wa mambo. Pia nimetambua kuwa ni lazima kutafuta njia moja ya kumwezesha kila mwanafunzi asiwe mtu wa Asia anayepigana na nchi nyingine, bali anapaswa kuwa mtu wa Asia anayejua kuishi pamoja na watu wengine kwa amani.
Mwalimu wa historia wa shule ya sekondari ya mtaa wa Haidian mjini Beijing Bibi Xie Qun alisema:
Tunatakiwa kutambua ukweli wa mambo ya historia bila kuficha. Tunapaswa kuwawezesha wanafunzi wetu waelewe hali halisi ya historia ili wajue kufikiri na kutathimini kwa mitizamo yao wenyewe, kuwaacha vijana na watoto wetu wapiganie lengo la pamoja la binadamu, na kujua kuheshimu historia, hayo ni matumaini ya pamoja ya waalimu wa nchi mbalimbali.
Na mwalimu wa historia wa shule ya msingi kutoka Korea ya kusini Bwana Bae Neung-Jae alisema:
Kupotosha historia ni vitendo vya umwamba na ubabe wa kijeshi, kutambua historia kutoka kwa maslahi ya nchi moja kunaweza tu kusababisha mapigano ya kimwamba kati ya nchi na nchi. Katika miaka 100 iliyopita, tumechoshwa na madhara ya mapigano hayo. Kihistoria, tunapaswa kuwawezesha watoto wetu wapiganie lengo la pamoja la binadamu katika karne ya 21 na kuishi pamoja kwa amani kwa binadamu wote, kufuata haki na uhalali na kuwa mabwana wa jamii ya siku za usoni.
Mwaka jana wasomi zaidi ya 40 wa China, Japan na Korea ya kusini walitunga pamoja "Historia ya zama za karibu ya nchi tatu za Asia ya mashariki", kwenye mkutano huo, walimu wa historia wa nchi hizo tatu wamesifu sana kitabu hicho cha mafunzo.
|