Miongoni mwa wagonjwa wa Ukimwi karibu milioni 40 duniani, ni wagonjwa karibu 10% tu ambao wanapata fursa ya kutumia dawa, na wengi wa wagonjwa hao wanaishi katika nchi zilizoendelea. Mkutano wa 16 kuhusu ugonjwa wa Ukimwi duniani, ambao unaendelea kufanyika huko Toronto, Canada, umetoa wito wa kutaka nchi zilizoendelea kutekeleza ahadi zao za kutoa dawa na misaada ya fedha kwa nchi zinazoendelea, na kupunguza bei za dawa za Ukimwi ili kuwawezesha wagonjwa wote wapate dawa.
Mwenyekiti wa mkutano huo wa Ukimwi Bw. Mark. Wainberg alisema, lengo la mkutano ni kuhimiza haki sawa.
"Kila mgonjwa wa Ukimwi anatakiwa kupata tiba ya dawa bila kujali kama ana uwezo wa kulipa gharama ya tiba, hii ni haki yake, wala siyo haki maalumu."
Mwishoni mwa mwaka 2003, shirika la afya duniani, WHO na Umoja wa Mataifa vilianzisha kampeni ya "3 kwa 5", ikiwa na lengo la kutoa tiba kwa wagonjwa milioni tatu wanaoishi katika nchi zenye pato la chini na wastani ifikapo mwishoni mwa mwaka 2005.
Mkurugenzi wa ofisi ya Ukimwi ya WHO Bw. Kevin De Cock alisema, ingawa hivi sasa bado wako mbali sana na lengo la wagonjwa milioni 3, lakini hali ya kufurahisha ya tiba ya wagonjwa wa Ukimwi wakaoishi katika nchi zenye pato la chini na wastani imeonekana. Alisema,
"Katika sehemu ya kusini mwa jangwa la Sahara, ambayo Ukimwi umeenea zaidi, wagonjwa zaidi ya milioni 1 wamepata tiba, idadi hiyo imeongezeka kwa mara 10 kuliko ile ya kabla ya miaka 3 iliyopita. Hivi sasa idadi ya wagonjwa wa barani Afrika wanaopata tiba inachukua 63% ya jumla ya idadi ya wagonjwa wanaoishi katika nchi zenye pato la chini na wastani. Katika bara la Afrika, ongezeko la idadi ya wagonjwa wanaopata tiba imeongezeka zaidi ya mara 3.
Ili kusaidia wagonjwa wa Ukimwi wanaoishi katika nchi zenye pato la chini na wastani kupata tiba, gharama ya tiba ya wagonjwa wa Ukimwi imeongezeka mara dufu kuliko ile ya kabla ya miaka 3 iliyopita, ambapo gharama ndogo kabisa ya dawa ya mgonjwa wa Ukimwi imepungua kwa dola za kimarekani 130 hivi kwa mwaka, lakini hata hivyo bado kuna baadhi ya wagonjwa wa Ukimwi wanashindwa kumudu gharama ya dawa za Ukimwi.
"Vikwazo muhimu ni: usajili wa dawa mpya katika baadhi ya nchi unafanyika polepole sana, kupinga kulipa ushuru wa forodha kwa dawa za Ukimwi na kutoweza kutumia vizuri vifungu husika vya mkataba wa hifadhi ya haki-miliki ya kielimu."
Kifungu hicho kinaagiza kuwa, nchi zilizoendelea wanachama wa shirika la biashara duniani, WTO na nchi wanachama zilizoko nyuma kabisa kimaendeleo zinapokumbwa na mgogoro unaotishia afya za umma, ambazo ni pamoja na ugonjwa wa Ukimwi, malaria na kifua kikuu, zinaweza kutekeleza uidhinishaji wa kulazimisha bila kibali cha mwenye hataza, kuruhusu viwanda vyake kuzalisha dawa, kutumia na kuuza dawa zenye hataza ya watu wengine. Endapo zinaweza kutumia vizuri kifungu hicho, basi zitaleta manufaa makubwa kwa wagonjwa wa nchi zake. Serikali ya Brazil mapema katika mwaka 2001, ilitumia kifungu hicho, ikitangaza kuzindua uidhinishaji wa lazima, na kuzalisha dawa ya Ukimwi, ambayo kampuni moja ya dawa nchini Uswisi inamiliki hataza, hatua ambayo iliilazimisha kampuni hiyo ya dawa ya Uswisi kuuza dawa hiyo nchini Brazil kwa kupunguza bei kwa 40%.
Vyombo vya habari vinasema hatua zinazopigwa na nchi zilizoendela kuzisaidia nchi zinazoendelea na nchi maskini ni za taratibu sana. Hivi karibuni serikali ya Canada ilikosolewa kwa kutotekeleza ahadi zake za kusafirisha dawa za Ukimwi za bei rahisi kwa nchi za Afrika.
|